Valentine ya sasa, siyo upendo, ni mapenzi?

Msanii Shilole akiwa na mchumba wake Nuhu Mziwanda
Muktasari:
Badala ya kuhamasisha upendo kwa wote kama ilivyo dhana ya siku yenyewe, siku hii sasa inatumika kuhamasisha mapenzi kwa wale wenye uhusiano wao na hata kwa wale ambao hawana, huhamasisha kufanyika kwa mapenzi kiholela.
Leo ni siku ambayo Watanzania wataungana na watu wote duniani kuadhimisha Siku ya Wapendanao, kwa upande mwingine siku hii ikiangaliwa tofauti na Watanzania walio wengi hasa vijana.
Badala ya kuhamasisha upendo kwa wote kama ilivyo dhana ya siku yenyewe, siku hii sasa inatumika kuhamasisha mapenzi kwa wale wenye uhusiano wao na hata kwa wale ambao hawana, huhamasisha kufanyika kwa mapenzi kiholela.
Mambo mengi hutokea, likiwamo la vijana kuanzisha uhusiano na wapenzi wapya na wale wa zamani kubaki na wakati mgumu baada ya kuwakosa wapenzi wao katika siku hii ambayo wengi huichukulia kuwa muhimu kwa mahusiano yao.
Mara nyingi siku hizi, tunashuhudia kuvunjika kwa uhusiano wa wengi baada ya wapenzi kujikuta wakiwa katika kuelewana, hasa wale walio na wapenzi zaidi ya mmoja.
Wapenzi hutegemea vingi katika siku hii na baadhi ya vitu muhimu ambavyo huleta mashaka ni pamoja na:
Ukaribu
Hii ni siku ambayo wapenzi huamini kwamba ni vyema kutenga muda kwa ajili ya wenzi wao ili angalau kwa masaa mengi wawe pamoja na kutafakari kwa kina kuhusiana na mapenzi yao, wengine huitumia hii siku kwa maongezi maalumu.
Hapa ndiyo kunakuwa na mipango ya ndoa, kuvishana pete na wakati mwingine kujadili upungufu walionao ili kuweza kuyarekebisha na kuboresha uhusiano.
Tatizo kubwa huwakumba walio na wapenzi zaidi ya mmoja maana hukosa ule muda wa kukaa sana na wapenzi wao.
Matatizo zaidi huanzia hapa
Zawadi:
Ni kama utamaduni, kila mwenye mpenzi wa kudumu huwa na hisia kwamba ni lazima ataletewa zawadi na mpenzi wake ikiwa ni kama kumbukumbu ya mapenzi yao kwa mwaka husika.
Zawadi huwa za aina mbali mbali, kuanzia manukato, maua, vitafunwa, mavazi, wengine hupeana mpaka magari, au hata nyumba kulingana na uwezo wa mtu.
Hali mbaya huja tena kwa wapenzi walio na uhusiano zaidi ya mmoja, hapa gharama ya fedha na muda huwakuta.
Utapeleka nini kwa fulani na saa ngapi?
Mitoko:
Kila mtu anahisi siku ya wapendanao ndio ziku nzuri ya kutoka na kufurahi na mpenzi wake na siyo marafiki wa kawaida ambao hutoka nao kila kukicha.
Hali huwa ngumu pale na kijana anakuwa na wapenzi zaidi ya mmoja ambapo sasa hulazimika kadiri awezavyo kuhakikisha kwamba kila mmoja anafurahi kwa upande wake.
Balaa kubwa hutokea kwenye muda, kila mmoja huhisi kwamba usiku kwenye chakula ndio muda mzuri wa kutoka na mpenzi. sasa kama ukiwa na zaidi ya wawili, unafanyaje?
Wasanii mbalimbali wamezungumza wanavyoichukulia siku hii akiwamo Hemed Suleimani PHD, ambaye amesema kuwa kwake siku hii ni ya upendo kama nyingine.
