ACT -Wazalendo yaijibu Chadema madai ya usaliti
Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo (Bara), Isihaka Mchinjita, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- ACT-Wazalendo imesema haijasaliti hatua yake kusaini tamko la pamoja la maridhiano ya kisiasa Zanzibar
Dar es Salaam. Siku moja baada ya Chadema kuituhumu ACT-Wazalendo kwa kile ilichodai ni usaliti kutokana na kusaini tamko la pamoja la maridhiano ya kisiasa Zanzibar na CCM, chama hicho kimesema hakijasaliti misingi yake, bali kimetekeleza wajibu wake wa kisiasa kwa masilahi ya Wazanzibari.
ACT-Wazalendo imesema wao ndio chama pekee, kina wajibu na ushawishi wa kutosha, ukiondoa CCM Zanzibar, hivyo kuna madhara yanayotokea visiwani humo yanayogusa wanachama wao na wana wajibu kuhakikisha kunakuwa na mustakabali mzuri.
Jana, Ijumaa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika aliwaambia wanahabari Chadema imefuatilia tamko la pamoja la maridhiano ya kisiasa lililosainiwa baina ya CCM na ACT-Wazalendo akisema wakati mwafaka chama hicho kitatoa tamko.
“Zanzibar ni sahihi kuleta wasuluhishi wa kimataifa huku bara si sahihi, tutazungumza wakati ukifika na tutoa mwelekeo. Ninachokiona ACT-Wazalendo kwa mara nyingine tena, pamoja na yaliyotokea Oktoba 29,2025 imesaliti damu za watu na harakati za mabadiliko,” amedai Mnyika.
Hata hivyo, leo Jumamosi Julai 11,2026 Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita amewaambia wanahabari kinachofanyika Zanzibar si kipya bali mwendelezo wa mapambano yaliyoanza mwaka 1995.
“Hatua ambayo Tanzania bara imeipitia mwaka 2025, ni hatua ambayo Zanzibar iliipitia mwaka 2000.Yale mengine ambayo tunayadai huku bara, Zanzibar yalishafanyika, hatuanzi upya Zanzibar bali tunaendelea mbele,” amesema Mchinjita.
Jana, Mnyika alisema miongoni mwa mambo yatakayofanyiwa kazi katika maridhiano ACT na CCM ni Katiba ya Zanzibar, akisema huwezi kushughulikia hilo pasipo kuyafanyia kazi upungufu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Mchinjita amemtaka Mnyika kuwasiliana na viongozi wenzake wa Chadema wa Zanzibar kupata ufafanuzi wa kile kilichotokea Julai 9, 2026 kuhusu tamko la maridhiano hilo na yale anayoyaona si sawa sawa.
“Mnyika anasema ni usaliti kujadili Katiba ya Zanzibar huku tukiacha ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, hiki ni kituko na ujuzi mdogo wa sheria.
“Katiba ya Zanzibar haijawahi hata mara moja kutungwa pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzani,” ameeleza.
Mchinjita amedai kuwa, Mnyika hakuwa na hoja za msingi kuhusu suala hilo na hakuna mahali palipoandikwa kwamba Wazanzibari wakitaka kuandika Katiba basi wanapaswa kuisubiri ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kuhusu tamko la pamoja la maridhiano
Mchinjita amesema mazungumzo baina yao na CCM hayakulenga kugawana nafasi za uongozi bali yalilenga kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto za kisiasa zinazoikabili Zanzibar kwa kuenzi malengo ya maridhiano yaliyoasisiwa kupitia Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010.
“Mageuzi ya kisiasa ndiyo yalikuwa ajenda kuu ya ACT-Wazalendo. Katika mazungumzo yote yaliyofanyika, ACT- Wazalendo haikuwahi kuweka kipaumbele cha kujadili kuingia au kutokuingia serikalini,” amesema.
Mchinjita amefafanua kuwa kipaumbele cha ACT- Wazalendo kilikuwa kuhakikisha kunakuwepo makubaliano ya kisera na ya kimuundo yatakayoweka msingi wa mageuzi ya kisiasa, kuimarisha demokrasia, kulinda haki za wananchi na kuzuia kujirudia kwa migogoro ya kisiasa siku zijazo.
Amesema tamko la pamoja hilo linaashiria mwanzo wa utekelezaji wa makubaliano ambayo hadi Mei 2026, pande zote zilikuwa zimekamilisha majadiliano kuhusu ajenda muhimu za mageuzi na kukubaliana hatua inayofuata ni kuanzisha mfumo wa kisheria na kitaasisi wa kusimamia utekelezaji wake.
“ACT-Wazalendo ilikubaliana kushiriki hatua hiyo ya utekelezaji bila kuweka sharti la kuingia mara moja katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa,”
“Iwapo utekelezaji wa makubaliano hayo utafikia hatua ambayo, kwa mujibu wa makubaliano na sheria, itahitaji kuundwa au kukamilishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ndipo suala hilo litashughulikiwa kwa wakati wake,” amesema.
Mchinjita amesema ACT- Wazalendo inatoa wito wa ushirikiano katika utekelezaji wa makubaliano hayo ikiamini mafanikio ya mchakato huo hayatategemea tamko pekee, bali yatategemea dhamira ya kweli ya pande zote kutekeleza kwa uaminifu yale yaliyokubaliwa.
“Msimamo wetu kuhusu Tanzania Bara haujabadilika. Tunapenda kuweka wazi tamko la Pamoja la Zanzibar halibadilishi kwa namna yoyote msimamo wa yaliyotokea katika uchaguzi wa Oktoba 29,2025,” amesisitiza.
Kwa mujibu wa Mchinjita, ACT-Wazalendo inaendelea kuamini kuwa maridhiano ya kweli yanapaswa kujengwa juu ya misingi ya haki, ukweli, usawa na kuheshimiana.
“ACT- Wazalendo itaendelea kushiriki kwa dhati katika juhudi zote za kujenga Taifa lenye umoja, haki, demokrasia na ustawi kwa wananchi wote,” ameeleza.