Chadema ni mwendo wa operesheni

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Dar es Salaam. Hatua ya Chadema kuzindua Kata Funua 2017 imekifanya chama hicho kufikisha operesheni sita tofauti tangu mwaka 2004.

Chadema imetangaza mapema wiki hii kuwa Operesheni Kata Funua itafanyika kuanzia mwakani ikiwa ni mwendelezo wa chama hicho kujisogeza karibu na wananchi baada ya kufanya “Operesheni Chadema ni Tawi”, “Sangara”, “Chadema ni Msingi”, “Vuguvugu la Mabadiliko (M4C)” na “Operesheni Mshike Mshike”.

Mwenyekiti wa chama hicho cha upinzani, Freeman Mbowe alisema wakati wa kutangaza “Operesheni Kata Funua” kuwa itafanyika ndani ya kanda za Chadema na itahusisha kuendesha vikao vya ndani vya ngazi ya majimbo ya uchaguzi ya kanda zote kukagua uhai wa chama.

Hiyo itakuwa operesheni ya sita rasmi tangu Mbowe achukue uenyekiti wa chama hicho mwaka 2004.

“Mafanikio ya chama si tu kuingia madarakani, bali hata kuongeza idadi ya viongozi wa kuchaguliwa,” alisema Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini (Bukoba), Dk Azaveli Lwaitama alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu operesheni za Chadema.

“Kukiondoa chama tawala madarakani si kazi ndogo, unahitaji operesheni hata 100 si sita tu,” alisema Dk Lwaitama.

“Tangu operesheni hizo zianze, (Chadema) wameongeza wabunge na madiwani. Hata miji na halmashauri walizokuwa wakishikilia zimeongezeka.

“Unapozungumzia chama tawala, hata Katiba inakipendelea kucheza rafu. Huwezi kujua kama umeshinda au umeshindwa. Tume ya Uchaguzi inajazwa wateule wa Rais, haina wafanyakazi kwenye ngazi za chini. Tumeona mwaka huu Rais ameteua hata wale walioshindwa uchaguzi na watakuwa wasimamizi wa uchaguzi.”

Dk Lwaitama alisema uzoefu unaonyesha wapinzani wengi walichukua muda mrefu kushika madaraka.

“Kule Senegal, Abdoulay Wade alichukua miaka mingi kuingia madarakani. Hata harakati za uhuru hazikuchukua muda mfupi. Chama cha TAAA kilianzishwa mwaka 1920, kikaja kubadilika kuwa Tanu mwaka 1954, ni muda mrefu mno,” alisema.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Mohamed Bakari alisema kila chama cha siasa kina wajibu wa kuhamasisha wananchi, japo mafanikio ya operesheni yanategemea mambo tofauti.

“Huwezi kusema moja kwa moja kama operesheni hizo zimefanikiwa. Kuna kipindi operesheni zilifanikiwa, wananchi wakawa wanazomea viongozi wa Serikali na kuna wakati hazikufanikiwa, japo ujumbe ulifika,” alisema.

“Vyama vya siasa vina wajibu wa kuwahamasisha wananchi, lakini mafanikio sasa yanategemea, yanaweza kuwa mazuri au yasiwe mazuri,” alisema Dk Bakari.

 

Mrema achambua operesheni

Akizungumzia operesheni hizo katika tathmini yake ya mwaka mmoja wa Chadema tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu uliopita, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, John Mrema alisema operesheni hizo zimekiwezesha kujiimarisha na zinakiandaa kushinda uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na kuchukua dola mwaka 2020.

“Tangu alipoingia madarakani mwaka 2004, Freeman Mbowe amekuwa akiendesha chama kwa njia tofauti na za kuhamasisha Watanzania kujiunga na Chadema,” alisema Mrema.

“Mbowe alipoingia madarakani alipokea chama chenye wabunge sita nchi nzima ambao walipatikana mwaka 2000 baada ya uchaguzi mkuu. Watano wa majimbo na mmoja viti maalumu,” alisema Mrema.

Wabunge hao ni Mbowe, wa Jimbo la Hai, Dk Willbroad Slaa (Karatu), Philemon Ndesamburo (Moshi Mjini), Dk Aman Kaborou (Kigoma Mjini) na Grace Kiwelu (viti maalumu). Mbali na wabunge hao, Chadema ilikuwa na madiwani 72.

Mrema alisema kati ya mwaka 2004 na 2005, Mbowe aliendesha operesheni ya kimyakimya ambayo ilikuwa na lengo la kutafuta vijana wenye vipaji wa vyuo vikuu kuwashawishi kujiunga na Chadema.

“Operesheni hii haikuwa na jina kwa sababu ilikuwa ya kutafuta vipaji kimyakimya na katika kipindi hiki ndipo vijana kama kina Zitto Kabwe, Albert Msando, Halima Mdee, John Mnyika, mimi, Mhonga Said na wengineo waliokuwa viongozi wa wanafunzi (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) UDSM walipatikana na kujiunga na chama,” alisema.

Mbali na wanafunzi, Mrema alisema Mbowe aliendesha operesheni nyingine ambayo haikuwa na jina ambayo ililenga kuitangaza Chadema kama klabu ya michezo ya Real Madrid ya Hispania ambayo ililenga kukusanya vipaji kutoka vyama vingine vya siasa na asasi za kiraia.

