Kocha Azam asema Simba na Yanga kitu gani?

Muktasari:

Apania kuijenga Azam kuwa ya kimataifa zaidi badala ya kuangalia Ligi Kuu.

Mwanzoni mwa Mei, mwaka huu, uongozi wa Azam FC, ulifikia makubaliano na wakufunzi kutoka nchini Hispania, Kocha Mkuu Zeben Hernandez na Mtaalamu wa Viungo, Jonas Garcia kusimamia benchi la ufundi la timu hiyo.

Makocha hao wawili, wamesaini mkataba wa mwaka mmoja kukinoa kikosi hicho msimu ujao wakirithi mikoba ya Mwingereza, Stewart Hall, aliyeachia ngazi pamoja na benchi lake zima la ufundi.

Mpango mzima ni ujenzi wa sura mpya ya timu kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu na mechi za kimataifa kwa makocha hao pamoja na kocha msaidizi, Dennis Kitambi, daktari wa timu pamoja na kocha wa makipa.

Spoti Mikiki ilivinjari viwanja vya Chamazi Complex kushuhudia mabadiliko makubwa hasa katika ujenzi wa timu ikiwa ni pamoja na uwepo wa vifaa vya kisasa vya mazoezi ikiwamo mipira ya kisasa, jezi za mazoezi na viatu.

Pia, vibao vya kunyooshea enka, mipira ya kulalia kwa ajili ya mazoezi na vifaa mbalimbali vinavyotumiwa na timu ya kulipwa.

Baada ya mazoezi ya timu hiyo yaliyoanza saa 3 asubuhi hadi saa sita adhuhuri, yenye lengo la kuangalia wachezaji na kufanya mchujo, baadaye yalifuatia mahojiano na kocha mkuu wa timu hiyo, Zeben Hernandez.

Swali: Tumesikia uko Azam FC na jopo lako, watu wanataka kujua, wewe ni nani hasa na nafasi yako ya ukocha iko vipi, kwa kifupi sana?

Hernandez: Mimi ni kocha mwenye leseni ya juu ya ukocha ya Baraza la Vyama vya Soka Ulaya (UefaPro Licence) na nimewahi kuinoa Club Deportivo Santa Ursula ya Ligi Daraja la Tatu Hispania.

Swali: Tumeshuhudia mazoezi ya nguvu na muda mrefu bila kujali jua kali, nini mkakati wako wa ujenzi wa Azam kutoka ile ya Stewart Hall hadi ya Hernandez?

Hernandez: Ndiyo nimeanza programu na hiki nilichokianza, ninataka kuona kila mchezaji anaonyesha kiwango chake. Mpango wangu ni kufanya mchujo, sasa sitaki kufanya kazi hiyo bila kuona kwanza uwezo wa wachezaji.

Swali: Hii programu ni ya muda gani?

Hernandez: Nimepanga iwe ya wiki mbili hivi na baada ya hapo nitaandaa ripoti ya nani tubaki naye na nani aachwe...Ninataka kuona Azam ikicheza mpira wa uhakika na ndiyo maana katika siku 15 ninaamini utakuwa muda mwafaka wa kutoa nafasi kwa kila mchezaji na baada ya hapo ndiyo nitajua nani wa kumkata. Lakini nimeshauri kuwa wachezaji ambao tutawaacha wauzwe kwenye timu nyingine ili waendelee kucheza huko.

Nitataka uongozi unipatie fedha za kutosha nifanye usajili wa maana. Ninataka Azam ya matokeo, uwekezaji wake lazima ufanane na soka. Nitataka fedha za kutosha kwa ajili ya kupata wachezaji makini wa kuipa Azam matokeo.

Kuna wachezaji wengi wazuri ndani na nje, hataki kuangalia Azam ya kucheza Ligi Kuu pekee, lazima tuwe na matokeo mazuri Afrika na matokeo mazuri yanajengwa na wachezaji wazuri wenye vipaji.

Swali: Nimeona vifaa vipya hapa vya mazoezi, unavizungumziaje sanjari na programu yako?

Hernandez: Vifaa hivi siyo tu vina ubora, lakini ni vifaa mwafaka kwa wachezaji wetu na vitasaidia kuimarisha stamina kwa wachezaji na kuwaongezea utimamu wa kimchezo. Kama ulivyoona kila mchezaji alikuwa akiwajibika katika eneo lake.

