Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT -Wazalendo yawaandaa makada wake kupokea tamko la maridhiano

Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT Wazalendo, Salim Bimani.

Muktasari:

  • Tamko hilo la maridhiano litakalosainiwa Ikulu, Zanzibar linalenga kuimarisha maridhiano, mshikamano, utulivu wa kisiasa, amani na ustawi wa kisiwa hicho, litashuhudiwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi na Mwenyekiti wa ACT -Wazalendo, Othman Masoud.

Dar es Salaam. Wakati kesho Alhamisi ya Julai 9, 2026, Chama cha  ACT- Wazalendo na Chama cha Mapinduzi (CCM) vikitoa tamko la pamoja la maridhiano ya kisiasa Zanzibar, chama hicho cha upinzani kimewataka wanachama wake kulipokea kwa moyo mkunjufu tamko hilo.

Mbali na hilo, ACT Wazalendo kimewataka wanachama wake kulijadili kwa staha, na kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wake.

Tamko hilo la maridhiano litakalosainiwa Ikulu, Zanzibar linalenga kuimarisha maridhiano, mshikamano, utulivu wa kisiasa, amani na ustawi wa kisiwa hicho, litashuhudiwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud.

Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumatano Julai 8,2027 na Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT Wazalendo, Salim Bimani imeeleza katika mchakato huo, mshindi si chama fulani bali ni Zanzibar.

“Tunawashukuru kwa dhati wananchi wa Zanzibar, hasa wanachama na wafuasi wetu wa ACT Wazalendo, kwa kuonesha upevu mkubwa wa kisiasa, utulivu, na imani kwa uongozi wenu katika mchakato huu uliodumu kwa miezi minane.”

“Katika hatua ya sasa, tunawaomba na kuwasihi mlipokee tamko la pamoja kwa mioyo mikunjufu,” amesema Bimani.

Bimani amesema ACT- Wazalendo inaingia tena kwenye mchakato huo wa kuyajenga maridhiano na Umoja wa Kitaifa kwa imani, dhati, na moyo uleule uliorithishwa na mwasisi wao, Maalim Seif Sharif Hamad (marehemu).

“Kinachoweza kupatikana kwa njia ya amani na majadiliano kina thamani kubwa na endelevu kuliko kile kinachopatikana kwa njia ya machafuko. Huu ndio msingi mkuu uliotujenga.”

“Licha ya changamoto tulizowahi kukumbana nazo huko nyuma, msimamo wa ACT- Wazalendo unabaki thabiti: Zanzibar ni kubwa kuliko chama chetu, na ustawi wa Wazanzibari una thamani kubwa kuliko vyeo na madaraka ya viongozi,” ameeleza.

Bimani amesema ACT- Wazalendo, inawashukuru viongozi wakuu kwa busara zilizofanikisha mchakato huo ambapo walitanguliza masilahi mapana ya Zanzibar.

Mazungumzo ya kutafuta mwafaka Zanzibar, yaliyotawaliwa na vuta, nikuvute yalianza Novemba mwaka 2025 yakisimamiwa na Amani Abeid Karume na Dk Ali Mohamed Shein (marais wastaafu Zanzibar) kwa CCM.

Wakati ACT -Wazalendo waliwakilishwa na Juma Duni Haji (Mwenyekit Mstaafu wa ACT Wazalendo) na Othman Masoud Othman (Mwenyekiti wa ACT Wazalendo).