Mjadala wa mamlaka ya ma-DC, ma-RC umeibuka tena

Rais John Magufuli akizungumza katika kikao kilichowahusisha wakuu wote wa mikoa pamoja na makatibu tawala wa mikoa kilichofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam, Desemba mwaka jana. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Waziri Mkuchika ameonesha hisia zake Februari 07, 2019 alipokuwa akilihutubia Bunge. Amewakemea wakuu wa mikoa na wilaya kwa namna wanavyoitumia vibaya Sheria inayowapa mamlaka ya kuwaweka ndani raia pale ambapo wataamini raia hao wanahatarisha amani.

Wiki hii mjadala wa mamlaka ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuwakamata watu na kuwaweka ndani kwa saa kadhaa umerejea tena. Mara hii aliyeurejesha ni waziri mwenye dhamana ya masuala ya Utawala Bora nchini Tanzania, George Mkuchika.

Waziri Mkuchika ameonesha hisia zake Februari 07, 2019 alipokuwa akilihutubia Bunge. Amewakemea wakuu wa mikoa na wilaya kwa namna wanavyoitumia vibaya Sheria inayowapa mamlaka ya kuwaweka ndani raia pale ambapo wataamini raia hao wanahatarisha amani.

Mkuchika anasema, “...mkuu wa wilaya kumuweka mtu ndani muda wa saa 48 ni makosa kwa sababu sheria inampa yeye (DC) saa 24, mkuu wa mkoa (RC) amepewa saa 48. Si lazima wewe (DC au RC) umuweke mtu ndani, kama ni kosa la jinai OCD yuko, kama ni suala la uhamiaji Ofisa Uhamiaji yuko, kama mtu amekwepa kodi mtu wa TRA yuko, siyo lazima utamke wewe, haya mambo si lazima utamke wewe, tuache...”

Kauli hii ya Waziri wa Utawala Bora ni mwendelezo wa kauli nyingi za viongozi wakubwa wa serikali ambao wamewahi kuonyesha hisia zao hadharani, kwamba wakuu wa mikoa na wilaya wanaitumia sheria hii vibaya.

Sheria yenyewe inasemaje?

Mamlaka ya Mkuu wa Mkoa na Wilaya kuagiza kukamatwa kwa mtu na kuwekwa rumande yanapatikana kwenye vifungu vya 7 (mamlaka ya mkuu wa mkoa) na 15 (mamlaka ya mkuu wa wilaya) vya Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997.

Vifungu hivi vinawapa viongozi hawa mamlaka ya kukamata au kuagiza kukamatwa kwa mtu yeyote ambaye watadhani anatenda kosa au alitenda kosa ambalo linamfanya mtu huyo kuweza kukamatwa na kushtakiwa na kwamba kama wakuu hawa wakiamini kuwa mtu yeyote anaweza kuvunja amani au kuharibu utulivu...na uvunjifu huo hauwezi kuzuiwa kwa njia yoyote nyingine isipokuwa kumsweka rumande mtu huyo.

Vifungu hivyo vyote vinaendelea kusisitiza kuwa mtu aliyekamatwa kwa amri au maelekezo ya Mkuu wa Mkoa au Wilaya anapaswa kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24 au 48 kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka ya jinai. Endapo hatafikishwa mahakamani kwa muda unaopaswa, na muda kuisha, anapaswa kuachiwa na hapaswi kukamatwa tena kwa namna ileile.

Sheria hii imeweka utaratibu zaidi wa namna ya kumfikisha mhusika mahakamani, kwa bahati mbaya wakuu wa mikoa na wilaya wanaotumia mamlaka haya kuwaweka ndani raia huwa hawafuati na au hawasomi mahitaji ya sheria hii hata kidogo.

Wito wa JPM

Hawa wote ni viongozi wenye mamlaka mbalimbali katika nchi yetu ambao walau wamejitokeza hadharani na kueleza kutoridhishwa kwao na namna wakuu wa mikoa na wilaya wanavyotumia sheria hii vibaya.