Swali: Tunajua unajiandaa na Ligi Kuu na michezo ya kimataifa, unazungumziaje benchi lako la ufundi?

Hernandez: Kama unavyoona, tumekamilika, mazoezi ndio hayo...benchi langu la ufundi ninaweza kusema limetimia, lina watu 10, mimi Zebenzui Hernandez nikiwa kiongozi wao na nina wasaidizi wangu, Dennis Kitambi na Pablo Borges, kocha wa makipa Jose Garcia na mtaalamu wa mazoezi ya viungo Luis Garcia.

Katika mazoezi kila mtaalamu wa ufundi ana jukumu lake nami ninahakikisha kila mmoja anatimiza majukumu yake sawasawa...kama ulivyoona Garcia alikuwa akiwapa mazoezi ya viungo wachezaji.

Swali: Umeshawaambia wachezaji nini wanatakiwa kufanya katika wiki mbili?

Hernandez: Nimeshawaeleza, hata wasaidizi wangu wamewaeleza wajibu wao katika kipindi hicho, nimekuwa nikiwasisitiza umuhimu wa umakini uwanjani hasa safu ya ulinzi na kiungo na zaidi washambuliaji na nimewaeleza, nataka washambuliaji wanaotuliza akili golini, wawe makini wanaposhambulia wapinzani na kutumia nafasi wanazopata.

Mwanzoni uongozi uliniambia niangalie wachezaji sehemu mbalimbali kwa ajili ya kusajili lakini nimeona nitoe nafasi na muda wa kucheza na kuwaangalia hawa waliopo kabla sijaanza kufanya usajili mwingine.

Swali: Najua una utaalamu wako, ni nini hasa unakiangalia kwa wachezaji hawa?

Hernandez: Kuna vingi ninavyofuatilia, saikolojia ya mchezaji, ninaangalia nidhamu, stamina, umakini wa uwanjani, uwezo wa kupokea na kutoa pasi, mbio na fiziki ya mchezaji kwa jumla na hata uwezo binafsi wa mchezaji pamoja na kufunga mabao kaika nafasi rahisi na nafasi ngumu.

Swali; Uko katika uwanja ninaweza kusema uwanja makini, na si Tanzaia tu, sehemu kubwa ya mataifa ya Afrika ukiondoa Afrika Kusini yana matatizo ya miundombinu hasa viwanja, hii unaitazamaje?

Hernandez: Hii ni changamoto ambayo itanilazimu kubadilisha mfumo ili kupata matokeo. Nimeshafahamishwa tatizo la baadhi ya viwanja hapa, nitatumia mfumo mwingine badala ya kucheza mipira mirefu tu kwenye viwanja hivyo.

Tutacheza pasi kadhaa kwa haraka kisha tutapiga mipira mirefu, tukifanikiwa kuupata mbele tutapasiana na kumalizia shambulizi langoni kwa kufunga.

Swali: Nini matarajio yako?

Hernandez: Kuhusu matarajio yangu, kwanza nakiri kazi niliyoipokea ni kubwa lakini matarajio yangu ni kuhakikisha Azam inakuwa na wachezaji wenye nguvu na wanaoweza kupambana kuwania mataji mbalimbali. Ninataka wachezaji wenye nguvu na uwezo wa kupambana. Azam ni timu kubwa na inataka kusonga mbele.

Ninataka mashabiki wa klabu hii wawe na furaha, viongozi pia wafurahie mafanikio ya timu. Haya yatawezekana ikiwa nitaungwa mkono na uongozi ili nifanikishe mipango yangu ikiwamo ya kuwa na wachezaji wa uhakika.

Swali: Umeshazisikia Simba na Yanga? Hizi ndizo zinazotawala soka Tanzania, nini mipango yako ya kuleta mapinduzi ya soka si kwa Azam pekee?

Hernandez: Nimeambiwa na ninafahamu nitapata upinzani kutoka kwa timu hizo, lakini hazitanikwaza katika kazi yangu ya kuinoa Azam...nina taarifa za Simba na Yanga na ninajiamini nitakuwa na kikosi cha matokeo.

Mpira siku zote unabadilika, hauwezi kuwa upande mmoja, kwa timu hizi ninaamini hazitanisumbua akili na sioni kama zinaweza kunipa changamoto katika majukumu yangu. Ninachotaka ni kuijenga Azam ya matokeo, nikiwa na wachezaji makini.