Balozi Karume aikoroga CCM

Unguja. Vuguvugu la mpasuko ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar, linafukuta kutokana na kauli za mwanachama wake mashuhuri, Balozi Ali Abeid Karume kuwa mwiba kwa watawala na chama chake.

Mara kadhaa, mwanadiplomasia huyo ambaye ni mtoto wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Aman Karume amekuwa akitoa shutuma mbalimbali kwamba chama hicho kimekosa uhalali wa wananchi kuongoza visiwani humo.

Balozi Karume amekuwa na vipande vifupi vya video na sauti zinasosambaa mitandaoni akituhumu chama chake kuingia madarakani kwa wizi wa kura, akidai CCM haijawahi kushinda uchaguzi wa urais Zanzibar, bali wanaingia madarakani kwa wizi wa kura.

Kupitia video hizo, mwanasiasa huyo aliyegombea mara kadhaa nafasi ya kuongoza Ikulu ya Zanzibar bila mafanikio ndani ya chama, alisema makundi yaliyojitokeza ndani ya CCM yametokana na mfumo uliotumika kumpata mgombea urais visiwani humo mwaka 2020, kwa sababu ilikuwa kwa njia ya uteuzi badala ya uchaguzi katika vikao vya chama.

Gazeti hili lilipomtafuta Balozi Karume kujua kama amekwisha kuitwa au kuelezwa jambo lolote baada ya kauli hizo, alisema hakuna aliyemfuata au kuelezwa lolote na amekuwa akitumia haki yake kueleza kile anachokiona.

Licha ya viongozi wa CCM kutoeleza hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa dhidi ya mwanachama huyo aliyewahi kuwa waziri hadi mwaka 2020, gazeti hili limedokezwa mchakato umekwishaanza kumpeleka kamati ya maadili.

“Tumemsikia vizuri sana, tunamfuatilia kwa makini, kauli zake haziwezi kuachwa hivi hivi. Lazima jambo lifanyike kwa masilahi ya chama. Tutatumia utaratibu kumchukuliwa hatua za kinidhamu na si ajabu haitazidi mwezi huu,” alisema kigogo wa CCM kutoka Tanzania Bara ambaye hakutaka kuandikwa jina lake.

“Balozi Karume si mwanasiasa mdogo kwamba kauli zake tuzipuuze. Nafikiri tutampeleka kamati ya maadili ili kumwezesha kutulia. Tukimwacha atamchanganya Dk Mwinyi (Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi) ashindwe kuongoza vizuri.”

Ikiwa Balozi Karume atapelekwa katika kamati ya maadili na kukutwa na hatia, kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM, anaweza kupewa adhabu mbalimbali kama onyo, ikiwamo kuchunguzwa kwa miezi sita au miezi 12 na atakuwa katika hali ya matazamio kwa muda usiopungua miezi 18.

Katika kipindi hicho mwanachama hatakuwa na haki ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama, lakini atakuwa na haki ya kupiga kura kuwachagua viongozi wake wa chama.

Mchambuzi wa masuala ya siasa Zanzibar, Ali Makame alisema CCM ina nidhamu kutoka juu hadi chini, hivyo anapotokea mtu akafanya hivyo, tena kada mzoefu ni wazi amekiuka taratibu za chama.

Alisema wakinyamazia suala hilo kuendelea na wengine wakawa wanakosoa bila kufuata utaratibu, inaweza kuleta athari kubwa ndani ya chama hicho.

Makame alitaja moja ya athari kubwa ni chama kupoteza mvuto na uaminifu kwa wanachama wake, hivyo kusababisha makundi mengine kuibuka na kuanza kukosoa wakijua hakuna hatua zitakazochukuliwa.

Alisema kujibizana naye itamfanya aonekane ni shujaa kwa sababu yeye kama amekosea na wengine (wanachama) hawapaswi kukosea kujibizana naye, isipokuwa kuchukua hatua kama ambavyo wamekuwa wakichukuliwa makada wengine wanapokengeuka.

