Prime
Ado azuiwa kufanya mkutano, aibua mjadala
Muktasari:
- Polisi Ruvuma wasema wamezuia mkutano huo kwa kutekeleza zuio la mikutano ya kisiasa lililotolewa na Serikali. Mjadala waibuka kuhusu mipaka kati ya shughuli za kisiasa na za kibunge.
Dar es Salaam. Licha ya Serikali kutangaza kuwa zuio la mikutano ya hadhara linavihusu vyama vya siasa pekee, mbunge wa Tunduru Kaskazini (ACT Wazalendo), Ado Shaibu, amelalamikia kuzuiwa kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wake.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma, uamuzi wa kuzuia mkutano wa mbunge huyo unatokana na zuio lililotangazwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, Juni 26, mwaka huu, kutokana na sababu za kiusalama.
Akizungumza na Mwananchi leo, Julai 14, 2026 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya, amesema tangazo la zuio la vibali vya mikutano ya hadhara lilitolewa na waziri hadharani.
Ameeleza kuwa kilichofanywa na Jeshi la Polisi ni utekelezaji wa agizo hilo, akisisitiza kuwa Ado ni kiongozi na ana uwezo wa kufuata njia sahihi za kuuliza ili apewe ufafanuzi wa kina.
“Kitu pekee anachoweza kufanya ni mkutano wa ndani, hilo limeruhusiwa, lakini si mkutano wa hadhara. Maana tangazo lilitangazwa hadharani,” amesema Chilya.
Amesisitiza kuwa Ado anapaswa kufuata vyanzo sahihi ili kuomba ufafanuzi kuhusu zuio hilo na kupata maelezo ya kina.
Hata hivyo, Ado amesema zuio la Serikali lilihusu mikutano ya kisiasa, lakini yeye anatekeleza shughuli zake za kibunge, hivyo kumzuia ni kukiuka Kifungu cha 4 cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, Sura ya 296.
Mkanganyiko huo ulioibuka umewaibua wadau wa siasa, wanaosema kunahitajika ufafanuzi kuhusu mipaka ya zuio la mikutano ya hadhara, huku mashaka ya upendeleo yakiibuka kwa hoja kuwa, kwa nini kuna wabunge wanaendelea na mikutano.
Julai 10, mwaka huu, mbunge wa Makambako, Festo Sanga, alifanya ziara na mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Maleutsi, jimboni humo.
Siku mbili baada ya kutangazwa zuio hilo la mikutano ya hadhara, mbunge wa Ikungi Magharibi, Elibariki Kingu, alikutana hadharani na kundi la vijana wa bodaboda, kuzungumza nao na kuwachangia Sh5 milioni kwa ajili ya mtaji.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohamed Mahmoud, aliwahi kuiambia Mwananchi kuwa zuio hilo la mikutano ya hadhara haliwahusu wabunge, kwa kuwa shughuli zao si siasa, bali ni kupeleka mrejesho kwa wananchi.
Malalamiko ya Ado
Katika barua yake ya kulalamikia zuio hilo kwa Spika wa Bunge, Ado amesema Jeshi la Polisi limemzuia kutekeleza shughuli zake za kibunge, akidai hatua hiyo inakiuka Kifungu cha 4 cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, Sura ya 296.
Amesema sheria hiyo inampa mbunge uhuru wa kufanya mikutano ya hadhara katika jimbo lake na inazitaka mamlaka husika kuwezesha shughuli hizo. Pia, mtu yeyote anayezuia au kushiriki kuzuia mikutano hiyo anatenda kosa kwa mujibu wa sheria.
Ado amesema baada ya kuhitimishwa kwa Bunge la Bajeti, alipanga ziara rasmi jimboni kwake kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo, kutoa mrejesho wa shughuli za Bunge na kukusanya maoni ya wananchi kuhusu masuala yanayowahusu.
Amesema ratiba ya ziara hiyo iliwasilishwa kwa mkuu wa wilaya, OCD na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kama taarifa kwa wadau muhimu wa utekelezaji wa shughuli hizo.
Kwa mujibu wa Ado, Julai 11, 2026, alipanga kufanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Baraza la Idd, Tunduru, lakini OCD alimjulisha kuwa mkutano huo umepigwa marufuku kutokana na zuio la mikutano ya kisiasa.
