Vita vya ufisadi Kenya yaendelea kung’ata wakubwa

Muktasari:

  • Rais Uhuru Kenyatta ameanza kurejesha imani ya Wakenya waliokuwa wamekufa moyo kwa sababu ya ufisadi uliozidi mipaka.

Juhudi za kupambana na ufisadi zimeshika kasi. Unaweza kusema zimewaka moto. Baadhi ya mabwanyenye ambao ilikuwa vigumu kabisa kufikiria kwamba kuna siku wangelala rumande sasa ni wageni wa serikali.

Rais Uhuru Kenyatta ameanza kurejesha imani ya Wakenya waliokuwa wamekufa moyo kwa sababu ya ufisadi uliozidi mipaka.

Hata magavana hawajaachwa katika vita hivi vya kumaliza ubadhirifu wa mali ya umma. Gavana wa Jimbo la Busia, Sospeter Ojaamong’ alifikishwa kizimbani Julai 4 kujibu mashtaka mbalimbali ya ufisadi.

Ojaamong’ ambaye anahudumu muhula wake wa pili na wa mwisho kama gavana wa jimbo hilo, alifikishwa katika Mahakama ya Milimani, Nairobi akiwa amefungwa pingu.

Sasa Rais Uhuru ameonyesha kuwa uongozi wake unajali maslahi ya wananchi wa kawaida ambao wamehangaishwa kwa miaka mingi na mafisadi wanaoiba pesa za wananchi na kuwanyima huduma mbalimbali muhimu kama vile matibabu.

Rais ametuma ujumbe kwa waliokuwa wamezoea kujilimbikizia mali kupitia uporaji wa pesa za wananchi kwamba mambo yamebadilika. Rais angetaka kuacha nchi iliyonawiri. Hataki kukumbukwa baada ya 2022 kama kiongozi aliyeangusha nchi katika utawala wake wa miaka 10.

Kunaswa kwa washukiwa wa ufisadi kutaendelea hadi wote wafikishwe kizimbani. Lakini, watakutwa na hatia kweli? Nashuku. Hii ni kwa sababu, wachunguzi wa visa vya ufisadi hufanya kazi kubwa na kuzuia haki kutendwa.

Tume ya Kupambana na Ufisadi (EACC) imetuhumiwa sana kwa ulegevu wake kazini. Baadhi ya wakubwa wake wanadaiwa kuchukua hongo kutoka kwa washukiwa wa sakata za wizi wa pesa za umma.

Kwa kuwa EACC imekosa kufanya kazi yake ipasavyo, kuna juhudi katika Bunge la Kitaifa za kutaka tume hiyo ivunjiliwe mbali.

Lakini, mbali na hayo, kuna mwangaza mpya kutoka kwa Ikulu ya Rais ambayo imeanza kumulika na kutatua ufisadi tofauti na hapo awali.

Hali hii ya kupambana na ufisadi inaweza kufananishwa na kitendo cha kunyunyiza dawa sumu kwa wadudu.

Ingawa baadhi ya viongozi wamekuwa wakipinga zoezi hili la kumaliza wadudu waharibifu, Rais anaendelea kushirikiana na maofisa wake wapya kuhakikisha wezi hawawezi kufurahia mali waliyopata kihalifu.

Wanaopinga kitendo hiki dhidi ya mafisadi bado wanaamini kinamlenga Makamu wa Rais William Ruto na washiriki wake wa karibu. Lakini hii si kweli.

Gavana Ojamoong’si mshiriki wa Ruto wala yeye hatuhumiwi kuiba kwa niaba ya mwanasiasa huyo. Gavana Ojamoong’ni mwanachama wa ODM, chama kinachoongozwa na Raila Odinga. Kwa nini alishikwa ilhali si rafikiye Ruto?

Fauka ya hayo, kuna amri ya korti ya kukamatwa kwa Gavana wa Jimbo la Kiambo, Ferninand Waitutu kwa kosa hilohilo la ubadhirifu wa fedha za umma. Gavana Waititu anadaiwa amekuwa akijilimbikizia mali si haba tangu achaguliwe miezi 10 iliyopita.

Zoezi hili pamoja na maafikiano kati ya aliyekuwa waziri Mkuu Raila Odinga linaendelea na litaendelea kuzua hofu katika chama tawala cha Jubilee. Ni kwa sababu ya uamuzi wa Rais Uhuru wa kutaka kila mmoja anayeshukiwa kupora pesa za umma kuwekwa katika darubini ya uchunguzi ili mbivu na mbichi ijulikane.

Rais amemtenga mno Makamu wake na kumkumbatia Raila ambaye sasa hutumwa kila mahali kuiwakilisha serikali. Wiki bili zilizopita, Raila alitumwa na Rais Uhuru hadi Afrika Kusini katika harakati za kutafuta Amani Sudan Kusini.

Kiongozi huyo wa ODM alikutana na aliyekuwa makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar na kumshawishi azike tofauti zake na Rais Salva Kiir na kuleta Amani nchini humo.

Kabla ya kuzuru Afrika Kusini, Raila alikuwa amemtembelea Kiir na kumpa ujumbe kama aliompa Machar. Viongozi hao wawili wamekutana na kukubali kuzika tofauti zao ili nchi yao ipate Amani.

