Ado ataka kizazi kipya kuwa chachu mabadiliko ya jamii
Katibu Mkuu ACT Wazalendo, Ado Shaibu akizungumza katika hafla ya kuwapokea wanachama wapya kutoka vyuo vikuu, jijini Dar es Salaam Juni 14, 2026. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Ameeleza umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika harakati za kisiasa na kijamii, akisema hakuna mapinduzi yanayoweza kufanikiwa bila ushiriki wao.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amewataka vijana wapya waliojiunga na chama hicho kutambua wajibu wao wa kupigania masilahi ya umma, haki bila ubaguzi na demokrasia ya kweli, akisisitiza vijana ndiyo nguvu muhimu katika kuleta mabadiliko ya kijamii na kisiasa nchini.
Amezungumza hayo leo Jumapili, Juni 14, 2026 Makao Makuu ya ACT-Wazalendo yaliyopo Magomeni, jijini Dar es Salaam, alipokuwa mgeni rasmi kwenye hafla maalumu ya kuwapokea wanachama wapya 128 kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini.
Amesema harakati za wanafunzi wa vyuo vikuu si jambo jipya, bali ni sehemu ya historia ya mapambano ya kijamii na kisiasa, hivyo vijana wanapaswa kujiandaa kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa, ikiwemo maendeleo ya teknolojia ya Akili Unde (AI) na tatizo la ukosefu wa ajira.
“Msikatishwe tamaa kwa kuambiwa kuwa mkijiunga na upinzani hamtapata ajira. Ukweli ni kwamba ajira zenyewe ni changamoto kubwa kwa vijana wengi nchini, kwanza wanavyuo wengi ni waathirika wa mifumo iliyopo hivyo lazima msimame kupigania mambo haya matatu," amesema.
Amesema hatua ya vijana hao kujiunga na ACT-Wazalendo imetokana na uamuzi wao wenyewe, jambo ambalo ni nadra kujitokeza kwa idadi kubwa kwa wakati mmoja, hivyo chama hicho kimejipanga kuimarisha harakati za kisiasa vyuoni kupitia Ngome ya Vijana, kwa lengo la kuibua kizazi kipya cha viongozi wenye maono ya mabadiliko.
Ado ameeleza umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika harakati za kisiasa na kijamii, akisema hakuna mapinduzi yanayoweza kufanikiwa bila ushiriki wao.
“Wanawake ni nguzo muhimu katika mafanikio ya harakati yoyote ya mabadiliko. Kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wa kike wanaojiunga na chama hiki ni ishara ya matumaini makubwa kwa mustakabali wa harakati hizi,” amesema.
Amewataka wanachama hao wapya kutambua ACT-Wazalendo ni chama kinachopigania maslahi ya wananchi wote na si ya viongozi au wanachama wake pekee.
Amesema chama hicho kina wajibu wa kusimamia maslahi ya umma kwa ujasiri na bila kuyumbishwa na mazingira yoyote, kwani wananchi hutambua na kuhukumu mwenendo wa vyama vya siasa kulingana na namna vinavyosimamia masilahi yao.
"Vijana nawahimiza kuwa watu wa kuhoji, kufikiri kwa kina na kutafuta ukweli badala ya kukubali kila wanachoelezwa bila uchambuzi, akisema hatua hiyo itasaidia kujenga jamii yenye uwajibikaji na usawa, katika kupigania masilahi ya wananchi," amesema.
Kuhusu demokrasia, amesema moja ya majukumu makubwa ya ACT-Wazalendo ni kupigania mfumo wa demokrasia unaozingatia haki, uwajibikaji, utawala wa sheria, Katiba Mpya na ulinzi wa haki za binadamu.
“Tunapaswa kutetea haki za watu wote bila kujali tofauti zao za kisiasa. Wananchi wanapaswa kutuona kama chombo cha matumaini yao katika kupigania haki na maendeleo,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, Abdul Nondo, amesema mapambano ya kutetea haki za vijana hayawezi kupata mafanikio ya kweli ikiwa wanafunzi wa vyuo vikuu wataendelea kujitenga na siasa na masuala ya maendeleo ya taifa.
Amesema ingawa wanafunzi wana taasisi zinazowaunganisha, bado hazijaonyesha nguvu ya kutosha katika kusimamia maslahi yao, hivyo kuna umuhimu wa vijana kushiriki kikamilifu katika harakati za kuleta mabadiliko.
Nondo amesema chama hicho ni jukwaa sahihi kwa vijana wanaotamani kuona Tanzania yenye haki, usawa na uwajibikaji wa viongozi.
“Nchi hii ni mali ya Watanzania wote. Hatuwezi kuacha maamuzi yanayohusu maisha yetu yafanywe bila ushiriki wetu. Siasa zinaathiri ajira, elimu, mikopo ya wanafunzi na ustawi wa jamii kwa ujumla,” amesema.
Amesema changamoto nyingi zinazowakabili vijana, ikiwemo ukosefu wa ajira, rushwa na huduma duni za kijamii, zinatokana na maamuzi ya kisiasa, hivyo haiwezekani kujitenga na siasa huku ukitarajia kuona mabadiliko.
Nondo aliwataka vijana wenye maono ya kuona Taifa bora kutokaa kimya wanapoona maamuzi yasiyo na tija kwa wananchi, akisema ukimya katika nyakati za changamoto ni sawa na kuacha matatizo yaendelee.
Wanachama wapya waliopokelewa katika hafla hiyo wanatoka katika vyuo mbalimbali, vikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Taifa cha Usafirshaji (NIT), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Biashara (CBC), Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Kampala, Chuo cha Ustawi wa Jamii na Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA).