Sababu mwenza kuwaficha watoto wa nje

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa wanasaikolojia, kati ya mambo yanayosababisha wenza kuficha ukweli juu ya kuwa na watoto ni kutokana na baadhi ya watu kuamini waliowahi kupata watoto hawawezi kuachana.

Hofu ya kuachwa na mwenza inaelezwa ni moja kati ya sababu ya mwanamke au mwanamume kuficha kama ana mtoto anapoingia katika uhusiano mwingine.

Kwa mujibu wa wanasaikolojia, kati ya mambo yanayosababisha wenza kuficha ukweli juu ya kuwa na watoto ni kutokana na baadhi ya watu kuamini waliowahi kupata watoto hawawezi kuachana.

Katika mahojiano yake na Gazeti la Nation, Zipporah Kimani ambaye ni mtaalamu wa masuala ya familia, anasema kuna mambo kadhaa yanayowafanya baadhi ya watu, hasa wanawake kutokuwa wawazi kwa wenza wao kuhusu watoto waliopata katika uhusiano uliopita.

Kimani anasema moja ya sababu ambazo mara nyingi huwakumba wanawake ni namna gani amtambulishe mtoto wake kwa mwanamume mwingine atakayekwenda kumuita baba, hasa kama bado mzazi wa mtoto huyo anaendelea kutoa pesa za matumizi na mahitaji mengine kwa mtoto.

Pia, anasema baadhi ya wanaume katika jamii huamini kuwa mwanamke kupata mtoto kabla ya kuolewa ni ishara kuwa mwanamke huyo alikuwa akijihusisha na vitendo visivyo na maadili, hivyo kutilia shaka maadili yake.

“Kwa mtu aliyebakwa na akapata ujauzito anaweza kupitia katika changamoto mbalimbali za kisaikolojia kama vile maumivu, majuto, fedheha, kujidharau, mtoto anaweza kuwa ukumbusho wa mara kwa mara wa yale aliyopitia,” anasema Kimani.

Sababu nyingine zilizoelezwa na Kimani ni pamoja na hofu ya watoto kupitia unyanyapaa na ubaguzi kutoka kwa mwenza mpya, pengine mtoto amezaliwa na ulemavu na jamii anayoishi ikiwa bado inashikilia mila potofu dhidi ya watoto wanaozaliwa na ulemavu.”

Hata hivyo, Kimani anashauri wanawake na wanaume kutowaficha wenza wao wapya ukweli kama tayari una mtoto mwanzoni kabisa wanapoamua kuanzisha mahusiano.

“Kama unawapenda watoto wako huwezi kumficha kwa sababu yoyote ile,” anasema mshauri huyo wa familia.


Simulizi ya waliopitia mkasa huo

Abdul Msangi, mkazi wa Chanika jijini Dar es Salaam anasimulia namna alivyoingiwa na hofu ya kumpoteza mwenza wake mpya kama angemueleza ukweli kuwa aliwahi kupata mtoto mmoja katika uhusiano uliopita.

Anasema hofu yake ilianza kujengeka kutokana na mwenza wake ambaye sasa ni mkewe kusisitiza mara kwa mara katika mazungumzo yao kuwa asingependelea kuwa katika uhusiano na mwanamume ambaye tayari alishakuwa na mtoto.

“Mara nyingi alikuwa akiniambia hofu yake kuwa atakapoolewa na mwanamume mwenye mtoto, mwanamke aliyezaa naye anaweza kutumia kigezo cha mtoto kuwa karibu na mzazi mwenzie na hata pengine kurudiana,” anasema Msangi.

Kutokana na hali hiyo, anasema ilimlazimu kuficha ukweli huo kwa mwenza wake kwa muda huku akiwa anamuweka sawa kisaikolojia na kumuondoa hofu na dhana ambayo mwenza wake alijijengea akilini mwake ili atakapomueleza suala hilo iwe rahisi kulipokea.

“Japokuwa baada ya mwenza wangu kufahamu ukweli, ulizuka mgogoro kwa siku kadhaa lakini baadaye alinielewa na hadi sasa tunamlea mtoto pamoja.”

Juma Mashaka anasema alilazimika kumficha ukweli mkewe kwa muda wa takribani miaka mitatu kuwa alipata mtoto nje ya ndoa kwa kuhofia mgogoro katika familia yake.

“Nilikuwa nikitafakari nitawezaje kumwambia jambo hili na akanielewa bila kusababisha migogoro, japokuwa kutokana na visa na vitimbi kutoka kwa mwanamke niliyezaa naye, mke wangu alifahamu na kuibua mzozo mkubwa, japo baadaye alielewa na kumpokea mtoto,” anasema Mashaka.

Kwa upande wake Mariam Kalinga (si jina halisi) mkazi wa Iringa anasimulia namna familia yake ilivyomsukuma kuficha mtoto pindi alipokuwa anataka kuchumbiwa na mume wake wa awali ambaye kwa sasa ni marehemu.

Anasema baadhi ya sababu alizokuwa akielezwa na familia yake ni kuwa atakaposema aliwahi kupata mtoto pindi alipokuwa shuleni pengine mwanamume anayetaka kumuoa angemtafsiri kama mwanamke ambaye hajatulia.

“Pia, walisema akifahamu kuwa tayari alishawahi kuwa na mtoto anaweza asikubali kulipa kiwango cha mahari alichopangiwa kutokana na kuwa nilikuwa bado mdogo, ilinilazimu kukubaliana nao japo nilikuwa na maumivu moyoni kwa kuwa nilifanya bila ya ridhaa yangu,” anasema Mariam.

