URITHI WETU: Hawa ndio Wahehe na chimbuko lao-1

Muktasari:

  • Kwa kiasi kikubwa, Mkoa wa Iringa unabebwa na historia ya mkazi wake maarufu, Chifu Mkwawa.

Tuanze kwa kuamkiana ile salamu maarufu ya Wahehe ya ‘Kamwene’.

‘Kamwene’ ni salamu tu kama ilivyo habari za leo na ikiwa utaamkiwa hivyo basi huna budi kujibu neno hilohilo, ‘Kamwene’.

Kwa kiasi kikubwa, Mkoa wa Iringa unabebwa na historia ya mkazi wake maarufu, Chifu Mkwawa.

Kiuhalisia huwezi kuwazungumzia Wahehe bila simulizi za kusisimua za Chifu Mkwavinyika Mwamuyinga Mkwawa, ambaye inasadikiwa alijiua akiwa na umri wa miaka 41 tu.

Mpaka leo utawala wa kichifu unaendelea na kwa sasa Chifu Adam Abdul Mkwawa (20), ndiye aliyetawazwa kuliongoza kabila la Wahehe akisaidiana na wazee.

“Wakati natawazwa nilikuwa mdogo sana, nakumbuka kila kitu na nilikuwa nafahamu nitakuwa chifu baada ya baba yangu, Abdul Adam Sapi Mkwawa kufariki. Moyo wangu kwa wakati huo haukuwa unaona kitu, ila huzuni tu,” anasema Chifu Adam II


Historia ya Iringa

Iringa ni kati ya mikoa mitano ya Nyanda za Juu kusini, ukiwa na wilaya tatu ambazo ni Kilolo, Iringa yenyewe na Mufindi.

Mji wa Iringa ulianzishwa mwaka 1896 na Wakoloni wa Kijerumani kama kituo cha kijeshi ambacho walikiita Iringa Mpya.

Maandiko yaliyo katika jengo la Makumbusho ya Mkoa wa Iringa ( Boma) chini ya mradi wa fahari yetu Tanzania, yanaonyesha kuwa jina la Iringa lilitokana na neno la Kihehe ‘Lilinga’.

Lilinga ni jina linalomaanisha makazi ya karibu kuzunguka makao makuu ya himaya ya Wahehe chini ya Chifu Mkwawa.

Linamaanisha pia mahali palipozungukwa na ukuta kwa maana ya ‘Boma’.

Iringa ya zamani ilikuwa Kalenga na huko ndiko yaliko makumbusho ya Chifu Mkwawa, na ni kati ya vivutio vikubwa ya utalii ndani ya Mkoa wa Iringa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa na Meneja msaidizi wa mradi huo Dk Jimson Sanga, anasema Mkoa wa Iringa unabeba utajiri wa historia na simulizi za kusisimua zinazoweza kuvutia watalii wengi wa nje na ndani.

“Kila unapogusa unaweza kuandika simulizi ya kusisimua kuhusu Wahehe na chifu wao, utajiri huu ni wa kujivunia,” anasema.


Chimbuko la Wahehe

Wazee waliozungumza na Mwananchi wanasema chimbuko la kabila la Wahehe ni milima ya Udzungwa na wakati huo walikuwa wakiitwa ‘Wabena Manga’.

“Udzungwa ndiko walikoanzia Wahehe na walipohama huko walikuja moja kwa moja kwenye kijiji cha Luhota, wilayani Iringa, wakaweka makazi,” anasema Mzee wa kimila, Gerald Malangalila.

Hata hivyo, inasadikiwa kuwa asili ya kizazi cha Mkwawa sio Iringa, bali ni visiwa vya Comoro na walikabidhiwa uchifu baada ya kushinda vita.

Historia inaonyesha kuwa Mfwimi yaani ‘mwindaji’ ndiye aliyeanzisha ukoo wa Mkwawa. Huyu alifika Iringa kama mkimbizi, akikimbia vita kwao.

“Alikuja kwa mguu akiwa kijana na hajaoa, alitokea njia ya Kilosa Morogoro, akafikia milima ya Kidai na akaanza kuishi huko,” anasema Mzee Malangalila.

Akiwa milimani, Mfwimi wakati akiwinda alikutana binti, mtoto wa Mwakivamba, wakamzaa mtoto na kumpatia jina la Mdegela.

“Mdegela alivyozaliwa ndiye alipewa jina la Mwamuyinga kwa sababu alikuwa mtoto wa kiume na kama angekuwa wa kike, angeitwa Semuyinga,” anasema.

Mdegela akamzaa Kilonge na Kilonge akamzaa Chifu wa kwanza wa Wahehe aliyekuwa anaitwa, Ngaona Lupembe Malangalila (Babu yake Chifu Mkwawa).

Mzee Malangalila anasema, Ngaona Lupembe alimzaa Chifu Mnyigumba ambaye ndiye baba mzazi wa Chifu Mkwawa.

Hivyo jina kamili la Chifu Mkwawa ni Mukwavinyika Munyigumba Mwamuyinga.


Munyigumba karne ya 17

Historia inaonyesha kuwa katika karne ya 17, makundi yaliyojulikana kama Vamia na Vigavilo yaliishi katika eneo la Iringa.

Jamii hizo ziliunganishwa na Chifu Ngaona Lupembe na kuwa jamii moja ya Wahehe.

Chifu Ngaona Lupembe anajulikana kama baba wa Wahehe na alifariki mwaka 1920, huku kaburi lake likiwa bado linatumika kwa matambiko na wenyeji nyakati za shida.

Chifu Munyigumba, mtoto wa Ngaona Lupembe yeye aliongeza miliki ya Wahehe kwa kushambulia jamii nyingine ndogondogo kama vile Ilole, Ilula na Image.

Dk Sanga anasema inasadikiwa kuwa Chifu Mnyigumba alikuwa anatumia dawa inayoitwa ‘Amahomela’ ili kushinda mapigano.

Ushindi huo ulikuwa ni ushahidi wa ubora wa utawala wake wa kichifu.

Mnyigumba kama machifu wengine, alikuwa tajiri, aliheshimika na alikuwa na wake wengi na ikumbukwe huyu ndiye baba yake Chifu Mkwawa.

Simulizi itaendelea kesho, ikimwangazia Chifu Mkwawa, kutoka utoto hadi kuja kuwa shujaa wa Wahehe.