ACT: Wazanzibari kuweni wamoja haki za Muungano

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Juma Haji Duni ‘Babu Duni’ amesema Zanzibar inaminywa kwenye haki za msingi katika Muungano, hivyo kuwataka Wazanzibari kuweka kando tofauti zao za kiitikadi na kutetea maslahi ya Taifa hilo.

Alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa hadhara wa chama hicho katika viwanja vya Mjini Unguja na kusema wakati wa mchakato wa Katiba mpya mwaka 2014 baadhi ya wananchi hususani kutoka CCM waliwasaliti.

"Ndugu zangu Wazanzibari masuala haya hayataki chama linapokuja suala la maslahi ya Zanzibar, lazima tuwe kitu kimoja tutetee nchi yetu.
Alisema ndani (Zanzibar) wanaweza kuwa na tofauti zao ila wanapokwenda kudai haki zao nje ya nchi wanatakiwa wawe na kauli moja.

Babu Duni alisema viongozi wa chama hicho wamekutana na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na kumueleza kuwa ana deni liliachwa na marehemu Maalim Seif Sharif Hamad ambayo ni kujenga maridhiano.

"Tunaimani kwamba kamati iliyoundwa ya maridhiano italeta matumaini na ufumbuzi, ili uchaguzi wa 2025 twende kwa amani na utulivu," alisema na kuwataka wananchi wahudhurie mikutano ya hadhara waelezwe mambo ya msingi yatakayowapa utulivu.

Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud alisema chama hicho kina maono ambayo ni Zanzibar mpya akisema iwapo wakiendelea na Zanzibar ilivyo hawatafika popote. “Tumesema tutajenga nchi moja na watu wote wana haki sawa...

Zanzibar ni mchaganyiko wa watu huwezi kuwabagua kwa rangi wala asili yao," alisema Othman. Pia alisema ahadi ya chama hicho ni kujenga Zanzibar yenye mamlaka kamili na kwamba wananchi wake wanashindwa kufika wanapotaka kwa sababu hakuna mamlaka na watu hao hawana uwezo wa kujiamulia mambo yao. Alisema wamejenga subra kwa muda mrefu, lakini sasa ifike hatua subra iwekwe kando.

‘Kama tunataka kutimiza maono yetu lazima tuwe na mamlaka ya kuendesha nchi yetu, hayo yote yataelezwa. Tuhakikishe tunakwenda kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi yale ya mabavu yamepitwa na wakati sio ya kizazi hiki tena,” alisema..

Makamu Mwenyekiti ngome ya vijana ACT Wazalendo, Khadija Anwar Mohamed alisema kumeibuka kauli za kibaguzi zinazotolewa na viongozi hadharani, hivyo wanapaswa kuzipinga kwa umoja wao.
Mkutano huo ni safari ya mikutano 12 itakayofanywa na viongozi wa chama hicho kwa Unguja na Pemba.