CUF yaeleza madhara kuchelewa Ripoti Kikosi Kazi

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kuchelewa kwa ripoti ya kikosi kazi ndiyo sababu ya baadhi ya mambo kushindwa kutekelezwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23.

Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kimeeleza kusikitishwa na hatua ya Kikosi Kazi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kutumia miezi 10 kukamilisha ripoti yake, ilhali kingeweza kufanya hivyo ndani ya mwezi mmoja.

Kauli hiyo imetolewa leo, Januari 26, 2023 na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alipozungumza na wanahabari kuhusu kikao cha Baraza Kuu la Chama hicho kilichoketi Januari 21 na 22 mwaka huu.

Katika taarifa yake hiyo, Profesa Lipumba amesema kucheleweshwa kwa ripoti hiyo kumesababisha mambo yaliyopaswa kutekelezwa ndani ya bajeti ya 2022/23 yashindikane.

"Kama hili lingetekelezwa ndani ya mwezi mmoja bajeti ya Serikali ya wakati huo ingezingatia baadhi ya mambo, ikiwemo Katiba Mpya na tume huru ya uchaguzi," amesema.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo amesema katika kikao hicho baraza limempongeza Rais Samia kwa hatua yake ya kufungua mikutano ya hadhara.

Amesema zuio hilo lilikuwa kinyume na natakiwa ya Katiba na hivyo mkuu wa nchi hakuwa na mamlaka ya kuzuia.
Kuhusu mfumuko wa bei, Profesa Lipumba amesema baraza hilo limesikitishwa na taarifa ya Tume ya Taifa ya Takwimu (NBS) inayoenda kinyume na uhalisia kuhusu kupanda kwa bei za vyakula.

Amesema taarifa hiyo inaonyesha bei zimeongezeka kwa asilimia 4.8, akifafanua bidhaa iliyouzwa Sh100,000 mwaka 2021 imeongezeka Sh4,800 Tu.

Ameeleza taarifa hiyo ipo kinyume na uhalisia na hivyo Serikali inapaswa kuboresha mifumo ya NBS ili itoe taarifa sahihi.