"Suala la msingi tunayo rekodi ya wale makada ambao wamekosoa chama kinyume na utaratibu na wakachukuliwa hatua, kumuacha hiki kitakuwa kirusi kibaya kwa CCM, maana nidhamu itaondoka na ikishaondoka CCM watapata athari," alisema Makame.

Kuhusu CCM kupata athari iwapo wakimchukulia hatua Balozi Karume, Makame alisema “sidhani kama kutakuwa na athari yoyote kwa sababu inategemea huyo mtu ni nani na kwa sasa, Balozi Karume ni kada wa kawaida."


Alichosema Rais Mwinyi

Mei 30 mwaka huu, alipoulizwa kuhusu kauli za Balozi Karume wakati akizungumza na waandishi wa habari Ikulu Zanzibar, Rais Mwinyi alisema mpuuzi hajibiwi, hivyo wanampuuza.

Alisema utaratibu wa CCM upo wazi jinsi ya kuwapata wagombea wake na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ulikuwa wa wazi, hivyo kushangazwa na kauli za mwanasiasa huyo mkongwe.

"Ulikuwa ni uchaguzi wa wazi, kura zilipigwa wazi na kuhesabiwa hadharani kwa uwazi, sasa anapotokea mtu anasema mambo ya ovyo huna sababu ya kumjibu, unampuuza maana mpuuzi hajibiwi, anapuuzwa," alisema Dk Mwinyi.

Jana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Zanzibar, Dk Muhammed Dimwa alirejea kauli hiyo akisema hawatamjibu kada huyo kama alivyosema Dk Mwinyi.

"Tunaweza tukamuacha tu ili aendelee na upuuzi wake; na mimi kwenye mikutano yangu nimekuwa nikizungumza kwamba hatutamjibu mtu, tunajibu hoja kwa hoja kwa masilahi ya kujenga amani na maridhiano," alisema Dk Dimwa.

Kuhusu mwanachama huyo kuitwa kwenye kamati za maadili, Dk Dimwa alisema kwa sasa bado hawajafikia uamuzi huo kwa sababu uamuzi wa CCM unafanywa na vikao na yeye (Dk Dimwa) yupo safarini, akirejea watapanga siku kuitisha kamati maalumu.

Alisema akirejea watakaa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho - Zanzibar, Rais Mwinyi ili waitishe kamati maalumu itakayoamua nini cha kufanya.

"CCM ni taasisi, jambo haliamuliwi na mtu mmoja, kwa hiyo kamati ndiyo itakayoamua. Tunaamua kutokana na vikao na katiba yetu, vikao vikiamua na kutuelekeza tutafanya hivyo, lakini kwa sasa bado hatujaamua kufanya chochote," alisema Dk Dimwa

Juzi jioni, Katibu Kamati Maalumu NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Khamis Mbeto alisema chama kimesikia kauli hizo, hivyo suala lake litashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za chama.

“CCM ina taratibu zake, zipo kamati za maadili wenyewe ndio wanashughulikia masula hayo, kama wataona ipo haja kumuita watamuita kuzungumza naye kisha baada ya hapo tutatoa taarifa kitakachofuata,” alisema Mbeto.

Alimtaka Balozi Karume kutumia taratibu za chama kwa ajili ya kuwasilisha jambo lolote kama mwanachama mzoefu na mwenye heshima.

“Yeye amekuwa waziri Serikali ya awamu ya saba, kama ipo hivyo anavyosema, mbona hakujiondoa au kukataa akisema haridhishwi na upatikanaji wake? Ifike mahala asijivunjie heshima zake mana ni mtu anayeheshimika kwa nafasi zake alizopitia,” alisema.

Hivi karibuni Balozi Karume, aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano, Uchukuzi na Usafirishaji katika Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) alinukuliwa kauli hizo zilizosambaa mitandaoni wakati akijibu swali katika mahojiano yaliyofanyika kwa njia ya mtandao visiwani hapa.

Katika maoni yake, Balozi Karume alitakiwa kufafanua sababu za kuwapo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (Suki) visiwani humo uliotokana na makubaliano ya mgawanyo wa madaraka baada ya uchaguzi.