Umaarufu wa choo ni harufu

Muktasari:

  • Kwa maana hiyo mtu aweza kuwa na imani chungu nzima kwa wakati mmoja. Yeyote anayekuambia kuwa imani ni dini yake pekee muulize kwa nini anakwenda “kuhiji” kwao Moshi kila Krismasi kama Wayahudi wanavyofanya kila Pasaka. Anaamini kuwa mara atakapokutana na wazazi na ndugu atapata njia za kuongeza duka la pili mtaani kwake na atarekebisha afya kwa mtori halisi.  

Imani ni uhakika wa mambo yaliyokuwepo hata kama hutayathibitisha. Unaweza kusikia na kuamini jambo bila hata kuliona. Unalitafakari na kuhakikisha kuwa jambo hilo ni la kweli. Yupo anayeamini kuwa shetani yupo bila kuona hata mchoro wake. Mwingine anaweza kuziamini ndoto zake na akaishi nazo. Hiyo ndiyo imani.

Kwa maana hiyo mtu aweza kuwa na imani chungu nzima kwa wakati mmoja. Yeyote anayekuambia kuwa imani ni dini yake pekee muulize kwa nini anakwenda “kuhiji” kwao Moshi kila Krismasi kama Wayahudi wanavyofanya kila Pasaka. Anaamini kuwa mara atakapokutana na wazazi na ndugu atapata njia za kuongeza duka la pili mtaani kwake na atarekebisha afya kwa mtori halisi.    

Maisha ni suala la kifalsafa kuhusu madhumuni na umuhimu wa kuwepo duniani. Viumbe hai vyote vinaishi ingawa sidhani kama vinajua kwa nini vipo. Binadamu tofauti na viumbe vingine anafuata imani ili imjulishe yupo kwa ajili gani. Yupo anayeamini kuwa yupo kwa ajili ya kumtumikia Mungu, mwingine ili aiburuze dunia, mwingine ili aijaze dunia, apendwe au awe maarufu.

Tunaweza kuona jinsi binadamu anavyojikita kwenye uchawi akiamini yupo kwa ajili hiyo. Huyu akiambiwa amtoe mwanaye mpendwa kama sadaka au kafara hawezi kusita. 
Mwanachama wa kundi la ugaidi anaweza kujivalisha mabomu na kujilipua katikati ya watu bila kuhofia kuwa anaua raia wasio na hatia. Enzi zile akina Mfalme Chaka walikuwa wakizikwa na watumishi walio hai baada ya wao kufa. Watumishi hawakukimbia kwani waliamini kuwa walikuwepo kwa ajili ya Mfalme. Huu ndio utamu na uchungu wa imani.

Lakini leo tuna kazi na wanaoamini kuwa wapo kwa ajili ya umaarufu. Wapo ndugu wawili waliokuwa maarufu kwa uwindaji. Mmoja anasaidia familia zisizojiweza kwa mazao yake ya uwindaji. Ameongeza kitu cha ziada ambacho mwenzie hana. 

Huyu wa pili anaona usinitanie; anakwenda porini na katika mawindo anafanikiwa kumpata sungura. Anamleta sokoni kwenye kundi la watu. Anamwinua sungura na kumchinja kwa meno! Watu wanasahau gumzo la “Mwindaji hodari” na wanafungua ukurasa mpya wa “Mchinjaji kwa meno”. Anakuwa maarufu zaidi ya anayelisha masikini kwa mawindo yake.    
Bill Clinton, Rais wa 42 wa Marekani alishakuwa maarufu kutokana na kiti hicho. Akapata kashfa ya mapenzi na Monica Lewinsky mwaka 1998. Ili kujiondoa kwenye umaarufu huo na kulinda chama chake, mwaka huohuo akaenda kurusha maguruneti kwenye shamba la Shifa huko Sudan na Afghanistan. 

Clinton akafanikiwa kuufuta umaarufu alioupata kwa Monica na akajenga umaarufu wa kijasiri kwa kupambana na “wahalifu”.

Michael Jackson alimfuata Elvis Presley aliyefariki mwezi Agosti, 1977. Alimpenda hadi akamwoa binti yake, Lisa Marie mnamo mwaka 1994. Michael alichagua muziki wa pop kama Elvis na akajenga jumba lake katika ranchi, Neverland kama Elvis aliyejenga Jungle Room. Wote walifanya muziki kwa nguvu zao zote pamoja na za ziada, wakafanikiwa kuupata umaarufu.

Kwa bahati mbaya wote vifo vyao vilisababishwa na athari za vidonge vya kutuliza maumivu. Kama familia ya Presley, familia ya Jackson ilimzika Michael porini kwenye ulinzi mkali kuhofia “watalii” ambao wangefurika kuyatembelea malalo yake kama ilivyokuwa kwenye malalo ya Elvis. Familia zao ziliuogopa umaarufu wa ndugu zao.

Mtu yeyote mwenye akili timamu hujitathmini kabla ya kuiga. Kibongobongo tunaishia kuiga kutembea uchi hadharani kama Selena Gomez au Ashley Tisdale, kuvuta bangi hadharani ili kukamatwa kama Ja Rule, kubadilisha mabwana kama Jennifer Lopez na kujikweza wenyewe katika daraja ya “Superstar”. Fikiria ujinga huu; unakuwaje “Superstar” kabla hujawa “Star”.

Umaarufu ni jambo linaloweza kukuvaa kwa njia nyingi sana. Unaweza kuwa jambazi maarufu lakini ukalala mchana kutwa kwa kuogopa macho ya watu na mikono ya sheria. Umaarufu ulioujenga kwa nguvu nyingi unakutesa kama mtu akimbiaye kivuli chake mwenyewe. Yupo aliyerundika masanduku ya dhahabu chumbani kwake, lakini woga ukaanza kumtafuna.

Akajenga ukuta mrefu wenye nyaya za umeme juu yake, akaweka mitambo ya kubaini wezi kwenye kuta hizo hadi chumbani. Akasimika geti kubwa na imara, akaajiri kampuni za ulinzi wa masaa ishirini na manne kila siku. Akapachika vifaa vya utambuzi (GPS) kwenye kila sanduku, Alipoingia kulala hakuwaamini walinzi wake.

Alifunga mageti kuanzia la nje, ya milangoni na akafunga milango kuanzia sebuleni mpaka vyumbani. Ukifikiria sana unaweza kucheka; starehe gani hii?  Nasikitishwa na vijana wanavyokesha kwenye mitandao ya kijamii kuandaa “breaking news” ili kila uchao awe “juu”. Watatajwa kwa lipi wakati hawana mapya? Hapo ndipo unapoona habari mpya kila siku: “Nimempiga kibuti bwege yule, sasa nadunda supastaa mwenzangu!” .
Yeye na wenzie wajue kuwa huo ndio umaarufu kinyesi. Waige mazuri na kuyapotezea mabaya, walenge umaarufu wa tuzo za Kora, Oscar, Grammy.