“Baadaye askari walifika eneo la mkutano, wakaagiza vifaa vya sauti vizimwe na kuwatawanya wananchi waliokuwa wameanza kujikusanya. Kwa maoni yangu, hatua hizo zilikiuka sheria inayolinda shughuli za kibunge,” amesema.
Ado amesema alikutana na OCD na kueleza kuwa zuio la mikutano ya kisiasa halihusu shughuli halali za kibunge. Pia, aliwasiliana na Inspekta Jenerali wa Polisi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kutafuta ufumbuzi.
Hata hivyo, amesema hadi Julai 13 hakupata mrejesho wowote. Kutokana na hali hiyo, amemwomba Spika kuingilia kati, kufuatilia sababu za hatua zilizochukuliwa na kutoa mwongozo kwa mamlaka husika ili matukio kama hayo yasijirudie.
Serikali ilishasema wabunge ruhusa
Ado anakutana na hayo, wiki moja tangu gazeti hili lilipoandika habari likimnukuu Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohamed Mahmoud, aliyesema zuio la mikutano ya hadhara haliwahusu wabunge.
Alisema mbunge anaporudi jimboni kuzungumza na wananchi hawakilishi chama cha siasa, bali anapeleka mrejesho kwa waliomtuma.
“Jukumu la mbunge anapotoka bungeni ni kurudi kwa wananchi kuwaambia walichopata kutoka kwenye Bunge. Ile siyo siasa. Wameshatekeleza wajibu waliopewa na wananchi kusema bungeni, na wanarudi kupeleka mrejesho,” alisema.
Alieleza kuwa hiyo ni tofauti na anapotoka kiongozi wa chama, kwani chochote atakachokizungumza na kukifanya kitakuwa siasa.
“Ndiyo maana agizo la waziri amemwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa kuwa ndiye mwenye mamlaka ya kutoa kibali cha mikutano ya kisiasa, lakini mbunge haombi kibali, ila yeye labda anaomba ulinzi tu,” alisema.
Mtazamo wa wadau
Mchambuzi wa siasa, Dk Elias Mhando, amesema malalamiko ya Ado yanaibua tafakuri kuhusu mipaka ya mamlaka ya kiutendaji na uhuru wa shughuli za kibunge katika mfumo wa demokrasia.
“Sheria inapompa mbunge haki ya kuwafikia wananchi wake, mamlaka nyingine zinapaswa kuhakikisha haki hiyo inalindwa badala ya kuweka vikwazo visivyoeleweka,” amesema.
Kwa mtazamo wake, tofauti ya tafsiri kati ya zuio la mikutano ya kisiasa na shughuli za kibunge inahitaji ufafanuzi wa wazi kutoka mamlaka husika.
“Bunge na Serikali zinapaswa kujenga utaratibu wa mawasiliano ili migogoro kama hii isigeuke kuwa mvutano wa kikatiba,” amesema.
Mchambuzi mwingine wa siasa, Profesa Daniel Kweka, amesema suala hilo linaonesha umuhimu wa kutenganisha shughuli za kisiasa za vyama na majukumu rasmi ya wawakilishi wa wananchi.
“Mbunge anapowasilisha mrejesho wa Bunge, anatekeleza wajibu wa uwakilishi unaotambuliwa na sheria, siyo shughuli ya kisiasa ile,” ameeleza.
Amesema hatua za kiusalama zinapaswa kuzingatia mazingira halisi ya tukio na kutofautisha mikutano ya kisiasa na ya kibunge.
“Changamoto kubwa ni pale ambapo mamlaka zinapotumia tafsiri pana ya zuio bila kuangalia wajibu wa kikatiba wa mbunge,” amesema.
Kwa upande wake, Mchambuzi na Mtafiti wa Demokrasia, Dk Victor Lema, amesema malalamiko ya mbunge huyo yanaweza kuibua mjadala kuhusu uwiano wa mamlaka za dola na taasisi za uwakilishi.
“Katika demokrasia iliyoimarika, migogoro ya aina hii inapaswa kutatuliwa kupitia sheria na mazungumzo, siyo kupitia kuzuiwa kwa shughuli,” amesema.