CCM wawaite ACT-Wazalendo mezani

Muktasari:

Katibu Mwenezi wa CCM (Zanzibar), Khamis Mbeto amewataka viongozi, wanachama na wafuasi wa ACT-Wazalendo waache kulalamika pembeni kuhusu changamoto zinazojitokeza katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) bali wakae kwenye mazungumzo na wenzao wa CCM.


Unguja. Katibu Mwenezi wa CCM (Zanzibar), Khamis Mbeto amewataka viongozi, wanachama na wafuasi wa ACT-Wazalendo waache kulalamika pembeni kuhusu changamoto zinazojitokeza katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) bali wakae kwenye mazungumzo na wenzao wa CCM.

Mbeto ametoa kauli hiyo leo, Jumamosi, Februari 25, mjini Unguja aliposhiriki hafla ya uzinduzi wa ‘Ahadi ya ACT-Wazalendo Zanzibar’ ambapo amesema ACT-Wazalendo na CCM wanaunda Serikali hivyo yanapotokea matatizo ni vema zikatumika njia za mazungumzo badala ya kutoa matamko yanayowagawa Wazanzibar.

“Hali ya kisiasa ni nzuri, suala la SUK lipo kikatiba hivyo kama kuna shida pande hizi mbili zikae kwenye vyama vyao na baadaye itafutwe suluhu badala ya kila kukicha kuendelea na malalamiko ya pembeni” amesema

Naye Naibu Katibu wa Habari na Uenezi wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Salim Abdalah Bimani, amesema kila wanachokifanya kinazingatia masilahi ya Wazanzibari

Amesema kila mara zinapoibuka changamoto wao hufanya vikao na wakati mwingine huifikisha kwa wanachama wao ili waiamue kwa masilahi ya nchi yao.

“Tunahitaji dhamira njema ya kushirikiana, hii nchi yetu sote, ukiona mtu analalamika ujue mambo hayaendi sawa na inapaswa irekebishwe ili tuendelee na umoja wetu” alisema

Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), ilianzishwa mwaka 2010 baada ya Katiba ya Zanzibar kufanyiwa marekebisho baada ya maridhiano yaliyohusisha wadau mbalimbali.

Katiba hiyo inatoa fursa chama kilichoshika nafasi ya pili na kukidhi sifa za kupata wingi wa kura katika Uchaguzi Mkuu kushirikiana na chama kilichoshinda kuunda Serikali.

Chama hicho cha upinzani pia kitatoa Makamu wa kwanza wa Rais na mawaziri ambapo hivi sasa ACT-Wazalendo kimemtoa Makamu wa kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman na wamaziri wawili ambao ni Nasoro Ahmed Mazrui (Wizara ya Afya) na Omar Said Shaaban (Viwanda).