Bashiru atawashinda wapinzani kwenye uwanja uliojaa mbigili

Katibu Mkuu CCM, Dk Bashiru Ally amekuwa akitamba kuwa chama chake kutaibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao baadaye mwaka huu.

Katika vikao vyake vya ndani na mikutano ya hadhara anayofanya maeneo mbalimbali nchini katika ziara zake anazoita “za kufunga na kutesti mitambo” Mtendaji huyo mkuu wa chama tawala anatamba kuwa ushindi huo utafanana na ule ambao chama chake kilipata kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 24, 2019.

Dk Bashiru, mhadhiri wa zamani wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amerejea tambo hizo Januari 19, 2020 wakati wa majumuisho ya ziara yake ya siku tatu mkoani Kigoma.

Akiwa huko hakumung’unya maneno akitamba kuwa CCM italinyakua Jimbo la Kigoma Mjini linaloongozwa na Zitto Kabwe kwa tiketi ya ACT-Wazalendo.

Tambo za Dk Bashiru kuwa CCM itashinda kama ilivyofanya kwenye Serikali za mitaa zinaibua hofu miongoni mwa washiriki wengine wa uchaguzi ujao kutokana na kumbukumbu ya ‘figisufisu’ na rafu zilizodaiwa kufanyika katika uchaguzi huo uliofanyika chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Katika uchaguzi huo, wapinzani walianza kulia kuchezewa rafu kuanzia hatua ya kuandaa kanuni, kuchukua na kurejesha fomu Oktoba 29, 2019 baada ya wasimamizi wasaidizi kudaiwa kufunga ofisi kukwepa kutoa na kupokea fomu za wagombea wa vyama vya upinzani.

Waliendelea kulalamika kuwa wagombea wa upinzani waliofanikiwa kuchukua na kurejesha fomu pia walikumbana na rungu la kuenguliwa kwa sababu zisizo na mashiko, ikiwemo makosa ya kisarufi.

Wapo walioenguliwa kwa kudaiwa kukosea kujaza taarifa kuhusu kazi halali ya kipato, eneo wanaloishi na kugombea na kuwa na tuhuma za kesi za jinai katika vituo vya polisi.

Kutokana na kutoridhishwa na mchakato wa uchaguzi huo, vyama vikuu vya upinzani vilijitoa kwenye uchaguzi wa wenyeviti wa vijiji, mitaa, vitongoji na wajumbe wa Serikali za vijiji/mitaa na hivyo kufanya CCM kushinda kwa zaidi ya asilimia 99.

Ukiacha uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa, mfano mwingine wa CCM kushinda kwa kishindo ni kupitia chaguzi ndogo zote zilizoitishwa ndani ya miaka minne iliyopita,

ambapo kilishinda huku wapinzani wakilia kufanyiwa rafu, ikiwamo mawakala wake kunyimwa vibali na mahali pengine matokeo kutangazwa tofauti na kura za kwenye sanduku.

Hata hivyo, mazingira hayo yote yamekuwa yakitetewa na viongozi wa CCM kuwa ni sehemu ya mchezo wa siasa.

Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli alikipongeza chama hicho kwa ushindi mnono wa mitaa, akisema “hata waliojitoa nayo ni demokrasia”.

Ni kutokana na mazingira hayo, Wakili wa kujitegemea, Majid Kangile wa jijini Mwanza anasema ingekuwa siasa ni ulingo wa masumbwi, CCM ingefananishwa na bondia anayepambana na wenzake waliofungwa mikono.

“Kwa mujibu Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992 na marejeo yake yote kuanzia mwaka 2002, vyama vya siasa vinapewa haki sawa ya kufanya shughuli za siasa ikiwemo mikutano ya hadhara kwa lengo la kueneza sera kushawishi uungwaji mkono miongoni mwa wananchi.

“Lakini sheria hiyo inakanyagwa, CCM inaruhusiwa kufanya siasa kupitia viongozi wake na wale wa Serikali wenye vyeo vya kisiasa, huku vyama vingine vikizuiwa,” anasema wakili huyo.

