Tusiendelee kujenga jamii ya watu wanafiki

Kuna tabia inaanza kuchipuka nchini ambayo bila kuipiga vita tunaweza kujikuta tunajenga jamii au Taifa la watu wenye tabia ya unafiki.

Kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili, unafiki ni hali ya kujifanya kuwa rafiki ilhali ni adui. Ni hali ya kutokuwa mkweli.

Mnafiki anaweza kupindisha ukweli kwa nia ya kujinufaisha, kujipendekeza au kumfurahisha mtu au kikundi cha watu.

Mwenye tabia ya unafiki hutenda kinyume cha ukweli, uhalisia, dhamira na nafsi yake.

Tabia ya unafiki ina madhara ya muda mfupi, kati na mrefu kwa makundi yote mawili; kundi la wanafiki na wanaofanyiwa unafiki.

Upo usemi wa wahenga kuwa “kijana mnafiki akizeeka anakuwa mchawi” ni uthibitisho wa ubaya wa unafiki.

Watu wanafiki wapo katika awamu zote za uongozi wa Taifa hili kuanzia ile ya awamu ya kwanza, pili, tatu, nne na tano.

Katika awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere alifichua siri ya baadhi ya wasaidizi wake kumsihi asing’atuke wakidai hakuna mwenye kuweza kuvaa viatu vyake vya uongozi.

Baadaye, anasema aligundua kuwa watu hao (wanafiki) walilenga kulinda nyadhifa zao ambazo hawakuwa na uhakika nazo kwenye uongozi mpya.

Hata sasa watu hao wapo. Ndiyo wale wanaohamasisha ukomo wa muda wa urais kuondolewa kwenye Katiba kwa sababu zilezile zilizotolewa na wasaidizi wa Mwalimu Nyerere miaka mingi iliyopita.

Mifano ni Mingi. Kwa leo nitataja machache ambayo kwa mtazamo wangu inasukumwa ama na masilahi binafsi, makundi au itikadi za wahusika.

Mfano mmojawapo ni kuhusu Sheria na kanuni za kikokotoo cha mafao ya wafanyakazi iliyolalamikiwa na makundi ya wafanyakazi kupitia vyama vyao, wanasiasa kutoka vyama shindani na CCM.

Sheria hiyo ililalamikiwa kuwa haina uhalisia kwa baadhi ya kada za wafanyakazi, hasa wenye ajira za mikataba ya muda mfupi.

Mbunge wa Bunda mjini, Esther Bulaya (Chadema) alikuwa miongoni mwa wanasiasa waliopinga sheria hiyo na kuiomba Serikali kuifanyia marekebisho.

Wanaojipambanua kuunga mkono Serikali walimwandama Bulaya na kila aliyeonyesha matundu kwenye sheria hiyo.

Waliitisha mikutano ya waandishi wa habari, makongamano na vikao kadhaa kuelezea uzuri wa sheria hiyo na kuwanga kwa kila aina ya jina walioonyesha kasoro zake.

Hilo ni tisa, kumi ilikuwa siku Rais John Magufuli alipoeleza kasaro za sheria hiyo; watu walewale waliokuwa wanaisifu sheria, kwa mtindo uleule walijitokeza kuunga mkono kauli ya Rais.

Pamoja na ukweli kuwa Rais Magufuli ameleta ladha tofauti kuanzia kwenye usimamizi wa fedha na rasilimali za umma, nidhamu ya utumishi na ufanyaji wa maamuzi na kutenda kiasi cha kustahili pongezi, bado kuna dalili za unafiki unaibuka miongoni mwa baadhi ya viongozi kwa kupongeza kila kitu hata pale walipotakiwa kushauri kwa njia tofauti.

Baadhi ya wabunge na viongozi wa Serikali ambao awali walikuwa vyama shindani kabla ya kuhamia CCM nao hawakubaki nyuma kuonyesha rangi zao za kinafiki ndani na nje ya Bunge kwa kuvihusisha vyama vya awali na matukio ya kihalifu yaliyogharimu maisha ya Watanzania.

Ili kunusuru jamii na Taifa, kila mmoja wetu popote alipo na kwa nafasi yake ajitokeze kupinga aina na dalili zozote za unafiki ili kuinusuru jamii na Taifa. Ukweli uwe ukweli na usemwe kama ulivyo bila kuopindishwa.