Rais Samia anafundisha urais unavyopaswa kuwa katika nchi ya vyama vingi

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) pamoja na Wanachama wa Chama hicho kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Moshi Mkoani Kilimanjaro jana Jumatano, Machi 08, 2023. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Jumatano Machi 8, 2023 ilikuwa kilele cha Siku ya Wanawake Duniani. Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) linaadhimisha siku hiyo Moshi, Kilimanjaro. Kilichovutia zaidi ni mgeni rasmi, Rais Samia Suluhu Hassan.

Jana ilikuwa kilele cha Siku ya Wanawake Duniani. Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) linaadhimisha siku hiyo Moshi, Kilimanjaro. Kilichovutia zaidi ni mgeni rasmi, Rais Samia Suluhu Hassan.

Samia, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jumuiya ya wanawake wa chama chake ni UWT. Hata hivyo, Samia kwa kutambua kuwa yeye ni Rais wa wote, alipokea mwaliko wa Bawacha na kukubali.

Kwa mantiki hiyo, maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, kwa Tanzania, mwaka 2023, yanaweka alama muhimu ya siasa za upendo na maelewano. Kisha kuzika zama za uadui na visasi.

Bila shaka, Samia anatoa somo muhimu mno la jinsi ya kuwa rais katika nchi yenye kufuata mfumo wa vyama vingi. Kwamba ukiwa rais, wewe ni mali ya kila mwananchi. Waliokupigia kura na hata wale ambao hawakukuchagua.

Rais Samia anaonyesha kwa vitendo kuwa yeye ni Rais hata wa Chadema, chama kikuu cha upinzani kwa sasa. Hakuna tendo kubwa la uthibitisho kuliko hili la kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya wanawake ambayo yameandaliwa na Bawacha.

Tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa Julai 1992, marais wamekuwa wa CCM kuliko wa Watanzania wote. Unaweza kumweka pembeni Rais Ali Hassan Mwinyi, kwani wakati wake ndipo zama mpya za siasa zilizaliwa.

Mwinyi aliongoza nchi kwa miaka mitatu chini ya mfumo wa vyama vingi. Wakati wake, vyama vipya vilipata usajili na kulelewa, ikiwemo kupewa ruzuku. Uvumilivu ulikuwa mkubwa. Hakukuwa na bughudha kwa wapinzani.

Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa, alipoingia ofisini, alijikita kwenye kuimarisha CCM. Aina yake ya uongozi iliufanya urais wake kuwa wa CCM kuliko Watanzania wa vyama vyote. Hapo nagusia eneo la kisiasa.

Rais wa Nne, Jakaya Kikwete, kipindi chake upinzani uliimarika. Ni kwa sababu aliruhusu uhuru mkubwa kwa vyama na wanasiasa. Jakaya aliamini katika siasa za ushindani.

Mara kadhaa, Jakaya alikutana na wapinzani Ikulu na kujadiliana nao, hasa pale alipoona hali ya kisiasa imekuwa na wingu zito. Hivyo, kipindi hiki Samia anakutana na wapinzani na kujadili mustakabali wa nchi, dhahiri anaendelea pale alipoishia Jakaya.

Pamoja na mazingira bora ya kisiasa, vilevile urafiki alioudhihirisha Jakaya kwa wapinzani, bado wakati wote aliposimama, alibeba uhusika wa CCM.

Haukutokea wakati wowote, wapinzani walivutiwa kusimama mbele na kumwona Jakaya ni rais wa wote, kiasi cha kumwalika kwenye shughuli zao.

Tusimjadili kabisa Rais wa Tano, Dk John Magufuli, kwa sababu wakati wake siasa zilibeba sura ya uadui mkubwa. Hata maridhiano ya kisiasa yanayoendelea kufanyika hivi sasa, sababu ni yeye alikuza uhasama wa kisiasa.

Rais Samia Suluhu Hassan akiongoza Kikao cha majadiliano pamoja na Viongozi Wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema Ikulu Chamwino Jijini Dodoma Mei 20, 2022. Picha na Ikulu

Upekee wa Samia

Haikushangaza mwaka 1995, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipanda majukwaa ya CCM, kumwombea kura Mkapa, wakati huohuo, mwanaye, Makongoro Nyerere, alimnadi Augustino Mrema, aliyekuwa anawania urais kupitia NCCR-Mageuzi.

