Baraza la Wazee CCM launga mkono kazi za JPM
Muktasari:
- Wazee hao wanaunga mkono juhudi za Rais Magufuli katika kupambana na wahujumu uchumi na kuwashangaa watu wenye macho lakini wanajifanya hawaoni na wanataka kumkwamisha Rais.
Sumbawanga. Baraza la Wazee wa CCM Mkoa wa Katavi limetoa tamko la kumuunga mkono Rais John Magufuli katika jitihada zake za kupambana na watu wanaohujumu rasilimali za nchi na kulaani vikali mauwaji yanayotokea Kibiti na Mkuranga mkoani Pwani.
Tamko hilo limetolewa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga katika kikao cha Baraza la Wazee wa CCM Mkoa wa Katavi kilichofanyika katika Ukumbi wa Maji mjini humo.
Akisoma tamko hilo leo, Jumapili, Julai 9, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CCM Katavi, Thomas Ngozi amesema baraza hilo linamuunga mkono Rais Magufuli katika jitihada kubwa anazofanya kupambana na wahujumu wa rasilimali za nchi.
Amesema wamekaa na kuona nchi inavyokwenda hivyo wameona wamtie moyo Rais kutokana na kazi ngumu anayoifanya ya kuiongoza nchi.
Mwenyekiti huyo alieleza kuwa wanatambua upendo alionao Rais Magufuli kwa Watanzania na hasa kwa kuwajali wale walio masikini bila kuwabagua kutokana na umasikini wa watu hao.
Amesema wapo baadhi ya Watanzania wachache wenye macho lakini wamekuwa wakijifanya hawaoni na wamekuwa wakitaka kukwamisha jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano.
Alieleza kuwa kama ni wizi ulivuka mipaka na Serikali imekuwa ikiibiwa kwa kipindi kirefu hivyo Rais ameamua kupambana na wizi huo hivyo ni vyema jitihada hizo anazozifanya zikaungwa mkono na watu wote bila kujali itikadi za vyama.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Mstaafu Muhuga alisema Serikali ya mkoa huo inaunga mkono jitihada kubwa katika vita ya wahujumu wa uchumi wa nchi.
Amesema vita hii inahitaji Rais aungwe mkono kwani si watu wote ambao wanaifurahia licha ya kwamba kwa kipindi hiki kifupi mabadiliko yameanza kuonekana .