Operesheni hiyo ilivuna vijana kama Antony Komu, ambaye alikuwa NCCR-Mageuzi, Shaibu Akwilombe (CUF), Msafiri Mtemelwa (NCCR-Mageuzi), Suzan Kiwanga, Godbless Lema (TLP), Peter Msigwa na wazee kama Said Arfi, Chiku Abwao na Marehemu Chacha Wangwe.

“Baada ya uchaguzi mkuu, Mbowe alianzisha operesheni za wazi zilizokiinua chama kwa kuongeza idadi ya wabunge,” alisema Mrema.

“Chama kiliongeza madiwani wake hadi kufikia 102 na kuongoza halmashauri tatu za Karatu, Tarime Mjini na Kigoma Ujiji.”

 

Operesheni Chadema ni Tawi 2006-2008

Kampeni za wazi zilianza na Operesheni Chadema ni Tawi, ambayo ililenga kujenga matawi ya chama kutimiza utashi wa katiba.

“Mafanikio ya operesheni hii ni pamoja na kukisogeza chama karibu zaidi na wananchi,” alisema Mrema.

 

Operesheni Sangara

Mkakati huo ulifuatiwa na “Operesheni Sangara” iliyofanyika mwaka 2008-2010, ambayo ililenga maeneo ya Kanda ya Ziwa na kwa mujibu wa Mrema, mafanikio ya mpango huo ni kushinda Jimbo la Tarime Mjini katika uchaguzi mdogo.

“Iliitwa Sangara kwa sababu ya aina ya samaki maarufu (sangara) ambaye anapatikana Ziwa Victoria na ana tabia ya kuwala samaki wenzake wadogo. Ikumbukwe kuwa hiki ni kipindi ambacho ufisadi mkubwa ulikuwa umepamba moto nchini kama ule wa EPA na Buzwagi,” alisema.

Alisema operesheni hiyo ilifanyika mikoa ya Mara, Mwanza, Shinyanga, Kagera, wakati huo Simiyu na Geita haikuwa na hadhi ya mkoa.

“Mafanikio ya moja kwa moja yalionekana katika kampeni za chaguzi ndogo za majimbo ya Busanda na Biharamulo Magharibi ambako ushindani ulikuwa mkubwa kwa CCM kuliko wakati mwingine wowote katika siasa za kanda hiyo,” alisema Mrema.

Alisema operesheni hiyo ndiyo iliyoibua vijana kama Vicent Nyerere, Ezekiah Wenje, marehemu Alphonce Mawazo na Mwita Waitara.

Pia Mrema alisema chama kiliongeza idadi ya wenyeviti wa vijiji, vitongoji na mitaa mwaka 2009, na katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 Chadema iliongeza idadi ya madiwani kutoka 102 hadi kufikia 584 na idadi ya halmashauri za wilaya ilizoshinda iliongezeka kutoka tatu hadi saba.

“Tumeendesha ajenda kuu za nchi kwa wakati huo kama kuendesha vita dhidi ya ufisadi (List of Shame).”

 

Chadema ni Msingi

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Chadema iliibuka na operesheni nyingine ya “Chadema ni Msingi” iliyofanyika kwa mwaka mmoja.

“Ilikuwa na lengo la kukiweka chama katika ngazi ya msingi na sio tawi tena kama ilivyokuwa hapo awali, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa kila kitongoji kinakuwa na msingi wa chama.

“Operesheni hii ilikuwa na ajenda kuu ya kudai mabadiliko ya katiba na iliendeshwa kwa njia ya maandamano makubwa ya wananchi ambayo yalizinduliwa katika Mkoa wa Mwanza na kuendelea katika mikoa ya Mara, Shinyanga, Kagera, Tabora, Arusha na kwingineko,” alisema.

“Wakati huo Rais (wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya) Kikwete alitoa kauli kuwa kuna watu wanataka kumtoa madarakani kwa njia ya maandamano, Ndipo alipotuita kufanya mazungumzo ya Katiba Mpya na huu ulikuwa mwanzo wa kuundwa Tume ya Marekebisho ya Katiba,” alisema.

“Ni katikati ya operesheni hii, uchaguzi wa Jimbo la Igunga ulifanyika na tuliweza kupata mafanikio makubwa sana katika uchaguzi huu. Programu ya Chadema ni Msingi iliendelea kama ilivyokuwa ile ya Chadema ni Tawi.”

 

Vuguvugu la Mabadiliko

Chama hicho pia kilianzisha operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko mwaka 2012 baada ya Tume ya Marekebisho ya Katiba kuundwa.

Ilianzia Arusha na hasa katikati ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki ambako baadaye CCM ilishindwa.

Operesheni hiyo ilisimama kwa muda kutokana na kifo cha mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi, ambaye aliuawa kwa bomu la machozi wakati akifuatilia mzozo baina ya Jeshi la Polisi na wafuasi wa Chadema.

Katikati ya operesheni hiyo ndipo Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulizaliwa, ukipinga uendeshaji wa Bunge la Katiba kwa madai kuwa chombo hicho cha kihistoria kiliacha maoni ya wananchi na kuingiza sera za CCM.

“Tumeshinda kata mbalimbali zilizokuwa na chaguzi ndogo katika kipindi hicho, uchaguzi wa vijiji, vitongoji na mitaa kwa asilimia 33 mwaka 2014,” alisema Mrema.

 

Operesheni Mshike Mshike

Operesheni ya sita ni “Mshike Mshike” iliyoendeshwa jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 2014-2015, ambayo imewezesha wapinzani kutwaa umeya wa Dar es Salaam.