Haikutosha, Makongoro aligombea ubunge Arusha Mjini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi. Hivyo, tangu uchaguzi mkuu wa kwanza ulioshirikisha vyama vingi ndani ya Tanzania huru, Mwalimu Nyerere alitoa darasa kuwa siasa si uadui.

Haukutokea wakati wowote Mwalimu Nyerere alimwapiza Makongoro kwa sababu alichagua kushindana na chama alichokiasisi. Hakuna somo kubwa kwamba siasa sio uadui ambalo Mwalimu alilitoa kwa Watanzania kuliko hilo la yeye na Makongoro.

Joto la kisiasa mwaka 1995 lilikuwa kali. Wawania urais walishindana kumtembelea Mwalimu Nyerere, Msasani, Dar es Salaam. Mrema naye alikwenda Msasani, wakati alikuwa mgombea wa upinzani. Mwalimu alimpokea. Walizungumza.

Hivyo, Samia anapita kwenye njia za Jakaya ila amesogea mbele zaidi. Vilevile, anatembea kwenye misingi ya Mwalimu Nyerere. Kwamba upo wakati utasimamia masilahi ya chama, ila bila kusahau wajibu wako kama kiongozi wa Taifa.

Mwalimu Nyerere alipokuwa anafanya mikutano ya kampeni kumnadi Mkapa mwaka 1995, hakutembea na kauli mbiu ya mafiga matatu, kwa maana ya rais, mbunge na diwani, yeye alimwombea kura Mkapa, kisha akawaambia wananchi wanaweza kuchagua wabunge na madiwani kutoka upinzani.

Kwa mantiki hiyo, Mwalimu Nyerere alitaka vyama vya upinzani vipate uwakilishi, kuanzia bungeni mpaka kwenye mabaraza ya halmashauri. Zaidi, Mwalimu Nyerere alisema wananchi wangetaka wangeweza kuwapa wapinzani halmashauri hata ya Jiji la Dar es Salaam, lakini sio urais.

Mfano wa Mwalimu Nyerere ni kujenga hoja kwamba Rais Samia habuni siasa zake kwa kushirikiana na wapinzani, bali anairejesha nchi mahali siasa za vyama vingi zilipoanzia, kupitia malezi ya Mwinyi na Mwalimu Nyerere.

Jakaya alijitahidi kuulea upinzani, alipoingia Magufuli alikaribia kuuua kabisa. Rais Samia anafufua siasa za upinzani, anavipa uhai vyama na hadhi. Hata CCM watawaheshimu wapinzani, maana mwenyekiti wao anatenga muda na kushiriki shughuli zao.


Ndivyo siasa zinavyopaswa kuwa

Ukiwa mtawala wa nchi yoyote lazima ufahamu kuwa binadamu alipopewa mdomo, ulimi na sauti, maana yake uhuru wa kuzungumza, kutoa dukuduku, kuwasilisha mawazo yake na kadhalika ni haki yake ya kuzaliwa.

Jaribio lolote la kumfanya binadamu asiwe huru kusema alichonacho, huzaa ugomvi wa wazi au kimyakimya. Na kiasili, bora anayegombana nawe waziwazi kuliko kimyakimya.

Ugomvi wa wazi unajulikana, ila ule wa kimyakimya ni ububu. Kwamba unakuwa na ugomvi na mtu lakini hujui. Yaani anakugombeza kwenye fikra zake kila siku. Anakuchukia lakini mkikutana anatabasamu. Anakupigia makofi lakini moyoni amekununia.

Haki ya kuzungumza ni sawa kabisa na haki ya kufikiri na kuamua. Kila mtu amepewa ubongo wake, ndiyo maana kuna tofauti kubwa ya viwango na aina ya ufikiri kati ya mtu mmoja hadi mwingine.

Vivyo hivyo katika kuzungumza, kutoka binadamu mmoja hadi mwingine sauti hazifanani. Ujazo na ukali wa maneno ni tofauti. Ujengaji wa hoja haupo sawa. Ndiyo maana jambo moja likizungumzwa na mtu fulani unaweza kuona kero, akilisema mwingine ukatabasamu.

Ukiwa mtawala lazima ulijue hili kwa undani wake na uheshimu haki ya kuzaliwa ambayo binadamu wote wamepewa; kuzungumza, kufikiri, kukubali, kukataa na kadhalika.

