Chadema wanunue gari, nguo za Lissu alipopigwa risasi

Mwonekano wa gari la Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana mkoani Dodoma Septemba 7, 2017. Picha na maktaba

Unaitazama Tanzania na nidhamu yake ya kutunza historia, unazionea wivu nchi nyingine. Unafuatilia historia ya ukombozi Afrika, unauona mchango mkubwa wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Tanzania.

Yapo wapi maandishi ya wino wa dhahabu kuonyesha ukuu wa Tanzania na Mwalimu Nyerere katika kulikomboa bara la Afrika?

Angalau Rais wa Pili wa Zimbabwe, Robert Mugabe aliandika kitabu, akakiita “Asante sana, Mwalimu”.

Mugabe aliandika kutambua mchango wa Mwalimu Nyerere kwenye uhuru wa Zimbabwe na Afrika kwa jumla. Mugabe ametaka heshima ya Mwalimu itukuzwe kwa sababu mchango wake unapita Mwafrika yeyote katika ukombozi wa bara.

Tanzania ilikuwa taifa la kila Mwafrika mpigania ukombozi. Maficho salama ya wote waliokuwa hatarini kwenye nchi zao kwa sababu ya kupigania uhuru.

Kuanzia Eduardo Mondlane aliyeasisi Frelimo mwaka 1962, Dar es Salaam, kisha ikaikomboa Msumbiji, mpaka Nelson Mandela alipoizunguka dunia kwa pasipoti ya Tanzania.

Tanzania kupitia Mwalimu Nyerere ni mkombozi wa kila nchi Afrika. Kuanzia majirani Kenya na Uganda hadi kusini Namibia na Afrika Kusini. Ni wapi historia hiyo inaandikwa kwa wino wa dhahabu ili wajukuu na wajukuu wa Tanganyika na Zanzibar wajivunie kazi kubwa ya babu na bibi zao?

Hii si utunzaji wa nyaraka na picha za ushiriki wa kulikomboa bara la Afrika, tatizo linaanzia hata kwenye historia ya uhuru wa nchi. Angalau Mwalimu Nyerere aliandika, ameandikwa na anaendelea kuandikwa. Mashujaa wengine hawaonekani kwenye sura ya ukombozi wa nchi.

Ukiingia Makumbusho ya Chama cha ANC, Afrika Kusini, utapata wivu jinsi wanawake waliochangia japo kidogo harakati za uhuru wa mtu mweusi wanavyoenziwa. Utauelewa mchango wa Rebecca Kotane, na jinsi mboni zake zilipomtazama mume wake, Moses Kotane, kwa mara ya mwisho mwaka 1963.

Kotena aliondoka Afrika Kusini kuja Tanzania kwa ajili ya kukoleza mapambano dhidi ubaguzi wa rangi.

Alitembea nchi mbalimbali kwa kutumia pasipoti ya Tanzania. Alifia Soviet mwaka 1978, alipopelekwa kutibiwa kiharusi.

Sio Rebecca tu, ndani ya Makumbusho ya ANC, utaona mchango wa Albertina Sisulu (alikuwa mke wa Komredi Walter Sisulu), Helen Joseph, Lillian Ngoyi, Amina Cachalia, Winnie Mandela na wanawake wengine waliovuja jasho, walionyanyasika na hata kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya kupigania ukombozi wa mtu mweusi Afrika Kusini.

Unaporejea Tanzania, unapata simulizi kuwa mwanamke muuza vitumbua maarufu, Mtumwa Kitete, aliyekuwa anafanyia biashara yake mtaa wa New Street (siku hizi Lumumba), Dar es Salaam, alitoa mchango mkubwa kumwezesha Mwalimu Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa kutoa hotuba ya kudai uhuru. Mtumwa hayupo kwenye nyaraka zozote. Hata picha hazipo.

Hakuna nyaraka za kuwatambua wanawake waliomsindikiza Mwalimu Nyerere Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam (sasa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere), alipokuwa anakwenda Umoja wa Mataifa. Wanawake hao waliongozwa na Titi Mohammed, Chiku Kisusa na Tatu Mzee.

Yule msichana aliyefahamika kwa jina la Jamila, aliyemvalisha Mwalimu Nyerere skafu, aliporejea kutoka Umoja wa Mataifa mwaka 1955, historia yake imeandikwa wapi. Jamila ni mjukuu wa Chiku Kisusa.


Tufanye ushereheshaji

Huo ni muhtasari wa jinsi ambavyo taifa lina tatizo la kihistoria la kutothamini historia yake. Kile ambacho nchi inacho na haikipi heshima yake stahiki, mataifa mengine wangetamba na kujipongeza kupita mfano.

Udhaifu huo unaenda ndani kabisa kwenye familia. Viongozi wakubwa wa nchi hii, wanaharakati na mashujaa, wanapoteza maisha, watoto na wajukuu zao hawana historia ya kutosha kusimulia.

Malalamiko ni mengi kuhusu mashujaa na wafadhili wa harakati za uhuru, Dosa Aziz, Abdulwahid Sykes, Ally Sykes na wengine, kwamba uhusika wao katika safari ya kuikomboa Tanganyika toka kwenye makucha ya Uingereza, haijaandikwa sawia kwenye vitabu vya kihistoria.

