Bashiru ametema nyongo kusikostahili

Dar es Salaam. Dk Bashiru Ally ni mwanasiasa anayetamani kurudi kuwa Dk Bashiru mwana harakati wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam? Nimelazimika kuanza kwa kuhoji kutokana na mwenendo wa msomi huyu ambaye wiki iliyopita alizua sintofahamu ndani CCM.

Wiki iliyopita Dk Bashiru akihutubia mkutano wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata), mkoani Morogoro alisema mtandao huo sio chombo cha kutoa shukrani kwa yeyote yule, bali ni chombo cha kudai haki na heshima.

Msomi huyo alikwenda mbali zaidi akisema “...hata kinachoitwa amani, utulivu, mshikamano na umoja havipo kama jamii ya wakulima imekata tamaa. Mshikamano wenu uweze kufikisha ujumbe kwa hao wanaotuongoza, kauli zenu na misimo yenu iwatishe ili wawe upande wenu.

Baada ya kauli hiyo, Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kenani Kihongosi na baadhi ya wabunge wa chama hicho tawala, akiwemo Joseph Kasheku maarufu ‘Musukuma’ na Livingstone Lusinde ‘kibajaji walimshukia Dk Bashiru wakimtaka aombe radhi kwa kauli zake.

Sitaki kuingia kwa undani walichokisema kina Kibajaji, Musukuma na Kihongosi kuhusu mwanachama wao. Lakini niliposikia na kusoma kauli za Dk Bashiru sikushangaa, ndio maana katika maelezo ya hapo juu nimeanza kwa kuuliza Dk Bashiru ni mwanasiasa anayetamani kuwa Dk Bashiru mwanaharakati?

Kabla ya kuendelea mbele niwakumbushe Dk Bashiru alikuwa mhadhiri wa idara ya siasa (wanaita PSPA) ya Chuo Kikuu cha DSM kwa miaka mingi kabla ya kuteuliwa na Rais John Magufuli (hayati) kuwa mwenyekiti wa kamati ya kuhakiki mali za CCM.

Magufuli hakuishia hapo, alimteua Bashiru kuwa Katibu Mkuu wa CCM akichukua mikoba ya mtangulizi wake, Abdulrahman Kinana aliyeng’atuka nafasi hiyo Mei 28 mwaka 2018. Pia Dk Bashiru aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, akichukua nafasi ya Balozi John Kijazi baada ya kufariki dunia.

Hata hivyo, hakudumu katika kuhudumu ukatibu mkuu kiongozi baada ya Rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan kumteua Balozi Hussein Katanga kushika wadhifa huo, huku yeye akiteuliwa kuwa mbunge.

Wachambuzi wengi walitafsiri mabadiliko yale yaliyomfanya awe Katibu Mkuu Kiongozi aliyehudumu kwa muda mfupi kuwa ni anguko kubwa kwa safari yake ya kisiasa.

Walienda mbali na kushauri kuwa ulikuwa wakati mwafaka kwake kurudi chuoni na kuendelea na kazi ya kufundisha vijana. Hata hivyo, hilo lisingekuwa jambo rahisi kwa Dk Bashiru, kwani tayari kwa nafasi ya mafanikio aliyofikia asingeweza kumudu kuishi chuoni na kufundisha.

Akiwa chuoni, Dk Bashiru alijizolea sifa kemkemu za kuwa msomi mwenye msimamo mkali dhidi ya uvunjifu wa haki za binadamu na ukandamizaji wa haki za wanyonge. Alikuwa mtetezi mkubwa wa wakulima na alishiriki katika harakati nyingi za kuwatetea wananchi dhidi ya uporaji wa ardhi.

Alifanya kazi hizo kwa karibu sana na shirika la HakiArdhi. Alijitambulisha kama msomi aliyeiva katika nadharia za ujamaa na mfuasi mkubwa wa falsafa ya ujamaa ya Mwalimu Julius Nyerere.

Hata hivyo, Dk Bashiru baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM alibadilika na kuwa tofauti kabisa na yule aliyekuwa UDSM.

Aliacha kuwatetea wanasiasa wa vyama vya siasa, badala yake alionekana akitoa kauli nyingi zilizoashiria kuleta utata zilizodaiwa kutaka kukandamiza demokrasia na kukipendelea chama chake, CCM.

Ni katika kipindi chake vyama vya upinzani havikuruhusiwa kufanya siasa za majukwaani, lakini chama chake kiliendelea kufanya kazi za kisiasa bila kubughudhiwa.

Ni huyu huyu Dk Bashiru ambaye akiwa Katibu Mkuu wa CCM wanachama walihimizwa kuimba sifa za kumsifia Magufuli na Serikali yake.

Wasanii na wanamuziki mbalimbali walitunga nyimbo nyingi za kumsifia Magufuli kokote alikoenda na wale waliotunga nyimbo za kuikosoa CCM na wanasiasa wa upinzani walilazimishwa kuhamia CCM ili maisha yao yawe mazuri.

Wote tunakumbuka jinsi kipindi chake kulivyokuwa na wimbi kubwa la wanasiasa wa upinzani kuhamia CCM na wengine kuahidiwa vyeo na baadhi yao walivipata. Kilikuwa kipindi ambacho Dk Bashiru alikuwa mtendaji mkuu wa CCM.

Lakini Dk Bashiru, aliyekuwa kimya kwa muda mrefu, hivi karibuni ameibukia mkoani Morogoro kwenye Mviwata akionekana kuwakosoa wanaoimba nyimbo za kumsifia Rais.

Wengi wanaona kuwa Dk Bashiru alipata jukwaa la kutema nyongo kwa kilichotokea kwenye safari zake za kisiasa. Lakini kwa bahati mbaya anasahau kuwa yeye alipokuwa Katibu Mkuu wa CCM ndiye aliyeshiriki katika kuandaa nyimbo za kumsifia Magufuli.

Je, kutema kwake nyongo kunaashiria anataka kurudi kule alikokuwa, yaani Dk Bashiru wa UDSM aliyekuwa akiikosoa Serikali katika masuala mbalimbali yanayokwenda kinyume?

Lakini akumbuke kwa sasa yupo CCM, anapaswa kuwa makini na kauli zake, kwa jinsi CCM ilivyo wanachama hawawezi kumvumilia akiendelea hivi.