Yusuf Juma, Mtanzania anayezipigia hesabu Chelsea na Arsenal

Muktasari:

  • Hivi karibuni, kiungo wa Simba, Said Ndemla ametajwa kuwa ambaye amefuzu majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini Sweden katika klabu ya AFC Eskilstuna, yote hii inathibitisha kuwa ni wazi nyota wa Kitanzania wanapasua anga kwa kasi.

Wachezaji wa Kitanzania wanaendelea kupasua anga kwa kasi, kila mmoja kwa nafasi yake amekuwa akijitahidi kutafuta upenyo wa kwenda kujitafutia maisha ya soka kwenye mataifa yaliyopiga hatua kisoka.

Hivi karibuni, kiungo wa Simba, Said Ndemla ametajwa kuwa ambaye amefuzu majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini Sweden katika klabu ya AFC Eskilstuna, yote hii inathibitisha kuwa ni wazi nyota wa Kitanzania wanapasua anga kwa kasi.

Spoti Mikiki linaendelea kuibua wachezaji wa Kitanzania ambao wanatafuta maisha ya mpira nje ya nchi.

Wiki iliyopita tulikuwa na Benedictor Jacob anayeichezea Palos FC ya Ligi Daraja la Kwanza nchini Kenya anavyotamani kuitumikia Taifa Stars.

Leo tunahama kutoka Afrika hadi Marekani na kumleta kwako kiungo mkabaji wa Monroe SC, Yusufu Juma ambaye ametokea Mjimwema mkoani Kigoma kabla ya kutua Marekani.

Yusufu ana ndoto ya kuichezea Taifa Stars ambayo ipo chini ya kocha mkuu Salum Mayanga ambaye ameanza kutoa nafasi kwa wachezaji wa Kitanzania ambao amepata vielelezo vyao.

Katika mahojiano na Spoti Mikiki kutoka Marekani, anasema: “Kilele cha mafanikio yangu ninatamani sana kikamilike kwa kuwa mchezaji wa kutegemewa kwenye timu ya Taifa, ninasikia kuwa unapogusia Tanzania kwenye soka lazima umtaje Mbwana Samatta, amekuwa mchezaji muhimu ambaye kila mtu analitaja jina lake.

“Samatta ana uwezo mkubwa, amejituma mpaka kufika pale, lengo langu ni kujituma ili kufika ninapohitaji, Mungu akipenda hivi karibuni nitafungua ukarasa mpya wa soka langu kwa kwenda kufanya majaribio England.

“Pamojana yote yani inatakiwa nicheze kwenye kiwango cha juu, nitakapokuwa kwenye hicho kiwango hapatakuwa na wasi wasi kuhusu kuitwa kwangu timu ya Taifa,” anasema Yusufu.

Yusufu (17) alizaliwa kwenye Hospitali ya Maweni mkoani Kigoma na kuishi mkoani humo kwa zaidi ya miaka kumi kisha akapata nafasi ya kusafiri na wazazi wake kuelekea nchini Marekani.

“Wazazi wangu waliamua kuhama Kigoma na kuhamia Marekani, napenda sana soka tangu nikiwa mdogo kwa hiyo baada ya kuhamia Marekani nilianza kucheza mpira wa mtaani. “Nilipata elimu ya sekondari nikiwa Marekani, baada ya kumaliza elimu hiyo nilipata nafasi ya kujiunga na timu ya chuo cha Monroe SC, nilianza kawaida na mwisho wa siku waliamua pia kunipatia elimu ya bure kupitia kipaji changu.

“Sikuona tatizo kwa sababu walikuwa wakinilipa kwenye timu yao, huku kuna soka la vyuo ambalo ni maarufu na wachezaji wengi wa Ligi Kuu ya Marekani wamepitia kwenye mfumo huo,” anasema.

Hata hivyo, Yusufu anaonekana kutovutiwa hata kidogo na Ligi Kuu Marekani na ndiyo maana kaka yake Hamisi ambaye anamsimamia kama wakala amemtafutia nafasi ya kufanya majaribio London, Uingereza.

“Mwakani nimepewa ruhusu ya kufanya majaribio kwenye timu tatu za London ambazo ni Arsenal na Chelsea, kama nitafuzu nitapata nafasi ya kujiunga na vituo vyao vya kulelea vipaji vya soka.

“Pia nina upenyo wa kwenda Ubelgiji kama mambo hayatakaa vizuri, Ubelgiji nitafanya majaribio Standard Liege na Anderletch zote za Ligi Kuu, huku ni kama kule nikifuzu nitajiunga na timu zao za vijana,” anasema Yusufu.

Kiungo huyo anasema kuwa amekuwa akichukulia changamoto ni kama sehemu ya maisha na ndiyo maana kila akikutana na changamoto amekuwa akisonga mbele kwa kujua zinamjenga kukua kisoka.

“Kuna muda kunakuwa na mambo mazito kupita kiasi, nachofanya huwa naona kuwa yote hayo ni ya mpito hivyo huwa najipa moyo na nashukuru Mungu kwa sababu amekuwa akinishindia. Yusufu alimalizia kwa kusema mpango wa kaka yake kumtafutia sehemu ya kufanya majaribio umechangiwa na juhudi zake binafsi na hata hivyo kaka yake amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha anafanikisha ndoto zake.

Mchezaji huyo wa Kitanzania alimalizia kwa kusema kuwa anatamani kuwasaidia vijana wenzake ambao wana ndoto ya kucheza mpira kutokana na mfumo wa Marekani ulivyo.

“Mtu mwenye kipaji anatakiwa kusaidiwa na kuthaminiwa kama ilivyo Marekani, tukifika hapo tutakuwa kwenye hatua ya kuzalisha vipaji vingi kwa kuzingatia hayo,” anasema kiungo huyo wa kati.

Mbali na Yusufu ambaye anaichezea Monroe SC pia wapo Watanzania wengine ambao nao wanatafuta mafanikio ya soka nchini humo pamoja na kupatiwa elimu bure ambao ni Daud Aboud na Adolf Bitegeko wa Lcc Men’s Soccer na Ronald Makaramba ambaye kwa sasa anachezea TAMUT FC.