Pia, anasema baada ya kukubaliana na familia na taratibu za ndoa kukamilika alilazimika kwenda kuishi Dar es Salaam na kumuacha mtoto kijijini akilelewa na bibi yake.

“Baada ya kukaa kwa muda wa takribani mwaka mmoja uzalendo ulinishinda na nikaliweka hilo bayana kwa mume wangu ili niweze kuwa karibu na mwanangu na kumlea, japokuwa baada ya kufahamu alijawa na jaziba na kuhoji kwa nini sikumuweka bayana kile kinachoendelea tangu mapema, lakini alielewa na kukubali kumlea mtoto.”


Wanajamii wanazungumziaje

Sharifa Salum, mkazi wa Gongolamboto anasema hakuna sababu za msingi za kuficha mtoto kwa kuwa kama mtu amekupenda kweli basi hiyo haiwezi kuwa sababu ya msingi ya kukatisha uhusiano au kuvunja ndoa.

“Waswahili husema ukipenda boga basi penda na ua lake, hivyo kama mtu amekupenda kwa dhati basi atampenda, kumjali na kumtunza mtoto au watoto wako kama anavyofanya kwako,” anasema Sharifa.

Joseph Kaniki anasema baadhi ya wanaume huwa na hofu ya kuingia katika uhusiano na wanawake ambao tayari wana watoto kwa kuhofia pengine mtoto anaweza kuwa sababu ya wenza hao kuwasiliana mara kwa mara na pengine hata kurudiana.

“Baadhi ya wanaume pia huwa wanahofia kuongeza mzigo wa malezi kama wakiingia katika uhusiano na mwanamke ambaye tayari ana watoto”.


Wanachosema wanasaikolojia

Mtaalamu wa Saikolojia, Charles Mhando anasema ni kweli katika jamii wapo baadhi ya watu huwa wanaficha ukweli kuwa waliwahi kupata mtoto au watoto pale wanapoingia katika uhusiano mapya.

Mhando anasema hilo linaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, ikiwamo kuhofia kuvunjika kwa uhusiano wake.

“Pengine mwanamke au mwanamume aliwahi kuanzisha uhusiano na mtu mwingine na baada tu ya kugundulika kuwa na mtoto, labda uhusiano ulilegalega au kuvunjika, mtu aliyepitia hali hii huenda akaingiwa na hofu kwa yale yaliyomkuta awali, hivyo anapoingia katika uhusiano kwa mara nyingine anaweza kuficha ukweli kuwa aliwahi kupata mtoto,” anasema Mhando.

Mhando anasema jambo jingine linalosababisha wenza kuficha ukweli juu ya kuwa na watoto ni kutokana na baadhi ya watu kuamini waliowahi kupata watoto hawawezi kuachana.

Hata hivyo, Mhando anasema kuficha ukweli kuwa una watoto unapoingia katika uhusiano mpya inaweza kumfanya mtoto kukosa baadhi ya haki zake.

Mwanasaikolojia na Mchambuzi wa Masuala ya Kijamii, Charles Nduku anasema tabia ya kutoeleza ukweli juu ya kuwa na mtoto pale unapopata mwenza mpya si jambo zuri, kwa kuwa utakapogundulika unaweza kuleta athari, ikiwamo mifarakano kwa wenza au kwa mtoto husika.

Anasema mwanamke au mwanamume anapoficha ukweli ana mtoto baadaye ukweli ukajulikana unaweza kufanya hata uaminifu ukapungua au kutokuwepo kabisa katika uhusiano huo.

“Anaweza fikiri kama ameweza kumficha kuwa aliwahi bahatika kupata mtoto awali basi anaweza hisi yapo mengine mengi ambayo mwenza wake anayafanya bila ya yeye kufahamu na kusababisha uaminifu kupungua,” anasema Mhando.

Anasema pamoja na kusababisha migogoro, tukio hilo linaweza kumnyong’onyeza mtoto aliyefichwa na kujiona kuwa hathaminiki na mzazi wake.

“Pindi mtoto anapogundua mzazi wake hajisikii fahari kusema kwa watu wengine kuwa yule ni mtoto wake, inaweza kumsababishia athari mbalimbali za kisaikolojia, ikiwamo msongo wa mawazo, manung’uniko na hata kupunguza uwezo wake wa kujiamini,” anasema Mhando.

Hata hivyo, alishauri kwa wenza pale wanapoingia katika uhusiano mwingine kuwa wakweli kama waliwahi kubahatika kupata watoto katika uhusiano wa awali ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza baadaye na hata kupoteza mapenzi na uhusiano wa karibu na watoto wao.


Vipi kuhusu ustawi wa jamii

Ofisa Ustawi wa Jamii, Dk Zena Mabeyo anasema kitendo cha mzazi kumficha mwenza wake kama ana mtoto kunaweza kumuathiri mtoto katika ukuaji wake kimwili, kiakili, kifikra na kihisia.

Dk Mabeyo, ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo cha Ustawi wa Jamii anasema ili mtoto aweze kukua vyema anahitaji kuwa karibu na mzazi au wazazi na inapotokea mzazi huyo hana ukaribu na mtoto huweza kuathiri ukuaji wake.

“Kukosa ukaribu kati ya mzazi na mtoto husababisha mtoto kukosa upendo wa karibu na mzazi wake na anapogundua kuwa mzazi alimtelekeza humpunguzia mtoto uwezo wa kuwa na imani na upendo kwa wengine,” anasema Dk Mabeyo huku akishauri mzazi anapoanzisha uhusiano mwingine kuwa muwazi kwa mwenza wake ili kulinda masilahi ya mtoto.