Kwa mambo haya Zanzibar inaelekea wapi?

Muktasari:

  • Wakati ulipopatikana mwafaka wa tatu wa kutuliza mfarakano wa kisiasa wa zaidi ya miongo minne Zanzibar nilizungumzia katika safu hii umuhimu wa kauli za viongozi kutekelezwa kwa vitendo.

Wakati ulipopatikana mwafaka wa tatu wa kutuliza mfarakano wa kisiasa wa zaidi ya miongo minne Zanzibar nilizungumzia katika safu hii umuhimu wa kauli za viongozi kutekelezwa kwa vitendo.

Niliweka wazi kwa hili kwasababu ilikuwa lazima pande mbili zifanye kazi pamoja kuitengeneza Zanzibar. Pande hizo ndizo zilipaswa kuwapa Wazanzibari furaha, amani na kuaminiana.

Nilisema maelewano yasiishie katika uongozi wa juu tu, bali yafike mpaka kwenye mizizi.

Lililo muhimu ni kushauriana na kuaminiana. Hata Machi mwaka huu, nilieleza wasiwasi wangu juu ya mwendo wa mwafaka palipotokea kulaumiana.

Baadhi ya vongozi wa ACT- Wazalendo walidai Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilikuwa ya maneno tu na haionekani kwa vitendo na kwamba ilikuwa inaendeshwa kinyume na makubaliano. Hili wanalijua wahusika waliofanikisha huo mwafaka kwa sababu kilichokubaliwa hakikuwekwa hadharani.

Viongozi wa ACT Wazalendo walidai Rais, Dk. Hussein Mwinyi, alikuwa hawatendei haki Wazanzibari katika uteuzi wa nyadhifa muhimu, kama vile hawana elimu na uwezo wa kuongoza taasisi za umma.

Wapo waliodai uteuzi wa viongozi ulitegemea zaidi utashi wa kisiasa na sio uwezo wa mtu kwamba Wazanzibari walikuwa hawapewi nafasi za kushika nyadhifa muhimu katika Serikali na taasisi zake.

Hapo tena wakachomoza viongozi wa CCM kujibu mapigo na ikawa kunyoosheana vidole vya lawama kwa kauli zilizokuwa na cheche kali za moto ambazo nilizieleza kama za kuwasha moto na ukija kuwaka mzimaji nani?

Nikasema ni vizuri Wazanzibari na ndugu zao wa Bara wakatafakari hali iliyojitokeza na kujiuliza siasa za Zanzibar zinaelekea wapi au zilikuwa zinarudi zilikotoka ambapo chuki na uhasama vilisababisha mauaji na kufanyiana vitendo vya kinyama vilivyokosa utu na uungwana.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi katika mkutano wake wa kila mwezi na wahariri na waandishi wa habari alikataa kujibu shutuma zilizoelekezwa kwa Serikali yake na kusisitiza umuhimu wa kutumia mazungumzo kupata suluhisho mambo yasipokwenda sawa, badala ya kutumia majukwaa.

Nauliza baada ya sokomoko ile palifanyika kikao cha kutafuta maridhiano?

Mazungumzo ni muhmu, kwani hata huo mwafaka ulipatikana kupitia mazungumzo.

Niliuliza na leo narudia tangu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) mara ngapi viongozi wa pande hizi mbili walikutana kufanya tathimini ya utakelezaji wa mwafaka?

Nilishauri kuwepo na ratiba ya majadiliano angalau kila baada ya miezi mitatu ili kuepuka mikwaruzano.

Sasa limezuka jipya ambalo tukitaka tusitake limeteteresha misingi ya mwafaka na viongozi kupeana lawama.

Hii imetokana na uteuzi wa mara nyingine tena wa Thabit Faina Idarous kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi.

Hapa ikumbukwe kabla ya kufanyika uchaguzi wa 2020 ACT-Wazalendo walimlalamikia Idarous, hasa aliporuhusu zifanyike kura za mapema kwa vikosi vya ulinzi, pia aliwaengua wagombea zaidi ya 10 wa ACT-Wazalendo kwa maelezo ya kukosa sifa za kuwa wagombea.

Miongoi mwa walioenguliwa ni waliowahi kushika nafasi za juu za uongozi katika Serikali na kuwa wawakilishi au wabunge.

Kilichowaumiza zaidi ACT Wazalendo ni hakuwapo mgombea wa CCM aliyeenguliwa kwa kukosa sifa za kugombea.

Kwa wanaofuatilia siasa za Zanzibar hili halikushangaza, kwani hata marehemu Maalim Seif Sharif Hamad ambaye ni nguzo ya huo mwafaka aliwahi kuwekewa ngumu asiwe mgombea kwa vile Sheha wa Mtoni, mjini Unguja, alipokuwa anaishi alidai hamfahamu Maalim Seif.

Katika hali kama hii mtu aliyedaiwa (mimi sijui ukweli wake) kuvuruga uchaguzi anapoteuliwa tena huku ACT Wazalendo wakiwa na shaka naye tuseme nini?

Kwa mtazamo wangu angetafutwa mtu mwingine kushika nafasi hiyo ili kuepusha mgongano usiokuwa wa lazima.

Jingine ni je, hapakuwepo mashauriano? Je, mapendekezo ya kikosi kazi cha kuimarisha demokrasia visiwani ya kutaka nafasi hii itangazwe na watu wanaostahiki wagombee haikutiliwa maanani?

Jamani kwa lugha ya Wazanzibari tufanye mambo aste aste tukitilia maanani yaliyotukuta katika chaguzi zilizopita ambapo watu waliuawa na wengi kuwa vilema, mayatima na vizuka.

Ni vizuri kwa pande hizi mbili kukutana na kujadiliana haraka ili pasitokee mfarakano wa mwafaka kuvunjika na matokeo yake kuzusha balaa.

Wazanzibari wamechoshwa na siasa za chuki na uhasama zinazozalisha vizuka, mayatima na wakimbizi kwa sababu za uchaguzi.

Tujifunze kabla ya ulimwengu haujatupa funzo jingine na historia kutulaumu kwa kujali maslahi na utashi wa vyama vya kisiasa badala ya maslahi ya Zanzibar.

Najiuliza na sipati jawabu: Zanzibar inaeleka wapi?