Prime
Saa 96 za moto Chaumma, ACT Wazalendo, CUF
Muktasari:
- Vigezo vya uadilifu, uzalendo, uwezo wa kiuongozi na kukubalika kwa umma vinatajwa kuwa miongoni mwa misingi mikuu itakayoongoza mchujo wa wagombea urais wa vyama mbalimbali.
Dar es Salaam. Saa 96 ndizo zitakazoamua nani na nani watakaopeperusha bendera za vyama vya ACT Wazalendo, Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) na Chama cha Wananchi (CUF), katika nafasi ya urais Tanzania na Zanzibar kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.
Hiyo inatokana na ratiba za vyama hivyo kufanya vikao vya uamuzi kisha mikutano mikuu, ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kuwapitisha makada watakaopewa ridhaa hiyo, kushindana na mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan.
ACT Wazalendo, inatarajiwa kulikamilisha hilo leo Jumatano, Agosti 6, 2025 kumpitisha ama Luhaga Mpina au Aaron Kalikawe kuwa mgombea urais wa Tanzania huku Othman Masoud Othman kuwa mgombea wa nafasi hiyo kwa upande wa Zanzibar.
Saa hizo 96 ni kuanzia leo hadi Jumamosi Agosti 9, 2025 ambayo Chama cha Wananchi (CUF) watakuwa wanafanya mkutano wao mkuu.
Kwa upande wa Chaumma, ni John G’wanambuke ndiye aliyechukua fomu kuwania nafasi hiyo, huku majina mbalimbali yakitajwa kuja ‘ku-supraizi.’
Vikao hivyo pia, vinafanyika kwa CUF, kumpitisha kati ya Rose Kuhoji, Gombo Gombo na Mkungutila na upande wa Zanzibar ni Masoud Hamad Masoud na Mohamed Khatibu na Mohamed Mnyaa.
Vigezo vya uadilifu, uzalendo, uwezo wa kiuongozi na kukubalika kwa umma vinatajwa kuwa miongoni mwa misingi mikuu itakayoongoza mchujo huo, ikiwa ni turufu kwao na kujipunguzia mzigo wa kutumia nguvu kubwa kuwauza wagombea wao kwa hadhira.
Mbali na hivyo, kupitia mikutano hiyo vyama hivyo vinatarajiwa kuzindua ilani zao zinazoeleza dira, malengo na mikakati yao katika kutatua changamoto mbalimbali za kitaifa. Ahadi kwa wananchi kuhusu mambo ambayo chama hicho kitayatekeleza endapo kitapata ridhaa ya kuunda serikali.
Hatua hiyo inakuja huku vyama hivyo vikijipanga kuhakikisha vinatoa wagombea wenye ushawishi, umaarufu na uwezo wa kuleta ushindani wa kweli dhidi ya chama tawala katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na baadhi ya makatibu wakuu wa vyama hivyo, mikutano hiyo inaanza leo itafanyika kwa siri kubwa, ikihusisha vikao vya kamati kuu, sekretarieti na mashauriano ya ndani ya vyama, huku vingine ni mikutano mikuu.
“Hatufanyi kazi hii kwa pupa. Tunahitaji mtu mwenye dira, uthubutu na uwezo wa kujenga umoja wa kitaifa. Ni wakati wa upinzani kuonesha uimara na utayari wa kuongoza Taifa,” amesema mmoja wa kiongozi wa chama cha Chaumma.
Katika vyama 18, vilivyojizatiti kushiriki kinyang’anyiro cha uchaguzi huo, Chaumma, ACT-Wazalendo na CUF bado havijawajua wagombea wao kwa nafasi hiyo Ingawa pazia la uchukuaji na urejeshaji fomu walifungua muda mrefu.
Chaumma
Chaumma wanaingia kwenye hatua hiyo lakini hadi vikao hivyo vinaanza kuketiwa ni kada mmoja ambaye amechukua fomu ya kutiania kuwania urais wa Tanzania ambaye ni John G’wanambuke.
