CCM yateua mgombea ubunge Aman

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan ameongoza kikao cha kamati kuu ya chama hicho, jijini Dodoma pamoja na mambo mengine, kimemteua Abdul Yusuf Maalim kuwa mgombea wa Ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Aman, Zanzibar.

Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimemteua Abdul Yusuf Maalim kuwa mgombea wa Ubunge katika uchaguzi mdogo Jimbo la Amani Mjini Zanzibar unaotarajiwa kufanyika Disemba 17, 2022.

 Uchaguzi huo wa marudio utafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Mussa Hassan Mussa kilichotokea Oktoba 10, 2022.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Novemba 22, 2022 na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka imesema uteuzi huo umefanyika baada ya Kamati Kuu ya CCM, kukutana Dodoma katika kikao chake maalumu chini ya Mwenyekiti wake Rais Samia Suluhu Hassan.

"Pamoja na mambo mengine Kamati Kuu imefanya uteuzi wa wagombea wa nafasi ya ubunge Kwa tiketi ya CCM katika Jimbo la Amani Mjini Zanzibar ambapo imemteua Abdul Yusuf Maalim Kuwa mgombea wa Ubunge katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Disemba 17 Mwaka huu," Imeeleza taarifa hiyo

Aidha Kamati Kuu hiyo imepokea taarifa ya maendeleo ya uchaguzi wa Chama hicho na jumuiya zake unaendelea katika ngazi ya mikoa nchini na imeendelea kuwakumbusha wanachama, wagombea wote juu ya umuhimu wa kuheshimu miiko ya uongozi Kwa mujibu wa Katiba na kanuni za Chama hicho.