Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanayokwamisha mafanikio ya michezo Tanzania

Kocha Simon Shimahoka (wa kwanza kushoto).

Muktasari:

"Timu ya taifa inategemea kupata wachezaji kutoka kwenye klabu,  lakini tatizo lililopo Tanzania ni klabu nyingi kuchezesha washambuliaji wa kigeni kuliko wazawa hali inayonipa wakati mgumu katika kuinoa timu hasa katika upande wa washambuliaji,"anasema Kim.

MAKOCHA ni muhimu. Hakuna mchezaji au timu yoyote duniani iliyofikia mafanikio bila kuwa na msaada wa makocha.

Ndiyo maana hata hapa nchini tumeshuhudia timu mbalimbali au wachezaji binafsi wakihaha kutafuta makocha wazuri.

Kutokana na umuhimu wa makocha, Spoti Mikiki imewafuatilia baadhi ya makocha nchini na kuzungumza nao ili kubaini changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika kutekeleza majukumu yao.

Kim Poulsen
Kocha huyu hana muda mrefu tangu alipokabidhiwa rungu la kuinoa timu ya taifa ya soka akichukua mikoba iliyoachwa na Mdenmark mwenzake, Jan Poulsen.

"Timu ya taifa inategemea kupata wachezaji kutoka kwenye klabu,  lakini tatizo lililopo Tanzania ni klabu nyingi kuchezesha washambuliaji wa kigeni kuliko wazawa hali inayonipa wakati mgumu katika kuinoa timu hasa katika upande wa washambuliaji,"anasema Kim.

Anasema,"pia mchezaji anapokuwa timu ya taifa anapaswa kufanya mazoezi na kujituma kwa sababu mazoezi ya timu ya taifa huwa ya  muda mafupi kuliko mchezaji akiwa katika klabu, lakini kuna baadhi ya wachezaji wakiwa timu ya taifa hawajitumia kama wanavyokuwa katika klabu zao."

David Yombayomba
Yombayomba ana uzoefu wa muda mrefu kwenye timu ya taifa ya ngumi za ridhaa akiwa ni miongoni mwa makocha wakongwe wa ngumi za ridhaa.

"Ngumi zinaanza kurudi kama ilivyokuwa enzi zetu, vijana wanajitahidi ingawa hakuna watu wa kuupromoti mchezo huu ili tufikie mafanikio, hii ni changamoto kubwa,"anasema Yombayomba.

Zacharia Gwandu
Kocha Gwandu alikuwa miongoni mwa makocha waliombatana na ujumbe wa Tanzania kwenye michezo ya Olimpiki iliyofanyika  England mwaka huu huku yeye akiinoa timu ya taifa ya riadha.

"Timu ingekuwa na wadhamini ni wazi riadha ya Tanzania ingefika mbali kwani vipaji vipo vingi ingawa havijaandaliwa, tunakosa maandalizi, tukiwaandaa wanariadha wetu Tanzania itapiga hatua kwenye mchezo huu,"anasema kocha Gwandu.

Simon Shimahoka
KOCHA huyu raia wa Japan aliambata na timu ya taifa ya judo iliyokwenda kutafuta vigezo vya kushiriki Olimpiki nchini Morocco ingawa haikufanikiwa kufikia vigezo hivyo.

Anasema,"tunafundisha vizuri katika maandalizi, lakini jambo la  kushangaza ni mchezaji anapofika ulingoni anashindwa kufanya moja ya kumi ya kile alichofundishwa, hali inayosababisha makocha kulaumiwa timu inapofanya vibaya."

Clinus Namajojo
Huyu ni kocha wa muda mrefu wa Paralimpiki (michezo ya Olimpiki ya walemavu) hapa nchini.

"Paralimpiki inahitaji vifaa maalumu kwa sababu michezo yenyewe inahusu walemavu, lakini wachezaji wanakumbana na wakati mgumu katika suala la vifaa na maandalizi hasa pale wanapotakiwa kujiandaa na mashindano ya kimataifa,"anasema Namajojo.

Abdallah Salehe 'Comando'
Huenda akawa kocha wa kwanza mwenye mafanikio msimu huu kwenye ngumi za kulipwa anayemnoa bondia namba moja hapa nchini, Francis 'SMG' Cheka.

"Ngumi za kulipwa bila jitihada binafsi hauwezi kufika mbali, mfano mzuri ni namna bondia wangu alipotokea hadi alipo hivi sasa, hakuna msaada wowote aliopewa zaidi ya juhudi binafsi, mabondia wa Tanzania wakiandaliwa ipasavyo wana uwezo wa kuitangaza nchi kimataifa," anasema kocha Salehe.

Mary Protas
Aliiongoza timu ya taifa ya netiboli 'Taifa Queens' kutwaa medali ya fedha katika michezo ya Afrika mwaka jana nchini Msumbiji anasema mfumo wa maandalizi ndiyo chachu ya taifa kufanya vibaya kwenye mashindano ya kimataifa.

"Hatuna msingi mzuri wa kuandaa vijana kuanzia ngazi ya chini, mchezaji anaibuka ukubwani na kuanza kujifunza kucheza, lakini tunasahau msingi mzuri unaanzia chini kwenye mashindano ya shule ya Umitashumta na Umisseta, pia tunatakiwa kuwa na makocha wengi wa michezo,"anasema Protas.