Hapa pia ifahamike kuwa uhuru ambao ni haki asili ya binadamu, msingi wake siyo Katiba wala sheria za nchi. Katiba ambayo inamzuia mtu kutoa maoni yake au kuweka wazi dukuduku alilonalo, hiyo ni batili.

Katiba ya aina hiyo lazima iingie kwenye mgogoro na watu. Wananchi wataipinga waziwazi na wakishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya hofu, basi wataigombeza kimyakimya.

Ni kwa sababu hiyo hakuna utawala wowote ambao hukosa upinzani. Hata katika Taifa la chama kimoja, wanachama wa chama tawala hugawanyika na kuupinga uongozi unaokuwa madarakani na hata utawala wa nchi.

Katika nchi za kifalme ambazo siasa zimepigwa marufuku na hakuna kabisa vyama vya siasa, kama Bahrain, Kuwait, Saudi Arabia, Oman, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), bado wananchi hupingana na watawala kwa sauti au kimyakimya.

Zipo jamhuri za Micronesia, Palau na Tuvalu ambako siasa siyo shughuli halali na hakuna kabisa vyama vya siasa. Pamoja na hivyo, wananchi hufungua vinywa vyao na kutoa mawazo yao yenye kupingana na watawala.

Huo ni uthibitisho kuwa haki ya kuzungumza na kutoa maoni haisababishwi na uwepo wa wanasiasa, wala msingi wake siyo Katiba. Hiyo ni haki ya kuzaliwa ambayo mtawala kwa usalama wake hupaswa kuilinda.

Kufikia hapo, hakuna palipoacha shaka kuwa kinywa cha mtu hakipaswi kufungwa isipokuwa kiachwe wazi ili kusaidia watawala na wazungumzaji wenyewe. Mtu anapozungumza anakuwa ametoa la moyoni, kwa hiyo anapumua.

Mtu anapoona amebanwa pumzi na hupumui, hutapatapa ili aweze kupumua. Huko kutapatapa ndiyo hatari, kwani anaweza kufanya chochote mradi apate fursa ya kupumua.

Ipo nafuu kubwa ya mtawala endapo atawaacha watu wazungumze ili kujua sauti zao. Tena mtawala anapaswa kuwahimiza watu kuwa wazi ili ayajue zaidi mawazo ya watu anaowaongoza.

Ukizijua fikra za unayemtawala ndipo utaweza kumtawala kwa uzuri zaidi. Maana unajua anachokifikiria, kwa hiyo utaweza kupita kwenye mawazo yake na hata ikiwa kinyume na anachowaza, basi utakuwa na majibu yenye kumridhisha.

Namwona Rais Samia akifanya vema kukumbatia wapinzani. Kuruhusu watu wazungumze. Kukubali mikutano ya hadhara. Hiyo inamfanya aongoze kwa urahisi, maana atakuwa anazijua fikra za anaowaongoza.

Kutumia nguvu nyingi kuwakabili wapinzani ni mtindo wa hovyo. Waache wafanye siasa. Nawe fanya upande wako. Wananchi wataona nani anafaa kwa kesho ya taifa lao.

Matendo machache tu, tayari Rais Samia anapokea pongezi kila upande. Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu, anakiri mpaka mitandaoni kuwa Rais Samia anafanya mambo makubwa ambayo awali hakuyatarajia.

Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, anasema Samia ni rais wa wote. Anatolea mfano yeye alipomwalika kwenye tukio lake la kuadhimisha miaka 30 kwenye muziki, naye akakubali kuwa mgeni rasmi. Tukio hilo lilifanyika Mei 31, 2022, Serena Hotel, Dar es Salaam.

Hata Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amekuwa akirejea mara nyingi kutoa sifa kwa Rais Samia, kama ambavyo Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amekuwa akifanya. Ni wazi kwamba ukitoa uhuru wa kisiasa na kushirikiana na wapinzani, hutakuwa adui. Utasifiwa na kupongezwa hata katika majukwaa ya upinzani.

Dunia haisimami na siku hazina sumaku. Zinatembea. Anachokifanya Rais Samia, kitambeba na kumheshimisha katika historia kama kiongozi aliyebadili upepo wa kisiasa nchini kwa kuingiza “upendo” katika ya chuki iliyotamalaki.

Na historia itamkumbuka na kumweka huru kama rais wa mfano kwenye nchi inayofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.