G’wanambuke aliyejiunga na chama hicho Julai 31, 2025 akitokea Chama cha Mapinduzi CCM, na mtiania wa ubunge wa Kisesa mkoani Simiyu alichukua fomu kuomba ridhaa ya chama chake kupeperusha bendera ya kuwania urais siku hiyo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma, John Mrema, vikao hivyo vilianza Agosti 4, 2025 kwa Sekretarieti ya Taifa na kufuatiwa na Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa itaketi leo, Agosti 6,2025.
“Mchakato utafikia kilele Agosti 7, 2025, kwa Mkutano Mkuu wa Taifa, utakaofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam. Mkutano huo unatarajiwa kuwa wa kihistoria kwa chama, kwani mbali na uzinduzi wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025-2030, pia chama kitafanya uteuzi rasmi wa wagombea wake wakuu wa urais,” amesema.
Mrema amesema wagombea watakaoteuliwa ni wa nafasi tatu kuu, urais wa Tanzania, Mgombea Mwenza na urais wa Zanzibar.
“Mchakato huo umefuata taratibu zote za kikatiba ndani ya chama, na unaongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chaumma, Hashim Rungwe, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika siasa za upinzani kwa zaidi ya muongo mmoja akiongoza chama hicho,” amesema Mrema.
ACT-Wazalendo
Chama cha ACT-Wazalendo kilianza kujifungia kuanzia jana kwa kufanya vikao vya sekretarieti, Halmashauri Kuu, na Kamati Kuu kama sehemu ya maandalizi ya mkutano huo unatarajiwa kuanza leo na kuhitimishwa kesho.
Wakati wanachama wakiwa na shauku na kumaliza ubishi wa nani anayetarajiwa kuwa mgombea urais hadi wanaingia kwenye mkutano huo, ni makada wawili pekee waliochukua fomu ya kutiania kugombea urais wa Tanzania.
Makada hao ni Kiongozi wa Chama hicho, Dorothy Semu, Aaron Kalikawe anayetokea tawi la chama hicho Bukoba Mjini naye alichukua fomu ya kuweka nia ya kuhitaji kuwa mgombea.
Tayari Dorothy ameshawasilisha nia yake ya kujitoa kwenye mbio za nafasi hiyo na chama kimesharidhia, huku Luhaga Mpina na Kalikawe ndiyo pekee watakaopigiwa kura za maoni ili mmoja agombee nafasi hiyo.
CUF
Chama cha Wananchi CUF, leo nacho kitaanza kujifungia kuanza vikao vya Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho kwa siku mbili kufanya maandalizi ya mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika Agosti 9, 2025 wa kumpata mgombea urais wa Tanzania na Zanzibar.
Miongoni mwa jukumu la baraza hilo kwanza ni kupitia majina sita ambapo kati ya watatu waliojitokeza kutiania kugombea urais wa Tanzania na wanaobakia kugombea urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Waliotiania urais wa Tanzania ni Rose Kuhoji, Gombo Gombo na Mkungutila na upande wa Zanzibar ni Masoud Hamad Masoud na Mohamed Khatibu na Mohamed Mnyaa ambapo wote walihojiwa na Kamati ya Uongozi ya chama hicho.
Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa CUF, Mohammed Ngulangwa amesema katika mkutano huo kamati ya uongozi ya chama hicho itawasilisha taarifa ya wagombea wa urais kwa Baraza la Kuu la chama leo.
Baraza Kuu baada ya kupitia wanatakiwa kuwasilisha majina hayo kwenye mkutano Mkuu wa CUF, utakaofanyika Agosti 9, 2025 ili wajumbe wafanye uamuzi wa kumchagua mgombea urais wa Tanzania na Zanzibar kwa tiketi ya CUF," amesema Ngulangwa