Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SIMULIZI ZA MUZIKI NA ANKO KITIME: Upendeleo wa udhamini unadumaza muziki

[email protected] 0763722557

Muktasari:

Hili ni moja ya matamasha mengi ya muziki yanayoendelea nchini, lakini hayapati nafasi ya kusikika kwa wananchi. Hapa niseme kitu kuhusu wafadhili maarufu wa muziki kuwa hamtendi haki. Ni aibu kuwa matamasha ya muziki wa nyumbani hutegemea ufadhili wa taasisi na balozi za nchi za nje.

Jumamosi iliyopita katika Viwanja vya Biafra, Kinondoni Dar es Salaam kulikuwa na tamasha la muziki lililoitwa Marahaba Swahili Music Festival. Tamasha hili halikuwa limetangazwa sana kutokana na kukosekana kwa ufadhili wa matangazo.

Hili ni moja ya matamasha mengi ya muziki yanayoendelea nchini, lakini hayapati nafasi ya kusikika kwa wananchi. Hapa niseme kitu kuhusu wafadhili maarufu wa muziki kuwa hamtendi haki. Ni aibu kuwa matamasha ya muziki wa nyumbani hutegemea ufadhili wa taasisi na balozi za nchi za nje.

Kwa wale waliopata nafasi kuhudhuria tamasha hili kuna mengi ambayo yalitokea tofauti kabisa na matamasha makubwa yanayofahamika na kupewa matangazo makubwa.

Kubwa la kwanza ni kuwa tamasha la Biafra halikuwa na kiingilio na huu ni mwaka wa nne linafanyika kwa mtindo huu.

Pamoja na kuwa tamasha lilikuwa ni la bure, jambo lililoonekana ni utulivu wa watazamaji wa tamasha lile. Wazazi walikuja na watoto wadogo ambao walikuwa wakishiriki kwa kuangalia na kucheza mbele ya jukwaa kwa usalama.

Miaka yote tamasha hili limekuwa na sifa hii. Utulivu huu ulionekana kila kona waliosimama na waliokaa kwenye viti wote walionekana kuwa na utulivu wa hamu ya kufaidi kilichokuwa kinaendelea jukwaani bila kuzuia wengine. Jambo jingine kubwa ni kuwa muziki wote uliopigwa jukwaani ulitokana na wanamuziki kutumia vyombo halisi ni si kwa kutumia CD. Kulikuwa na aina mbalimbali za vyombo vilivyotumiwa, ngoma za aina mbalimbali, magitaa, marimba za mkononi na za kugonga, vibuyu vilivyotumika kutoa sauti za muziki, vyombo vya kupuliza kama filimbi, saksafon, tarumbeta, manyanga njuga, na vyombo vingine vingi. Hivyo, waliopanda jukwaani walikuwa ni wanamuziki waliofanya mazoezi makali ya ala zao na muziki wao.

Kila kundi lililopanda jukwaani lilikuja na muziki wa aina yake. Kundi la kwanza kupanda jukwaani lilikuwa na wanamuziki wa kike wengi zaidi na wote walikuwa wakipiga ngoma. Ngoma zao zilikuwa za chuma na walizipiga na kucheza katika mtindo mpya kabisa katika masikio na macho ya wengi na hivyo kwa mara nyingine kuondoa dhana ya kuwa wapiga vyombo ni wanaume pekee.