Tukubali hilo, kisha uliza; familia zao mbona kimya? Hata kuandika vitabu kutibu ombwe?

Gari alilopata nalo ajali Waziri Mkuu wa Pili wa Tanzania, Edward Sokoine, lipo wapi? Lililomgonga?

Matokeo yake mwanafunzi aliyezaliwa miaka ya 1990 kupanda juu, anafundishwa kuhusu ajali tata iliyochukua maisha ya waziri mkuu wa nchi yao kwa nadharia.

Anapelekwa sehemu ajali ilitokea, anaoneshwa mnara wa Sokoine. Sura nzima ya ajali haipo, kumbukumbu zote zilishafutika. Unajiuliza ilikuwa inagharimu nini gari la ajali kuwekwa makumbusho kama lilivyo?

Lile gari lililomgonga na mengine katikati msafara wa waziri mkuu?

Mataifa mengine wanatunza mpaka kumbukumbu za wahalifu wakubwa. Nyakati za Adui wa Umma mwaka 1930 mpaka 1935, Marekani iliteswa na mfululizo wa matukio ya uhalifu. Mengi yalifanywa na vijana wadogo kabisa.

Ukifika Gibsland, Louisiana, Marekani kuna jumba la makumbusho linaitwa Bonnie and Clyde Ambush Museum. Ndani yake kuna historia pana ya vijana wapenzi wahalifu, Bonnie Parker na Clyde Barrow.

Kila kitu kuhusu siku ya mwisho ya uhai, walipouawa katika mashambulizi na risasi, kipo.

Mapambano ya polisi dhidi ya Bonnie na Clyde yaliyotokea Mei 23, 1934. Kumbukumbu zote zipo, hata gari walilokuwa wanalitumia Bonnie na Clyde siku ya mwisho lipo na matundu yake ya kuchakazwa na risasi.

Bonnie and Clyde walitikisa jimbo la Texas, hususan jiji la Dallas kwa matukio ya uhalifu. Walikuwa vijana wadogo sana, ila wapenzi. Uhusiano wao wa kimapenzi na ushirikiano wao katika uhalifu, imekuwa simulizi yenye kuvutia watu wengi. Watu wanatunza.


Ushauri kwa Chadema

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu, alipigwa risasi zaidi ya 30. Kati ya hizo, 16 zilizama mwilini. Ni tukio Septemba 7, 2017.

Tukio la Lissu kupigwa risasi ni moja kati ya matukio machache yenye kushangaza mno. Risasi nyingi lakini mhusika amepona, japo si mzima kama alivyokuwa kabla ya mashambulizi.

Tukio la Lissu ni kielelezo cha mapambano ya kisiasa nyakati za giza. Chuki za kisiasa zilifika mahali utu wa Mtanzania ulipotea.

Hali ya kutoaminiana ilipotea, kiasi Lissu aliposhambuliwa, moja kwa moja serikali ilituhumiwa.

Hivi karibuni Lissu alikwenda Makao makuu ya polisi, Dodoma, akataka kuona gari lake, aone kama anaweza kulitumia au alipeleke makumbusho. Wazo la kwanza la kulitumia siyo zuri, la pili ni sawa

Hata hivyo, katika wazo la pili, nina ushauri wa kuwapa Chadema. Ni kuhakikisha kama chama, wanakuwa kitovu cha historia ya mashambulizi aliyofanyiwa Lissu.

Kwanza, Lissu alifanyiwa mashambulizi akiwa Mwanasheria Mkuu wa Chadema, vilevile mbunge wa chama hicho na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alifanya kila jitihada ndani ya uwezo wake kuhakikisha Lissu anavuta oksijeni leo. Mengine ni majaala ya Mungu.

Hivyo, Chadema, kama chama hawatakiwi kuruhusu kutengwa na tukio la Lissu. Na kwa kuanza wanapaswa kumshawishi Lissu awauzie gari alilokuwa amepanda kipindi anashambuliwa.

Niliona hivi karibuni, Lissu alipofanya ziara nyumbani kwao, Ikungi, Singida, akakabidhi nguo alizokuwa amevaa siku ya shambulio kwa wazee. Swali, wazee wanapewa nguo ili iweje? Wafanye tambiko?

Chadema wanatakiwa wapate umiliki wa zile nguo. Gari, matundu yake, nguo hizo na damu zake, viwekwe makumbusho ya chama, vitumike kama sehemu ya kielelezo cha safari ya mapambano ya kudai demokrasia nchini.

Umuhimu wa Chadema kumiliki kumbukumbu za tukio la Lissu ni kwa sababu yajayo ni mengi. Lissu anaweza kuhama chama, akastaafu siasa, isisahaulike, yeye ni binadamu. Chadema wanatakiwa kuhakikisha tukio la Lissu ni sehemu ya historia ya chama siku zote, si kwa nadharia, bali kwa mifano hai. Gari la Lissu na nguo zake ni mfumo mkubwa.