Uzee ukizidi unageuka utoto
Muktasari:
- Jibu lake ni mzee kikongwe aliyezaliwa pasipo na uwezo wa kusogea, akatambaa utotoni, akatembea ujanani, nguvu zilipoanza kuisha akatembea kwa msaada wa mkongojo. Zilipomwishia kabisa akatambaa, na hivi sasa anabebwa kupelekwa nje kuota jua.
Inasemekana mtu akishakula chumvi nyingi anarudi kwenye utoto. Wataalamu wanasema wazee hukumbuka mambo ya utotoni kuliko ya ujanani. Utotoni (na mimi nahisi kuzeeka) tulikuwa na kitendawili kilichohoji ni nani alianza kwa kulala, baadaye akatumia miguu minne, kisha akaja na miwili, baadaye mitatu, akarudia minne na sasa amelala.
Jibu lake ni mzee kikongwe aliyezaliwa pasipo na uwezo wa kusogea, akatambaa utotoni, akatembea ujanani, nguvu zilipoanza kuisha akatembea kwa msaada wa mkongojo. Zilipomwishia kabisa akatambaa, na hivi sasa anabebwa kupelekwa nje kuota jua.
Kitendawili hicho hakina maana kwamba hayo ndiyo maisha ya kila mwanadamu, japo kwa asilimia kubwa ilikuwa au ipo hivyo. Mara nyingi mtu akishafikia kuitwa mzee hukubaliana na hali ya uzee ya aina hii itakayomtokea. Lakini wapo wazee wanaowasaidia vijana wao kusoma namba za vocha bila msaada wa miwani. Hilo ni angalizo tu kwamba maisha ya vijana wa sasa hayatafikia kutembelea miguu minne wala mitatu.
Moja ya sifa kubwa za uzee ni kupoteza nguvu za ogani za mwili kuona, kusikia, kunusa, na kuhisi mguso wa mwilini. Hayo huenda sambamba na kupoteza kumbukumbu, maana ubongo huwa mzito kutafsiri mambo. Mara nyingi wazee humfurahia mgeni kabla ya kumuuliza: “Wewe ni nani vile?” Mkewe atamsaidia: “Baba Hiki na wewe... Unamsahau mtoto wako mwenyewe!”
Hapo sasa mzee kwa kuzingatia mfumo dume atajiongeza kwa kumpa mikono mgeni. Huku akitabasamu na kumsogeza karibu “Akh! nikusahau vipi tena jembe langu Hiki? Habari za Mjini?” Bi Mdashi atamnyoosha: “Siyo Hiki, huyu ni mdogo wake, Kijacho wa Mwanarumango!” Mzee atanung’unika chini kwa chini “Mi nilisema huyu ni Kijacho mkanikatalia...” Kunung’unika kuna raha yake uzeeni.
Wakati mwingine uzee una athari zaidi ya athari za uzee. Yupo mmoja aliyekuwa hajambo kidogo kwa ukwasi aliokuwa nao, alikuwa akiopoa binti mchanga kila uchao. Mzee alifunga ndoa na kutaliki kama anayebadilisha nguo za kulalia. Mfumo wake ulikuwa “kwenda katika kasi ya Sayansi na Teknolojia”, akawa akipunguza wake waliofanya kazi na kuoa waliojua kujifunza kula bata!
Watoto na wajukuu walimtafutia wataalamu wa afya wampe nasaha. Wataalamu waligundua kuwa mzee si kwamba hakuweza kupata watoto, bali hakuwa na uwezo hata wa kushiriki tendo la ndoa. Jibu likaja kwamba alikuwa ameingiliwa na uchaa uliompelekesha kwenye mzuka huo. Alishapoteza kumbukumbu kiasi cha kutaka kuoa mabinti wa watoto wa kuwazaa mwenyewe.
Mwenyewe aliona sifa kutoka na vifaranga hao kwenda nao klabu, akiwavalisha mavazi ya masistaduu, naye akiwa amevalia kama sharobaro. Vijana aliokutana nao walijua ni wajukuu wanampa zoezi babu yao. Lakini kila walipotupa macho ya husuda kwa mabinti wale, mzee aliwaambia “Sijalala wanangu, mtauawa bure!”
Hapa ndipo ninapojiuliza maswali: Inawezekana wazee wengine hivi leo wanazeeka zaidi ya wazee wa zamani? Wazee wetu walikuwa na umakini sana katika suala la familia, hivyo hawakukubali watoto wao wakaokote yeyote wanayemwona anawafaa. Walihakikisha watoto wanachumbiwa kutoka kwenye familia bora, tena pengine walisimama kidete kuhusu masuala ya mahari. Hata kama binti ni mrembo, akitokea kwa wazazi mafyatu hakuwa na nafasi kwenye familia zao.
Wenzetu huko Ughaibuni wana ndoa za mkataba, potelea mbali baba ni chizi na mama ni hamnazo, wanasaini mkataba wa miaka mitano kwa malengo ya kuzaa watoto wawili. Mkataba unasema baada ya kizazi hicho, mume atamlipa mke nyumba na gari. Je, wana uhakika na afya ya akili ya huyu? Wanajua malezi aliyopewa na wazazi wake? Na wanahakikishaje usalama wa mtoto wao mikononi mwa binti huyo?
Hivi ndivyo vilio tunavyosikia hivi sasa kutoka kwa wanasiasa, viongozi wa imani, wasanii na watu wengine maarufu hapa duniani. Wanafanya mambo makubwa na mazuri lakini wanakwazwa na watoto na wajukuu zao mashoga na wala unga wanaofunika vyombo vya habari. Imefikia hatua wananchi wao hawataki kuwapa dhamana viongozi hawa kwa sababu “fair starts at home”. Uongozi wa nyumba umekushinda, utauwezaje uongozi wa nchi?
Tuje hapa kwetu. Ni kweli tumezeeka kiasi cha kusahau tutavuna tulichokipanda? Una mke mzuri wa kukuzalia watoto, lakini humpi huduma hadi akuzalie mtoto. Tena kule kwenye utajiri wa mang’ombe mama anaambiwa: “Mpaka unizalie mtoto wa kiume!” Hivi watu wana akili kweli? Hawafikirii miujiza ya Mwenyezi Mungu, hata kwa ukatili mdogo waseme “Mpaka unizalie binadamu”? Hawajui anaweza kuzaliwa nyoka!
Hivi kweli unaacha kutengeneza timu, halafu unaiambia timu uliyoiokota: “Mkishinda nakupeni bilioni!” Wapo watu walioanza miradi na misingi midogo kama laki moja, na sasa tunashuhudia wakiwa wafanyabiashara wakubwa. Kwa nini hiyo bilioni jumlisha milioni tano za magoli zisifanye kuwa mbegu ya kuandaa timu kabla haijaingia uwanjani? Ni fedha nyingi ambazo zingewekezwa kwa mipango tungeweza kunyakua kombe la dunia huko baadaye.