Baada ya hapo palifuata muziki wa aina mbalimbali wenye mahadhi ya makabila tofauti ya Kitanzania, na hata muziki ambao ni mchanganyiko wa ngoma za makabila mbalimbali. Kama ilivyo katika matamasha yoyote ya muziki mavazi mbalimbali yenye ubunifu yalivaliwa na wanamuziki waliopanda jukwaani. Ubunifu huu ulikuwa wa Kitanzania zaidi, hivyo hakukuwa na nguo zilizodhalilisha jinsia yoyote. Hii pengine imekuwa moja ya sababu kwanini wazazi wengi huja na watoto wao katika tamasha hili. Nilimsikia mzazi mmoja akisikitika kwanini hakumleta mtoto wake afaidi onyesho. Kulikuwa na uhakika kuwa hakutakuwa na mafunzo yaliyokosa maadili katika tamasha hili. Jambo jingine ambalo lilionekana wazi katika tamasha hili ni ushirikiano wa wanamuziki. Kulikuwako na mwanamuziki wa kike kutoka visiwa vya Mayotte, alipopanda jukwaani alisindikizwa na wanamuziki kutoka shule ya muziki ya Music Mayday, alipigiwa vyombo na wanamuziki wa Tanzania, yeye mwenyewe akiwa anapiga gitaa na kuimba. Lakini katikati ya wimbo walipanda madansa kutoka kundi la Dar Creators na kuchangamsha zaidi wimbo wake. Meya kutoka mji wake ambaye alimsindikiza aliendelea kusifu kilichotokea usiku mzima.

Mambo ya wazi yaliyoonekana na kuwa muziki uliokuwa ukipigwa katika tamasha la Jumamosi ni mara chache sana kuusikia katika radio na TV za hapa nyumbani, kingine ni kuwa asilimia kubwa ya wanamuziki walikuwa vijana, jambo linalodhihirisha kuwa muziki wa kutumia vyombo utaendelea kuwapo, kinyume cha mawazo ya wengi ambayo husikika wakilalamikia hali hiyo katika vyombo vya habari. Ila jambo la kushangaza vikundi vingi vilivyopanda vimewahi kufanya maonyesho nje ya nchi yetu mara kwa mara, hata taarifa hizo tu nazo zinazimwa na vyombo vya habari, pengine ili kuendeleza dhana kuwa muziki huo hauna thamani!!!. Wanamuziki wa muziki huu umri wao hauna tofauti na wale walioko katika muziki wa Bongofleva, lakini wale huitwa wanamuziki wa kizazi kipya na hawa wa umri uleule wameondolewa kwenye kundi la kizazi kipya!!!

Kusikiliza TV na redio ni kama kuhudhuria onyesho ambapo kuna jukwaa limefungwa kwa pazia, kuna mtu anaetoa sanaa anayoitaka kutoka nyuma ya pazia, mtu huyu anaweza akaamua kutozitoa sanaa nyingine kwa visingizio kuwa hakuna cha ziada, mtazamaji ukarudi nyumbani ukiamini hilo, kumbe kaamua tu kutokuonyesha sanaa nyingine na ndicho kinachotokea nchini.

Umefika muda wa kufungua pazia kutoka nje ya boksi walilojifungia na kuruhusu kila aina ya muziki kusikika, mchanganyiko wa muziki utawezesha kuzaliwa muziki mpya zaidi kwa vijana wenye ubunifu. Haileti mantiki kupiga muziki wa kiasili wa Kinaijeria halafu muziki wa kiasili wa nchi yako unauficha. Jambo jingine vizuri kuliweka wazi ni kuwa kwa bahati mbaya asilimia kubwa ya wanamuziki maarufu lazima watoke Dar es Salaam, hii ni kutokana na mfumo ulioko wa tasnia ya muziki.

Lakini haitumii akili kubwa kujua kuwa jambo hili ni kiini macho tu, ni dhambi kuamini kuwa vijana kutoka miji na vijiji vingine nchini hawana uwezo wa kutunga na kuimba muziki utakaopendwa. Pamoja na kuwa siku hizi kuna vituo vya radio karibu katika kila wilaya, vituo hivyo hujiona bora pale ambapo vinaiga vituo vilivyopo Dar es Salaam.

Unaweza kuwasha redio ukiwa nje ya Dar es Salaam ukadhani uko Dar es Salaam, watangazaji hujitahidi kutumia hata lafudhi za watangazi wa redio za Dar, muziki uleule, vichekesho vilevile na kusahau wasanii waliopo katika wilaya na mikoa yao. Nchi nzima yenye makabila zaidi ya 120 tunaishia kucheza ngoma ya aina moja tu. Aibu!