Ninapoandika makala hii, Raila na mkewe Mama Ida Odinga walikuwa ziarani India ambapo walikutana na kiongozi wa nchi hiyo, Nahendra Modi.

Raila alitumwa na Uhuru awasihi wote wanaojidanganya kwamba chama cha Jubilee kinagawanyika, kuwa wanajidanganya. Hata katibu mkuu wa Jubilee Raphael Tuju ambaye ana mazoea ya kupinga chochote kinachosemwa kuhusu chama hicho, sasa anakubali kwa haraka kwamba mambo si shwari.

Sasa ni bayana kwamba Jubilee imepasuka msamba. Jubilee sasa ni mbili. Hii si siri.

Ili kudhihirisha jinsi uhasama unavunjavunja chama hicho, mkutano wa wabunge na maseneta wa Jubilee ambao ulikuwa umepangwa kufanyika Ikulu ya Nairobi, Julai 3 ulivunjiliwa mbali wakati wa mwisho.

Wanasiasa wa mrengo wa Makamu wa Rais walitaka mkutano huo ufanyike ili kumuuliza Rais Uhuru maswali kadhaa. Walitaka kujua ikiwa kweli amevunja mkataba kati yake na makamu wake wa kumuunga mkono mwaka 2022 kama mgombea wa urais.

Mbunge mmoja wa mrengo wa makamu wa Rais alisema mkutano huo ungefanyika, kila kitu kingewekwa wazi kwa sababu hata mjinga anajua kwamba kuna shida kubwa chamani.

Ruto ana kila sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu ndoto zake baada ya Uhuru kustaafu. Mkataba wao umevunjwa kabla ya ndoto kutimia.

Ruto anajua kwamba Rais Uhuru ana mtu mbadala atakayempa Baraka zake kumrithi ama anamtayarisha kumnyonga kisiasa.

Pengine sasa Ruto anafaa kufikria jinsi kiongozi wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi alivyohisi 2012 alivyotemwa na Jubilee hata baada ya mkataba kati yake na Ruto na Uhuru.

Sasa Ruto anavaa kiatu kilekile alichokivaa Mudavadi kwani malipo ni hapa hapa duniani.

Lakini Ruto asubiri miujiza imwokoe. Anataka kufika ikulu bila usaidizi wa Uhuru ama kabila lake la Wakikuyu.

Ruto amekuwa akizuru maeneo kadha wa kadha nchini akiwa ameandamana na wanasiasa kutoka eneo la Kenya ya Kati (Wakikuyu). Lengo lake si kuungwa mkono na wanasiasa hao. Au anataka jamii yake ya Kalenjin iamini kwamba yeye bado anaungwa mkono na Wakikuyu ingawa dalili zinaonyesha kwamba mambo si hivyo.

Pia, kwa kutembea na wanasiasa hao ambao hufurahia marupurupu kutoka kwake, Ruto analenga kuwashawishi wapiga kura Wakalenjin kwamba yeye ana umaarufu zaidi kuliko hasidi wake wa kisiasa, Gideon Moi.

Mapema wiki jana, mbunge mmoja ambaye amekuwa kwenye msafara wa Makamu wa Rais alizua mzozo baada ya kukosa marupurupu yake.

Alitaka aelezwe kwa nini yeye hajalipwa ilhali wabunge wengine waliokuwa wanaandamana na Ruto walikuwa wamelipwa. Si ajabu pesa ni kiini cha mabaya yote. Watu wanauza nyoyo zao kwa sababu ya pesa.

Mpango wa Ruto wa kufanya kampeni za 2022 mapema mno ni kujitayarisha kwa vita vinavyokuja kati yake na Uhuru kuhusu uchaguzi huo.

Ruto anataka vita mno na hiyo ndiyo sababu kila siku anazuru maeneo mbalimbali akizindua mradi mmoja baada ya mwingine. Anajitafutia maarufu kupitia kwa maendeleo yanayodhaminiwa na pesa za umma.

Njia nyingine ambayo Ruto anatumia kujipatia uungwaji mkono ni kujiuza kwa wapiga kura kama anayeonewa na familia zilizoongoza Kenya tangu miaka ya 60. Anajiuza kama mtoto wa maskini ambaye anapigwa vita na kupingwa na watoto wa mabwenyenye kama vile familia ya Rais Uhuru, Mzee Daniel arap Moi na Jaramogi Oginga Odinga.

Mbali na hayo, Ruto anawatumia wakereketwa wake wa kisiasa kumshambulia Rais Uhuru kutokana na sera zake na maamuzi yanayolenga kumaliza ama kupunguza ufisadi.

Wanasiasa hao wamekuwa wakikubaliana na Rais huku wakifanya kila wawezalo kuzuia zoezi la kutathimini mali ya viongozi wa kisiasa na wafanyakazi wa serikali.

Wanasema Uhuru anamlenga Ruto katika vita dhidi ya ufisadi. Hii si kweli kama nilivyogusia hapo awali.

Si ajabu walimhusisha Muhoho Kenyatta (nduguye Rais Uhuru) na uagizaji wa sukari wenye madini yenye sumu.

Rais kwa kejeli aliwajibu, “Hata kama ni ndugu yangu, mfungeni.”

Kwa bahati mbaya marafiki wa Ruto ni hatari kwa ndoto zake. Hawajui kumtega panya ama sungura. Kumkasirisha Rais si mpango mzuri.