CCM Zanzibar yatoa kauli kuhusu Balozi Karume

Mwanasiasa na mwanadiplomasia, Balozi Ali Karume.

Muktasari:

  • Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinafuatilia kauli za Balozi Ali Abeid Karume anazozitoa kuhusu viongozi wa chama hicho kukosa uhalali wa wananchi kuongoza Zanzibar.

Dar es Salaam. Vuguvugu la mpasuko limeendelea kufukuta visiwani Zanzibar baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuahidi kufanya uchambuzi wa kauli mwanasiasa na mwanadiplomasia, Balozi Ali Abeid Karume kuhusu viongozi wa chama hicho kukosa uhalali wa wananchi kuongoza Zanzibar.

 Ali Karume aliyegombea mara kadhaa nafasi ya kuongoza Ikulu ya Zanzibar bila mafanikio ndani ya chama, ametumikia nafasi mbalimbali ndani ya chama na serikalini tangu akiwa na miaka 28 hadi Serikali iliyomaliza muda wake mwaka 2020 akiwa kwenye baraza la mawaziri. 

Leo Jumatano, Mei 31, 2023, Katibu Kamati Maalumu NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Khamis Mbeto akizungumza na Mwananchi Digital amesema chama kimesikia kauli hizo hivyo suala lake litashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za chama.

“CCM ina taratibu zake, zipo kamati za maadili wenyewe ndio wanashughulikia masula hayo kama wataona ipo haja kumuita watamuita kuzungumza naye kisha baada ya hapo tutatoa taarifa kitakachofuata,” amesema Mbeto.

Mbeto amemtaka Balozi Ali ambaye ni mtoto wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Karume kutumia taratibu za chama kwa ajili ya kuwasilisha jambo lolote kama mwanachama mzoefu na mwenye heshima.

“Yeye amekuwa waziri katika serikali ya awamu ya saba, kama ipo hivyo anavyosema mbona hakujiondoa au kukataa akisema haridhishwi na upatikanaji wake? Ifike mahala asijivunjie heshima zake mana ni mtu anayeheshimika kwa nafasi zake alizopitia,” amesema Mbeto.

Siku mbili zilizopita, Balozi Karume aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano, Uchukuzi na Usafirishaji katika awamu ya saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) alinukuliwa kauli hizo zilizosambaa mitandaoni wakati akijibu swali katika mahojiano yaliyofanyika kwa njia ya mtandao huko Zanzibar.

Katika maoni yake Balozi Karume alitakiwa kufafanua sababu za kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUKI) visiwani huko uliotokana na makubaliano ya mgawanyo wa madaraka baada ya uchaguzi.

“GNU ipo kwa sababu viongozi wa CCM walikuja kuona kwamba kila chaguzi za Zanzibar CCM inashindwa uchaguzi, sasa inashindwa kwa sababu gani, hilo tutazungumza siku nyingine. Lakini naamini walikuwa wanashindwa kwa kuweka wagombea wasio na mvuto,” alisema Balozi Karume akifafanua:

“Wakienda kwenye uchaguzi wa kweli na haki wanashindwa kura hawa wadogo zangu na matokeo tumeyaona mfano mwaka 2015 hebu tuambizane ukweli kama kweli tulikubaliana uchaguzi uwe haki ilikuwaje tutumie mabavu, nguvu?“

Kutokana na kauli hiyo, juzi rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Hussein Mwinyi, alijibu hoja hiyo kwakupuuza: “Kama nilivyosema, upuuzi haujibiwi, unapuuzwa. Hili siwezi kulijibu,”alisema Dk Mwinyi alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo.  “Nani asiyejua mfumo wa uchaguzi wa nchi yetu?.

“Maana watu wengine wanahoji kuanzia huko kwenye kura za maoni, ahaa kapewa tu na mwenyekiti. Jamani, kuna mwaka uliowahi kuwa wazi katika uchaguzi kama ilivyokuwa mwaka 2020? Kura zimepigwa hadharani, zimehesabiwa hadharani imewahi kutokea? Katika hili naomba nimpuuze tu.”