Bunge laongeza muda Rais Mnangagwa kutawala hadi 2030
Muktasari:
- Hatua hiyo inamaanisha kuwa muhula wa mwisho wa Mnangagwa, ambao kwa mujibu wa Katiba amewekewa ukomo wa mihula miwili, utaongezwa hadi mwaka 2030.
Zimbabwe. Seneti ya Zimbabwe imepitisha kwa kura nyingi marekebisho yenye utata ya Katiba ambayo yatamwezesha Rais Emmerson Mnangagwa kuendelea madarakani hadi mwaka 2030, hatua inayoyapa mabadiliko hayo uungwaji mkono wa Bunge baada ya kupata idhini ya awali kutoka Baraza la Taifa (National Assembly).
Marekebisho hayo yaliyopitishwa jana Jumatano Juni 24, 2026 ni miongoni mwa masuala ya kisiasa yaliyozua mjadala nchini humo, ambapo chama tawala cha Zanu-PF cha Mnangagwa mwenye umri wa miaka 83 kina wingi wa wabunge na kimekuwa madarakani tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 1980.
Rais wa Seneti, Mabel Chinomona amesema maseneta 75 walipiga kura kuunga mkono marekebisho hayo huku wanne wakiyapinga.
Muswada huo pia ulipitishwa kwa urahisi katika Baraza la Taifa Juni 18, ambapo wabunge 216 waliunga mkono na 42 waliupinga.
Ofisa mmoja amesema muswada huo utarejeshwa tena katika Baraza la Taifa kwa ajili ya kuridhia marekebisho ya kiufundi kabla ya kutiwa saini na Mnangagwa ili kuwa sheria.
Miongoni mwa mabadiliko hayo makubwa ambayo wakosoaji wameyataja kuwa ni mabadiliko ya kikatiba, kuna kipengele kinachoongeza muda wa muhula wa Rais na wa Bunge kutoka miaka mitano hadi miaka saba.
Hatua hiyo inamaanisha kuwa muhula wa mwisho wa Mnangagwa, ambao kwa mujibu wa Katiba amewekewa ukomo wa mihula miwili, utaongezwa hadi mwaka 2030.
Marekebisho mengine yanalipa Bunge mamlaka ya kumteua rais, na hivyo kuondoa uchaguzi wa moja kwa moja wa rais ambao ulianzishwa mwaka 1987, miaka saba baada ya Zimbabwe kupata uhuru.