CUF wachapana makonde kabla ya kikao cha Baraza Kuu kuanza
Muktasari:
- Wajumbe 25 halali wasusia kikao baadhi yao wafunguka, CUF yajibu walidhibitiwa hawakuwa na nia njema
Dar es Salaam. Kikao cha Baraza la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF) cha kupitisha majina ya wagombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kimeanza kwa sintofahamu baada ya wajumbe kuchapana makonde ndani ya ukumbi wa Shabani Mloo, makao makuu ya chama hicho Buguruni jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo lililodumu kwa dakika kadhaa leo Jumatano Agosti 6, 2025 liliwahusisha wajumbe takribani 25 waliodai kuna wajumbe si halali, waliingia kwenye kikao hicho kinyume na katiba yao huku wakidai kutoridhishwa na utaratibu wa kikao hicho.
Kikao hicho cha Baraza la Uongozi kilipaswa kujadili ajenda kuu tatu ikiwamo ya kupitisha majina ya wagombea wa urais, kujadili na kupitisha rasimu ya ilani ya uchaguzi pamoja na kuandaa hoja kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa CUF unaotarajiwa kufanyika Agosti 9, 2025.
Kwa mujibu wa mashuhuda, vurugu zilianza baada ya viongozi waandamizi wa CUF akiwamo Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba, Katibu Mkuu, Husna Abdallah na Naibu Katibu Mkuu Magdalena Sakaya kuingia ukumbini.
Baadhi ya wajumbe waliopinga mwenendo wa kikao walitaka wale waliodaiwa kuingia kwa njia isiyo halali waondolewe, lakini viongozi waligoma hali iliyozua tafrani.
Akizungumza na Mwananchi jana, mjumbe mmoja aliyeomba asitajwe jina amesema, “mlango na madirisha ya ukumbi yakafungwa watu wakaanza kuzichapa.”
Amesema kwa kuwa milango na madirisha yalifungwa, wajumbe waliotaka kutoka kujinusuru na vurugu hizo, wakawa wanatapatapa wasijue la kufanya.
Mwananchi imeshuhudia vurugu hizo zikitulizwa na walinzi wa chama waliofanikiwa kufungua mlango na kuwezesha baadhi ya viongozi kutoka ukumbini bila kudhurika.
Profesa Lipumba na viongozi wenzake walitoka ukumbini hapo kuelekea ofisini, wakiwaacha wajumbe wakiendelea kuzichapa.
Wajumbe 25 wagomea kikao
Pamoja na vurugu hizo, kundi la wajumbe 25 waliodaiwa kuwa ni halali, wamegomea kushiriki kikao hicho kwa madai kinakiuka katiba na kanuni za CUF.
Mjumbe mwingine ambaye pia ameomba kutotajwa jina, amesema uamuzi wa kuruhusu watu wasiokuwa wajumbe halali kuhudhuria kikao hicho ulikuwa kinyume cha sheria za chama.
Amedai kuwa, ulikuwa ni mkakati wa kutaka kulazimisha kupitishwa kwa mgombea wa urais (hakumtaja jina).
Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa wajumbe waliogomea kikao hicho, Salum Mohamed amesema: “Tangu tulipofika hapa kutoka Zanzibar hatujapewa hata chakula. Wapo baadhi ya watu wanaitwa pembeni kupewa maelekezo huku wengine tukiwekwa pembeni. Tunajiuliza kuna ajenda gani ya siri? Huu si utaratibu sahihi.”
Salum amesema vurugu hizo zimechochewa pia na makundi ndani ya chama chao huku akionya kama hali hiyo itaendelea, huenda kukatokea mpasuko utakaosababisha chama kudhoofika wanapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
“Makundi yametufikisha hapa. Viongozi wanawapendelea watu wao. Ndiyo maana tumegomea kikao na tumeamua kurejea Zanzibar,” amesema mjumbe huyo.
Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa CUF, Mohammed Ngulangwa amesema wajumbe waliogomea kikao hicho walikuwa na nia ya kuvuruga amani na hawakuwa na hoja za msingi.
“Walinzi waliwadhibiti na kikao kiliendelea kama kawaida. Hakuna mjumbe asiye halali aliyeshiriki, wote waliokuwepo walikuwa wanajulikana na kuthibitishwa,” amesema Ngulangwa.
Amesema madai yaliyotolewa na wajumbe waliogomea kikao hayakuwa ya kweli na amesisitiza kuwa, lengo la kikao hicho ni muhimu sana kwa hatima ya chama chao, hasa kwa kuzingatia kuwa kililenga kupitisha majina ya wagombea wa urais na rasimu ya Ilani ya uchaguzi.
Hata hivyo, mvutano wa ndani uliodumu kwa siku kadhaa kabla ya kikao cha leo, umeendelea kutia doa mchakato mzima wa maandalizi ya uchaguzi kwa chama hicho kilichotarajiwa kuonyesha mshikamano na umoja.