UCHAMBUZI: Serikali itatue mgogoro mpaka wa Mbarali, Hifadhi ya Ruaha

Muktasari:

Mgogoro huo unatokana na tangazo lililotolewa kwenye gazeti la Serikali namba 28 la mwaka 2007 ambalo linaainisha mipaka ya hifadhi ambayo wananchi hao wanaipinga kwa madai kwamba imeingia kwenye makazi na mashamba yao.

Zaidi ya miaka 10 sasa wananchi wilayani Mbarali, Mbeya wamekuwa kwenye mgogoro wa mpaka kati yao na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), mgogoro unaotokana na upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Mgogoro huo unatokana na tangazo lililotolewa kwenye gazeti la Serikali namba 28 la mwaka 2007 ambalo linaainisha mipaka ya hifadhi ambayo wananchi hao wanaipinga kwa madai kwamba imeingia kwenye makazi na mashamba yao.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, zaidi ya vijiji 21 wilayani Mbarali vipo ndani ya hifadhi na wananchi wanatakiwa kuondoka. Hata hivyo, suala hilo ambalo limedumu kwa zaidi ya miaka 10, kwa nyakati tofauti, viongozi wa Serikali wamekuwa wakitoa matamko kadhaa kuhusiana na mgogoro huo.

Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Mbarali, Modestus Kilufi alipigania vijiji hivyo 21. Alifanya hivyo akiwa ndani na nje ya Bunge kwa kutaka wananchi wa Mbarali watendewe haki kwani eneo la vijiji hivyo linashikilia uchumi wa wilaya kutokana na kilimo cha mpunga na ufugaji.

Februari 2015, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alienda wilayani Mbarali na kusema vijiji vyote vilivyotajwa havitaondolewa na kuutaka uongozi wa mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe kuchukua hatua za haraka kurekebisha tangazo lililoleta mabadiliko ya mipaka ili eneo hilo liwe mali ya wanannchi kwa mujibu wa sheria.

Kana kwamba hiyo haitoshi, wakati wa kampeni zake za uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, Rais John Magufuli aliahidi kushughulikia mgogoro huo na kwamba hakuna mwananchi hata mmoja atakayefukuzwa au kunyang’anywa mashamba yake kwa sababu za kupisha upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Licha ya matamko na ahadi hiyo, hali ipo tofauti na wananchi hao wanatakiwa kuondoka kwenye maeneo hayo yakielezwa kuwa ni sehemu ya hifadhi kwa mujibu wa sheria.

Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune akiongozana na maofisa wa Tanapa walikwenda Kijiji cha Mwanavala wilayani humo na kuwakamata baadhi ya wakulima hao na kuwafungulia mashtaka mahakamani kwa madai kuwa wanaendesha kilimo ndani ya hifadhi.

Kutokana na ‘kamata kamata’ hiyo, zaidi ya wakulima 1,000 wa Ushirika wa Nguvukazi Mwanavala wanaoendesha shughuli zao kwenye mashamba ya mpunga Kijiji cha Mnazi, Kata ya Imalilo wameunda tume ya watu watano ili wakaonane na Rais John Magufuli na kumueleza kilio chao. Wanaamini Mfune na maofisa wa Tanapa hawawatendei haki. Wakulima hao walifanya uamuzi huo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kitongoji cha Mnazi kwa kile walichodai wameanza kunyanyaswa na moafisa na askari wa Tanapa.

Hata ofisi ya Mkuu wa Wilaya wamesema imekuwa ikitoa amri ya kuwakamata wanaokutwa wakiandaa mashamba kwa ajili ya kilimo cha msimu huu. Hata hivyo, Mfune anakana kuwahamisha wakulima hao na badala yake anasema wanaokamatwa kwa amri yake ni wanaokutwa wakiharibu mazingira kwa kukata miti ovyo kandokando ya mto Ruaha ambao ni chanzo cha maji.

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Ruaha, Dk Christopher Timbuka anasema ni kweli Serikali ilisitisha mpango wake kuwaondoa wananchi katika maeneo ila anawataka wasiendeleze kilimo kwenye maeneo mapya zaidi ya waliyokuwa wakilima mwanzo hadi mwafaka utakapopatikana. Ni matumaini yangu Serikali itatafuta ufumbuzi wa kudumu na kuziruhusu pande hizi kuendelea na majukumu yao ya kujenga nchi.

Godfrey Kahango ni mwandishi wa Mwananchi. Anapatikana kwa 0715 059 107