Alisema haitumii kubadili msimamo wa maisha yake ya uhusiano kama ana kimwana wake atatoka naye kama kawaida lakini atabadili mazingira kuonyesha kuwa siku hiyo ni ya kupendana zaidi.
“Jambo la msingi nitapiga pamba na nitampigilia kimwana wangu, ili azidi kuwa mkali na kutoka naye na nitatumia siku hiyo kuwakumbuka ndugu jamaa na marafiki kuonyesha kuwa hata wao nawapenda wakiwamo wazazi wangu na zitakuwa salamu rasmi za siku hiyo,” alisema PHD.
Shilole
Mwimbaji na mwigizaji Shilole alisema kuwa siku ya leo ataitumia kuonyesha upendo zaidi kwa familia ikiwamo wanaye, ndugu jamaa na majirani, lakini zaidi atamwonyesha mahaba ya nguvu mpenzi wake Nuhu Mziwanda.
Alisema siku hiyo ni ya malavidavi, hivyo hata yeye atatumia muda mwingi kuonyesha ni jinsi gani mapenzi yanatakiwa kuwa.
“Hiyo siku ni ya malavidavi siyo kwa wapenzi wetu pekee, bali kwa watu wote kwa ujumla, inavyotumiwa sasa mimi sikubaliani nayo, watu huifanya siku hii kama ndiyo ya kufanya mapenzi kiholela hapana, ila kama una mtu wako wa kila siku, inabidi atambue kuwa unampenda,” alisema Shilole.
Dully Sykes
Alisema siku hiyo inatumika vibaya kwa watu kutongoza wasichana au wasichana kuwakubali wavulana wapya ili kujirusha nao siku hiyo, sidhani kama ndiyo maana halisi ya uwapo wake.
Alifafanua kuwa kuna haja ya watu kama hawa kubadilika kwani wanatia aibu na kinyaa hii ni siku ya kuongeza upendo kwa watu wote wanaotuzunguka ikitumika ndivyo sivyo ni kujishushia hadhi.
“Inanishangaza utakuta kijana mzima anadiriki hata kuachana au kugombana na mpenzi wake wa siku nyingi kwa sababu tu ya siku hiyo ya kupita, hivyo mimi kwangu huo ni ushamba,” alisema Dully.
Dully hakuacha kuingiza utani wake mwingi kwa kusema kuwa anategemea pia siku hiyo kupata ushirikiano tofauti kutoka kwa mwandani wake huku na yeye akifanya kama ambavyo anatarajia kufanyiwa.
Lina Sanga
Alisema tabia ya watu kukariri kuwa siku hii ni ya kuanzisha uhusiano mpya wa mapenzi imepitwa na wakati ndiyo maana inajirudia kila mwaka hivyo unatakiwa kuitumia kwa kuwa karibu na watu wote kuonyeshana upendo.
Kwangu siku hii ni kama tunakumbushwa kuwa binadamu wote ni sawa na tunastahili kupendana na kuheshimiana na tunatakiwa kuitumia siku hii kupima upendo wetu kwa jamii inayotuzunguka.
Siyo mbaya kama utafanya kitu maalumu kwa mpenzi wako uliye naye siku zote kwa kumnunulia zawadi kumtakia heri ya siku hiyo na hata kutoka naye kwenda eneo ambalo kila mmoja atafurahi na kusahau magumu mliyopitia katika mapenzi yenu, ingawa hiyo siyo tiketi ya kupata wapenzi wapya.
Hassan Moshi William
Siku hiyo ni maalumu ya kuonyeshana upendo wa dhati na ambao kila mmoja akikaa anakumbuka mwaka mzima jinsi watu wanaompenda hasa wapenzi wao walichowafanyia.
Siyo vizuri kutafuta wanawake wengine lakini ni vyema kutoka na huyo aliyekuwapo tena mtoko maalumu ambao utabaki kuwa historia kichwa kwa kila mwenza.
Mimi kwangu hiyo ni siku maalumu, nitawapenda wote lakini nitaonyesha upendo zaidi na wa wazi kwa kumnunulia zawadi, kumtoa out mwandani wangu.