ACT wazindua kampeni za ubunge Amani Zanzibar

Muktasari:

ACT iliyomsimamisha Mohamed Khamis Mohamed inachuana na CCM, kilichotangulia kuzindua kampeni zake tangu  Desemba 1, 2022 kwa kumnadi mgombea wake chama hicho, Abdul Yussuf Maalim.

Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimezindua kampeni zake katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Aman mjini Unguja, kikiwataka wananchi kukichagua ili kuwaletea maendeleo.

Uchaguzi wa kumpata mbunge wa jimbo hilo unatarajiwa kufanyika Desemba 17, mwaka huu ili kuziba nafasi ya aliyekuwa Mbunge wake, Mussa Hassan Mussa aliyefariki Dunia Oktoba 10, 2022.

ACT iliyomsimamisha Mohamed Khamis Mohamed inachuana na CCM, kilichotangulia kuzindua kampeni zake tangu  Desemba 1, 2022 kwa kumnadi mgombea wake chama hicho, Abdul Yussuf Maalim.

 Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Kampeni hizo zilizofanyika viwanja vya Masumbani jimbo la Amani Zanzibar leo Desemba 8, Mjumbe wa kamati kuu ya ACT-Wazalendo, Ismail Jussa amesema CCM haiwezi kuleta mageuzi ya kuwaondolea dhiki zinazowakabili wananchi wake.

“Kwakipindi chote tangu kuingia mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1995 wamekuwa wakiahidi majukwaani lakini hakuna utekelezaji.

“Hawawezi kufanya lolote kwa sababu CCM, haikuanzishwa kutumikia watu na badala yake kinatumika kuwakandamiza watu, kuwatafunia haki na kuwadhulumu,” amesema Jussa.

Amesema wananchi wa jimbo hilo wana dhiki zinazofanana na majimbo mengine nchini wanakabiliwa na mfumuko wa bei ya vyakula, changamoto ya maji safi na salama pamoja na ufukara ambao kwa kiasi kikubwa ni ufundo unaonuka kwenye kila nyumba ya mtanzania.

“Chama chetu kinajua tukipata mamlaka kamili tutaweza kumaliza dhiki zinazotusumbua Zanzibar haina mamlaka kamili kila kitu wanategemea kuletewa mipango kutoka Tanzania bara jambo ambalo sisi haturiziki nalo,” amesema.

Naye Katibu mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu amesema uchauguzi huo ni fursa kwa Tume ya Taifa ya  Uchaguzi (NEC), kutengeneza muelekeo mpya wa kisiasa  kwa kuzingatia maoni ya kikosi Kazi kilichoundwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Shaibu pia aligusia kuwa kudai chama hicho bado kinafuatilia maisha ya Wazanzibari, ambapo kwa tathimini waliyofanya hawaridhiki na maisha wanayoishi.

“Uchaguzi huu mnapaswa kutumia fursa kukataa utawala wa chama cha Mapinduzi kuonesha wanayofanya siyo sahihi na kuichagua ACT inayojua na kutambua matamanio ya wananchi tumpe mgombea kura za kutosha,” amesema.

Kuhusu wasiwasi yao juu ya uteuzi wa bosi mpya wa Tume ya Uchaguzi ya Zabzibar (ZEC), Thabit Idarous Faina, amesema;

“Sisi ACT Wazalendo kwa mienendo ya hivi karibuni, tunatilia shaka nia ya wenzetu katika kuyaenzi maridhiano ambayo ndiyo tunu ya kumkomboa Mzanzibar na kuwaleta pamoja nakuwaletia tija ya kiuchumi na kijamii na mshikamano wao wa pamoja,” amesema Shaibu.