Makocha watano bora waliopo sokoni Ulaya

London, England. Wakati makocha watano wakijiweka sokoni, klabu za Ulaya zinasaka mtu makini ambaye ataleta mafanikio na kufikia malengo ya klabu.

Idadi kubwa ya klabu zinasaka makocha bora wapya katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi na makocha wachache maarufu hawana timu za kufundisha.

Pamoja na wingi wa makocha hao, wapo makocha watano waliotikisa katika ligi Ulaya, lakini kwasasa hawana timu za kufundisha kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kufukuzwa.

Massimiliano Allegri

Aliifundisha Juventus ‘Kibibi Kizee’ cha Turin miaka mitano na katika kipindi chote alichodumu ndani ya klabu hiyo aliipa ubingwa.

Licha ya kuipa mafanikio Juventus, Mtaliano huyo ana bahati katika mashindano ya Ulaya, kwani hakuwahi kuipa timu hiyo Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lakini Allegri amewahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Italia ‘Serie A’ akiwa na kikosi cha AC Milan. Kocha huyo yuko huru baada ya kutangaza ataondoka baada ya msimu kumalizika.

Antonio Conte

Antonio Conte yuko nje ya uwanja tangu alipotupiwa virago Chelsea mwanzoni mwa msimu huu na nafasi yake ilijazwa na Mtaliano Maurizio Sarri.

Pamoja na kufukuzwa, Conte aliipa Juventus ubingwa wa Ligi Kuu mara tatu na mara moja akiwa Chelsea. Pia amewahi kuzipa mataji kadhaa ya ndani timu zote mbili.

Conte anahusishwa na mpango wa kujiunga na Inter Milan kujaza nafasi ya Luciano Spaletti.

Julen Lopetegui

Huyu ni kocha wa zamani wa Real Madrid aliyepita kipindi kigumu, lakini anatajwa kuwa mmoja wa makocha bora waliofanya vyema Hispania.

Lopetegeui alifanya vyema kwa asimilia 100 alipokuwa kocha wa timu ya Taifa ya vijana ya Hispania chini ya miaka 21, lakini katika kikosi cha wakubwa alipata asilimia 70.

Kocha huyo ndiye aliyeipeleka Hispania katika fainali za Kombe la Dunia, anasaka klabu mpya baada ya kuwa nje ya uwanja muda mrefu.

Arsene Wenger

Wenger alikuwa kocha wa maisha Arsenal baada ya kuinoa kwa miaka 20 kabla ya kujiuzulu msimu uliopita kutokana na shinikizo la mashabiki wa klabu hiyo.

Mfaransa huyo alipata mafanikio makubwa akiwa kwa washika bunduki hao baada ya kuwapa mataji matatu na kuweka rekodi ya kutwaa mara saba Kombe la FA.

Wenger amethibitisha anataka kurejea katika kazi yake na anahusishwa na mpango wa kutua Paris Saint Germain au Monaco aliyowahi kuinoa kabla ya kutua Arsenal.

Jose Mourinho

Jose Mourinho alikuwa na bahati mbaya Manchester United, licha ya kupata mafanikio katika klabu mbalimbali alizowahi kuzinoa kwa nyakati tofauti.

Tofauti na alipokuwa FC Porto, Inter Milan na Real Madrid, Mourinho alishindwa kuisuka Man United tangu alipopewa mikoba ya Mdachi Luis Van Gaal.

Kocha huyo raia wa Ureno amekuwa akifanya kazi ya kuchambua soka katika televisheni tangu alipofukuzwa Desemba, mwaka jana. Hata hivyo, Mourinho anahusishwa na mpango wa kutua Juventus.