CCM yataja mikakati minane kuleta maendeleo

Mkutano wa CCM siku ya pili waanza Dodoma

Muktasari:

Naibu Katibu Mkuu Bara (CCM) Christina Mndeme ametaja miongoni mwa malengo waliyojiwekea katika kipindi hicho ni kusimamia utekelezaji wa kazi na maadili ya viongozi wa chama kwa kuzingatia Katiba na kanuni.

Dodoma. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza malengo na mikakati minane ya maendeleo ya chama na jumuiya zake katika kipindi cha miaka mitano ijayo 2022 hadi 2027.

Mikakati hiyo imeelezwa leo Desemba 8, 2022 na Naibu Katibu Mkuu Bara (CCM) Christina Mndeme wakati akitoa taarifa ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ya kazi kwenye siku ya pili ya mkutano mkuu wa chama hicho jijini Dodoma.

Mndeme amesema miongoni mwa malengo waliyojiwekea katika kipindi hicho ni kusimamia utekelezaji wa kazi na maadili ya viongozi wa chama kwa kuzingatia katiba na kanuni.

Pia kufanya tathimini ya mfumo wa kura za maoni, mchakato wa uteuzi wa upatikanaji wa nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani ili kujua changamoto na kuzipatia ufumbuzi.

Malengo mengine ni kuendeleza mageuzi ya kiuchumi kwa kusimamia utekelezaji wa sera ya miradi na uwekezaji ya mwaka 2021 ambapo utekelezaji wa sera hiyo utakuwa vipimo vya uwezo wa watendaji na viongozi katika nafasi wanazopewa.

Ametaja pia mkakati wa kubuni na kuandaa utekelezaji wa awamu ya nne ya mradi wa kuimarisha chama ili kuendeleza nguvu, uhai na maendeleo ya jumuiya zake pamoja na kuendeleza jitihada za kusimamia kampuni za CCM ili kuhakikisha zinapatiwa uwezo na kutekeleza sera za chama ikiwemo kutoa gawio la kila mwaka.

“Jambo la sita ni kusimamia Serikali mbili za Tanzania na Zanzibar katika kutekeleza Sera za CCM na ilani ya uchaguzi wa CCM ili kuimarisha mahusiano mema kati ya CCM na vyama rafiki vya kindugu na wanamapinduzi wengine duniani,” amesema Mndeme.

Aidha Mndeme amesema CCM imejipanga kusimamia utekelezaji wa kazi za chama na majukumu ya kila idara kama yalivyoainishwa katika Katiba na ilani ya uchaguzi kwa weledi pamoja na ufanisi.