Anasema hata vyombo vya dola vinavyotakiwa na sheria kujiepusha na siasa, vimejikuta vikijiingiza ama kwa kutojua, kuelekezwa au kujipendekeza kwa mamlaka, kwa kuzuia isivyo halali shughuli za kisiasa, vikiwemo vikao vya ndani vya vyama vya upinzani ambavyo havihitaji vibali wala taarifa ya polisi.

“Kisheria tuna usemi kuwa haki siyo tu inatakiwa kutendeka, bali inatakiwa ionekane ikitendeka. Malalamiko ya vyama vya upinzani kutotendewa haki inaibua hofu tunapoelekea uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu,” anasema Wakili Kangile

Uchaguzi huru na haki

Ili kuondokana na matatizo yanayoshuhudiwa katika ulingo wa siasa nchini, Wakili Kangile huyo anashauri pawepo utashi wa kisiasa katika kufuata na kuheshimu misingi ya sheria na haki kwa wote.

“Haki, usawa kwa wote, kuheshimiana, utu na uzingatiaji wa Katiba, sheria na kanuni ndizo nguzo kuu itakayotuhakikishia na kutuwezesha kuwa na uchaguzi huru, wa haki, unaokubalika na kuheshimika, si tu machoni mwa Watanzania, bali pia kwa Jumuiya za Kimataifa,” anasema.

Zitto asema imetosha

Akizungumzia zuia la shughuli na mikutano ya kisiasa ya vyama na viongozi wa upinzani, Zitto anasema “Kwa miaka minne sasa vyama vya siasa vya upinzani vimezuiwa kufanya shughuli za siasa kwa uhuru kama inavyoruhusiwa na sheria za nchi yetu. Hata wabunge tunapata wakati mgumu kufanya mikutano kwenye maeneo yetu ya uwakilishi. Sasa imetosha.”

Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo anasema vyama vya upinzani kikiwemo anachokiongoza, vimelalamikia vitendo hivyo kwa kipindi kirefu bila mafanikio.

“Tumefungua mashtaka mahakamani hayaishi na mengine yanatupwa. Tumefanya kila juhudi. Sisi kama chama (ACT-Wazalendo) tutaanza mikutano yetu bila kujali zuio la Serikali. Mara baada ya mkutano mkuu wa chama mwezi Machi 2020, tutaanza kufanya mikutano kwa mujibu wa sheria na kupuuza maagizo haramu. Tumechoka kuonewa.”

Mkutano wa Zitto umezuiwa siku tatu tangu Jeshi la Polisi Wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba kumuhoji mshauri mkuu wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad na Mwenyekiti wa kamati ya uhusiano wa chama hicho, Salim Bimani kwa tuhuma za kufanya mkutano wa hadhara.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani humo, Juma Sadi Khamis, viongozi hao wanadaiwa kufanya mkutano wa hadhara katika Shehia ya Kiuyu, Wilaya ya Micheweni, Desemba 9, mwaka jana.

Maalim Seif amekanusha madai hayo akieleza kuwa alifanya vikao vya ndani na mazungumzo na baraza mbalimbali za chama zinazolenga kujiimarisha kuelekea uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.

Akizungumzia kuhojiwa kwao, Bimani anasema; “kinachofanywa kwenye siasa za Tanzania hususani Zanzibar kinashangaza; hivi karibuni vijana wa CCM waliandamana maeneo yote ya Unguja bila ya kuulizwa lolote, huku wakichana bendera za chama chetu.

“Kwa mazingira haya, ni wazi watawala na vyombo vingine vimeamua kufanya kazi ya kukandamiza upinzani.”

Akizungumzia mikakati ya kukabiliana na hali hiyo, Maalim Seif anasema; “Sitasita kufanya siasa na ataendelea na shughuli hizo kama kawaida.”

Suala la Maalim Seif liliibia utata pale Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alipoeleza kushangaa polisi kutozuia mikutano ya kiongozi huyo Pemba, huku kamanda wa polisi wa eneo hilo alisema uchunguzi unaonyesha hakuna kosa lililofanyika lakini msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alisema, “Jeshi la Polisi limepokea maelekezo ya Masaunina limeanza kuyafanyia kazi.”