Rais JPM alifanya hivyo Januari 29, 2019 wakati akiwaapisha majaji 21 wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani kwa pamoja Ikulu jijini Dar es Salaam. JPM alinukuliwa akiwaeleza wateule wake ya kwamba “kuelekeza kunaweza kuwa na matokeo chanya wakati mwingine kuliko hata kuweka watu ndani.”

Mawaziri Lugola, Jaffo

Kama hiyo haitoshi, Agosti 28, 2018, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alieleza kutoridhishwa kwake na namna wakuu wa mikoa na wilaya wanavyoitumia sheria hii ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1977 na kuwataka kutowaonea wananchi.

Lugola alinukuliwa akisema “Hayo mambo yako kisheria na hiyo sheria ina vigezo vyake na kama vimetimia, watakuweka ndani. Kama DC ameona huyu tusipomweka ndani usalama wake utakuwa hatarini, lazima atakuweka,” akaendelea, “Lakini siyo mtu yuko kwenye mkutano ameuliza swali ambalo DC anaona linaleta challenge (changamoto), anasema huyo weka ndani saa 48. Hilo halitawezekana, katika Serikali hii hatutaki wananchi wapate shida.”

Septemba 15, 2017 na Agosti 14, 2018 katika mazingira tofauti ya kikazi, waziri wa nchi, ofisi ya rais, tawala za mikoa na serikali za mitaa, Selemani Jaffo, alitoa msisitizo na onyo kwa wakuu wa mikoa na wakuu wilaya kutotumia madaraka yao vibaya katika sheria hiyo na kuwaonea wananchi.

Jaffo alisisitiza kuwa hapendezwi na tabia ya baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa kutumia vibaya mamlaka waliyonayo ya kuwaweka watu ndani. Aliwataka viongozi hao wawe wanasoma na kuzielewa sheria kabla ya kuzitumia.

Katibu Mkuu Iyombe, Mtaka

Agosti 15, 2018, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi –Mussa Iyombe aliwaonya Wakuu wa Wilaya wateule dhidi ya tabia ya kuwaweka ndani watumishi wa umma au kugombana na wawakilishi wa wananchi bila sababu.

Agosti 17, 2018 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, wakati akifunga kikao cha madaktari wa mikoa na wilaya zote nchi nzima kilichofanyika mjini Dodoma, alionesha kushangazwa sana na tabia ya wakuu wa wilaya kuwaweka ndani watumishi wa umma.

RC Mtaka alinukuliwa akisisitiza “sisi viongozi tuwalinde watumishi wetu, mimi nilipoenda kuwa mkuu wa mkoa wa Simiyu niliwaambia wakuu wangu wa wilaya kuwa sitaki kusikia mtumishi wa umma anawekwa mahabusu...kwenye mkoa wangu hutaona upuuzi huo.”

Bado tunaihitaji sheria hii?

Ni wazi kuwa kama taifa hatutaweza kuwa tunakimbizana na ma-DC na ma-RC au kuwafukuza kazi kwa sababu wameitumia sheria hii. Kwa sababu inatumia vibaya ni muhimu sasa serikali na bunge vikaweka utaratibu wa kuifanyia marekebisho kwa kufuta vifungu vya namna hii na kwamba mamlaka ya kuamrisha watu wakamatwe yaendelee kuachwa kwa vyombo vingine vya dola. Taifa letu linazo mahakama na linazo mamlaka za upelelezi ambazo zinaweza kuifanya kazi hii, tuwatue ma-RC na ma-DC mzigo huu, tuwavue kitanzi hiki.

Julius Mtatiro ni mchambuzi na mfuatiliaji wa utendaji wa Serikali barani Afrika; ni mtaalamu mshauri wa miradi, utawala na sera; pia ni mtafiti, mfasiri na mwanasheria. Simu; +255787536759 Baruapepe: ([email protected])