Wanawake wasomi, matajiri hukumbana na vikwazo kupata wenzi

Muktasari:
- Tamaduni, mfumo dume na kutojiamini imeendelea kuwa changamoto kwa wanaume wasomi kupata wenza wa kudumu.
Baadhi ya jamii zinaamini mwanaume ndiyo anatakiwa kujimudu kielimu, kiuchumi, hivyo inapotokea mwanamke akawa na uwezo wa kifedha, msomi wanamuona kama amemtawala ndugu yao.
Tamaduni, mfumo dume na kutojiamini imeendelea kuwa changamoto kwa wanaume wasomi kupata wenza wa kudumu.
Ipo mifano hai mingi ya wanaume kulalamika au kuonekana wasio na hadhi mbele ya jamii pale wanapokuwa katika uhusiano au ndoa na wanawake waliowazidi kipato au elimu.
Mmoja wao ni Antony Kaizer anayekiri kuwa pamoja na kuwa na mke msomi na anayefanya kazi yenye malipo mazuri, anapata wakati mgumu kwa familia yake.
Anasema mke wake hana nafasi ya kuchangia mawazo kwenye familia yake kwa sababu wanaamini anaringa kutokana na kipato na elimu aliyonayo.
“Inachukua muda familia kukuelewa na wengi wao huamini umetawaliwa. Inafika wakati hata kumuhudumia mtoto wako kwa mapenzi unaonekana umefanywa msaidizi wa kazi, ”anasema Kaizer.
Kaizer anafafanua aliwahi kupata mkasa wa ajabu miaka mitano iliyopita, ambapo familia nzima walisusa kufika nyumbani kwake kwa madai kuwa wanapangiwa usafi.
“Baadhi ya wasomi wana taratibu za maisha tofauti kidogo, kwa maana ya kuwa wasafi, kuvaa nguo kulingana na wakati, kuzungumza Kiingereza wanapokuwa na watoto na mwenza na kuchanganya na Kiswahili kulingana na mazungumzo.
“Uandaaji wa chakula kinatayarishwa cha wastani na kuwekwa mezani kila mmoja ajipakulie, familia yangu ilisema mke wangu mchoyo na wakakata mguu kuja nyumbani, ilinitesa alikuja kuokoa jahazi mjomba wangu anayeishi Uganda, ”anasema.
Mkazi wa Tabata Segerea jijini Dar es Salaam, Irene Japhet anasema yupo ndani ya ndoa kwa miaka 12 na huenda kwa wakwe zake kipindi cha kubatiza watoto tu, kwa sababu hakubaliki kabisa.
Irene anafafanua kuwa mumewe ni msomi kama yeye ingawa wanafanya kazi tofauti lakini ana kipato kikubwa kuliko mumewe kidogo.
“Nimetengana nae kila mmoja anaishi kwake, hatuna ugomvi na huja kutizama watoto wake watatu tuliozaa pamoja, ”anasema Japhet.
Hoja hizo zinapata upinzani kutoka kwa Haika Lazaro anayesema wanawake wasomi mara nyingi wasumbufu na wanaamini wanaweza kila kitu kutokana na baadhi yao kuwa na kazi nzuri.
“Hata mimi sikubali kaka yangu au ndugu yangu wa kiume kuoa msomi na mwenye kazi nzuri kuliko yeye, kwa sababu huwa hawajali na hawapokei oda yoyote kutoka kwa waume zao na ndugu pia.
“Kuna jamaa yetu alioa Mzungu na mwingine alioa Mswahili tena kabila letu aliyesoma, basi bora uende kwa Mzungu atakupokea vizuri kuliko huyo msomi hana muda na wageni yupo bize na mambo yake muda wote, hapana hawafai, ”anasema Lazaro.
Mtaalamu wa masuala ya saikolojia Modester Kamongi anasema hali hiyo hutokana na athari za kisaikolojia ambapo mwanaume ameumbwa na nguvu na ubora.
Anasema kwa asili tangu enzi mwanaume ni kichwa au mtawala wa familia, hata awe mdogo kwa umri ila ana asili hiyo yaani ni kitu ambacho kipo ndani yake.
“Sasa inapokuja kwenye suala la uhusiano nguvu hiyo pia huchukua nafasi. Mwanamke kwa asili ni kiumbe anayesikiliza, mwanaume yoyote anaamini hivyo, kwa hiyo anataka ile asili yake ya nguvu na utawala ionekane, hapo ndiyo inapokuja tofauti.
“Wanawake wasomi wanapenda kuolewa kama wanawake wengine, wanakosa wenza kwa sababu wanaume huwaogopa na wakiwaoa huishi nao kwa machale wakiamini watatawaliwa, ” anasema Kamongi.
Anafafanua ili ile hulka yao ya kuwa vichwa kwenye familia itimie wanaume huwakwepa, huku wanawake wakihitaji kuolewa wanajikuta hawapati anayeendana nao kwa sababu ya mitizamo ya asilimia kubwa ya wanaume.
“Wanawake hao wasomi ikumbukwe ni binadamu kama binadamu wengine, wanahitaji upendo, kuheshimika na ikumbukwe ni watu wanaokuwa na mambo mengi, wanahitaji kuwa na mwenza mwelewa, wanapoona hawalipati hilo huamua kuishi wenyewe na watoto wao, ”anasema.
Anaeleza tofauti ya wanawake hao na wengine ni kuwa wao wanakua tayari wamejua vitu vingi, wamekwenda sehemu mbalimbali pengine duniani, kitu kinachowafanya wajione kuwa wako na nguvu na nafasi katika maamuzi ya familia na huona ni jambo la kawaida.
“Kwa upande wa wanaume hisia zao zisingependa kuwa chini ya kitu wanachoamini kuwa ni kidhaifu na wana uwezo wa kukitawala ndiyo maana wengi wanawaepuka wasomi wakihofia kuongozwa ilhali wao wanaamini kuwa ni viongozi.
“Mgongano huanzia hapo na wanawake hawa wasomi mara nyingi huona hamna shida kwani wana nguvu ya ziada inayoshabihishwa na ile elimu waliyonayo ambayo saa nyingine huweza kuwafanya kutoogopa chochote.
“Wanaume wangependelea wanawake wenye elimu za kawaida wasio na elimu kabisa kwa sababu wanaamini mwanaume anaongozwa na mwanamke hata kama sio kweli, kumbuka tamaduni zetu hasa za Kiafrika wanawake walikua n wa kukaa nyumbani kusubiri na siyo kwenda kwenye mahangaiko ya maisha, suala la wanawake kusoma ni changamoto kwao”anasema.
Kamongi anafafanua kuwa siyo kwamba wanawake wasomi ni wakorofi, wapo ambao huchukuliwa kila kitu pamoja na usomi wao, isipokuwa dhana iliyojengeka ndiyo tatizo.
Anasema inafikia mahali hata kama wawili hao wamependana watu wa nje na familia huvumisha kuwa mwanaume hajampenda huyo mwanamke amefuata fedha na ipo siku atamuacha.
Anafafanua dhana hizo na nyingine ndiyo zinawafanya wasomi wanawake kukosa wenza, kuolewa wakiwa wakubwa, au kuogopa kuolewa na wanaume kuwaogopa pia.