Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Balozi Karume aliamsha tena

Mwanasiasa na mwanadiplomasia, Balozi Ali Karume.

Unguja. Siku 21 tangu Chama cha Mapinduzi (CCM) kimuandikie barua ya onyo na kumweka chini ya uangalizi kada wake, Balozi Ali Abeid Karume kutokana na kauli zake akidaiwa kukidhalilisha chama na viongozi wake, ameibuka na mengine.

Mwanadiplomasia huyo aliingia kwenye mzozo na chama chake baada ya kutoa kauli ya kukituhumu chama na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho upande wa Zanzibar, Rais Hussein Mwinyi.

Kabla ya kuitwa na kuhojiwa na kamati za maadili za tawi la Mwera, jimbo la Tunguu na Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja kwa nyakati tofauti na kisha kupewa barua ya onyo Juni 15, mwaka huu, Rais Mwinyi alionekana kushangazwa na chama chake kushindwa kuwachukulia hatua makada wanaojitokeza hadharani na kukitukana chama.

Rais Mwinyi alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti katika Mkoa wa Kusini na Kaskazini, alipozungumza na viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya mashina hadi wilaya, akisema anashangazwa kuona watu hao wanaachwa bila kuitwa kwenye kamati za maadili za chama.

Miongoni mwa kauli za Balozi Karume zilizosababisha kuitwa na kuonywa ni ya tuhuma dhidi ya chama hicho kuwa hakijawahi kushinda kihalali kisiwani humo na kumkosoa hadharani Rais Mwinyi kuhusu sera za kukodisha visiwa, akipinga utaratibu huo.

Pia alipinga utaratibu wa wananchi wa Kilimani kuondolewa, ili kujenga ukumbi wa kimataifa na ujenzi wa uwanja wa Amani akidai vinakiuka utaratibu.

Baada ya kupewa onyo na chama chake, Balozi Karume alipotafutwa na gazeti hili alisema hajapokea barua yoyote, iwapo atapokea atakuwa mtiifu na kuzingatia maadili ya chama.

Hata hivyo, hivi karibuni zimeonekana baadhi ya vipande vifupi vya video za mwanadiplomasia huyo akirejea kauli yake akisisitiza kwamba, licha ya kueleweka vibaya kwa chama chake, lakini hakuna demokrasia ya kweli ndani ya chama hicho.

“Kinadharia (CCM) wanadai kuna demokrasia, lakini kiuhalisia imevamiwa na watu ambao si tu wanavunja katiba, wanaichezea katiba ya chama na wanapata madaraka na wanakwenda wanasema hawafuati katiba ya chama wanafuata katiba nyingine,” alisema.

Alisema: “Katika CCM Taifa watu watano wakishakubaliana kwamba mtu mmoja anatosha, hawa wengine wanasindikiza, kwa hiyo mimi nafikiri ni udanganyifu, bora wakawaambia watu kwamba bwana sisi tumeshakaa tumepata mtu basi, hata zamani tulifanya hiyo, Mwalimu Nyerere alikuwa hivyo.”

Alisema inawezekana ikafanywa hivyo, lakini ni vema wakapewa watu fursa ili kukwepa kwenda kinyume na katiba ya chama hicho.

“Ukijitokeza kuwania nafasi utasikia huyu sifa yake kubwa baba yake alikuwa Rais, huyu baba yake alikuwa Rais hakufanya vizuri, je, hiyo ndiyo sifa pekee? Na mmefanya uchunguzi kuona sifa zake nyingine?” alihoji.

Akizungumzia udanganyifu aliodai unafanywa na chama chake, alisema CCM kiliomba ridhaa kwa wananchi, hivyo, “Mwenye kutawala lazima apate ridhaa ya kutawaliwa, lakini matatizo hayo yalianza enzi hata kabla ya mapinduzi na ndiyo yanayoendelea hadi sasa.

“Kama yangefanyika hayo mapinduzi yasingelitokea Zanzibar, lakini na wao waliona potelea mbali mpaka leo, kama mmesikia sauti zangu hivi karibuni ingawaje wenzangu hawakunielewa, lakini mimi nasema chama kiongozwe kwa uadilifu,” alisema.

Balozi Ali alisema katiba ya CCM inakitambua ni chama cha kitaifa, uongozi wake unatakiwa uwe wa kitaifa, hivyo hakuna CCM Zanzibar kama ambavyo kuna viongozi wanakigawa chama hicho.

“Nashangazwa sana kwamba kuna mtu kiongozi wa CCM Taifa, lakini ana nafasi ya makamu mwenyekiti wa CCM Zanzibar anamtuhumu mwanachama mwenzake ndani ya chama kwamba kakosea, sasa sijui yeye katoa wapi mamlaka hayo, yeye hapaswi atamke wazi kwamba mtu anayefanya makosa afukuzwe chama, bali kuna taratibu maalumu za vikao,” alisema. Licha ya kupongeza Serikali ya Muungano wa Tanzania kwamba inakwenda vizuri, alisema hofu yake ni wale wanaotaka kuwe na CCM Zanzibar.

“Iwapo hawa wakipata nguvu wanataka mambo ya kichama mengine yafanywe Zanzibar pekee, basi usimamizi wa Serikali ya Muungano utakuwa mzuri, lakini usimamizi Serikali ya Zanzibar utaanza kulegalega kwa sababu kuna watu hapa shughuli zote za Serikali si miradi ya Serikali ni miradi ya watu binafsi,” alisema.

Aliongeza kuwa, “Sasa narejea tena kwamba haiwezekani mtu upate uongozi kupitia chama chako, kisha unakoroga mambo kuwapa faida wapinzani wanapanda kwenye jukwaa wanakubaliwa na wananchi.”

Alisema masuala kama hayo yanatakiwa yashughulikiwe na Baraza la Wawakilishi na Rais aendeshe Serikali, akidai hakuna Rais duniani anakabidhiwa hatimiliki ya nchi na Serikali, halafu anatoka anavunja amri anavyotaka.

Mwanadiplomasia huyo alisema ipo haja kwa viongozi wakuu wakumbushwe kuwa walishikwa mkono na chama, hawapaswi kukidharau kwa sababu wamepata nafasi hizo kupitia mgongo wa chama.


Kauli ya CCM

Alipotafutwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto alijibu kupitia mtandao wa Whatsapp kwamba hajaona kipande hicho cha video, hivyo atakuwa kwenye nafasi nzuri kuzungumza baada ya kuiona.

“Nipo Hija Makka, narudi tarehe 8, Jumamosi, nitumie hiyo taarifa mpya ya Ali Karume. Nitakutumia ‘voice note’ nikitokea huku Saudi Arabia, lakini niione kwanza hiyo taarifa,” alisema Mbeto.