Dai la Katiba mpya lisigeuzwe maigizo

Baadhi ya wananchi wakiwa kwenye maandamano ya kuhamasisha umuhimu wa Katiba mpya. Picha na maktaba

Siku chache zilizopita Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro alitangaza kuwa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2023/2024 itaongezeka kwa Sh9 bilioni ambazo zitasaidia katika mchakato wa Katiba mpya ambalo ni dai la miaka 31 sasa.

Kila mdau wa demokrasia amekuwa akidai Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi, lakini kumekuwa na danadana kwenye utekelezaji wake.

Licha ya mchakato huo kupata nguvu ya aina yake katika utawala wa awamu ya nne, ulikwama mwaka 2015 baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuahirisha kura ya maoni kwa Katiba inayopendekezwa.

Fedha nyingi za umma zimekuwa zikitumika katika michakato ya upatikanaji wa Katiba lakini hakuna mafanikio. Imekuwa ni kama shamba la bibi kila mmoja anavuna anavyotaka.

Kimsingi tunahitaji viongozi wenye kuthubutu kushughulika na kiini cha madai ya Katiba badala ya kuzunguka kunakofanywa kila mara na fedha za umma ambazo zingetumika kuboresha huduma nyingine kuteketea pasi na matunda.

Tuna safari nyingine ya kuelekea katika Katiba mpya, tuna Sh9 bilioni zimetengwa. Sitarajii kuona na kusikia migawanyiko ya kisiasa kama iliyotokea miaka 10 iliyopita itukwamishe kufikia ndoto yetu.

Niwakumbushe safari ya dai la mchakato wa Katiba mpya ya Tanzania ulianza tangu mwaka 1992, kabla ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini 1995 kwa baadhi ya wadau kudai kwamba hatuwezi kuingia kwenye mfumo huo kwa kutumia Katiba ya chama kimoja.

Rais Ali Hassan Mwinyi aliunda Tume ya Jaji Francis Nyalali, huku Mwalimu Julius Nyerere akiwa kinara wa kuunga mkono, lakini hata hivyo kilichokusanywa na kupendekezwa kilifungiwa kabatini na badala yake waliweka viraka Katiba iliyopo na kuingia kwenye uchaguzi mkuu.

Tangu wakati huo hadi sasa kumekuwa na mchezo wa sumbuabwege unaopigwa na watu waliopo usukani kiasi cha kufanya majaribio ya kukumbusha mchakato huo lakini wanaishia njiani.

Mwaka 2010, mwanga wa kijani ulionekana kiasi cha Watanzania kuanza kupata matumaini kwa kitendo cha Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete kuamua kuutangazia umma dhamira na nia ya Serikali yake kuanzisha mchakato wa kutekeleza.

Mwaka 2011 mchakato ulianza kwa kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 83/2011 na baadaye ikatungwa Sheria nyingine ya Kura ya Maoni Na. 11/2013.

Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilitamka kuanzishwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilianzishwa chini ya Waziri mkuu wa zamani, Jaji Joseph Sinde Warioba, ikaratibu mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa rasimu ya kwanza ya katiba na kuzaa rasimu ya pili ya Katiba.

Kwenye Bunge hilo la Katiba, ambalo Makamu Mwenyekiti wake alikuwa Samia Suluhu, ambaye ni ndiye Rais wa Tanzania kwa sasa, ndiko mivutano mikali kuhusu masuala kadhaa yaliyomo kwenye katiba ilipoanzia kwa baadhi ya wajumbe wa bunge kutoka upinzani kususia mchakato.

Licha ya kususia huko, baadhi ya wajumbe waliobakia waliendelea na ikapatikana Katiba inayopendekezwa, lakini wengi waliiona kama imekosa mwafaka wa kitaifa na maridhiano ambayo yanaonekana ndiyo msingi wa kupata Katiba bora ya kitaifa yenye kukubalika na wengi.

Awamu ya tano ilikuwa, kimya haikutaka kabisa kujihusisha na suala hilo, japo vyama vya upinzani na wanaharakati walikuwa mstari wa mbele kuzungumza suala hilo liloonekana kuchochewa zaidi na kitendo cha serikali kuweka zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya upinzani.

Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia imekuja na kasi mpya ya kufufua tumaini jipya kwa Watanzania kwa kuwaahidi kuwapatia Katiba mpya.

Bado baadhi ya wadadisi wa mambo wanadai kuwa kitendo cha kuendelea kuunda tume na kamati ni kuendelea kupoteza fedha na badala yake alipaswa kujielekeza kwenye kuanzisha mchakato wa Katiba moja kwa moja ambayo ingekuwa msingi wa kushughulikia changamoto zote zinazolalamikiwa.

Rais Samia tangu aingie madarakani alianza kuunda kikosi kazi kilichokuwa kinapitia hoja zilizojitokeza katika mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa uliofanyika jijini Dodoma Desemba 15 hadi 17, na kinakusanya maoni kwa wadau.

Ameunda Tume ya Maboresho ya Haki Jinai inayoendelea kukusanya maoni, jambo linaloendelea kutoa wasiwasi kwa wadau na kuwaacha njiapanda na kuamini wanaweza kurejeshwa walikotoka ndio maana kwa sasa wameanza kushinikiza Rais atangaze ratiba ya kuanza mchakato huo.

Mtazamo wangu pamoja na Rais kuonekana kuwa na utashi wa kupatikana kwa Katiba mpya ni achukue mawazo na maoni ya wanaodai kuanza mchakato huo moja kwa moja badala ya kuendelea kuunda tume ambazo zimekuwa zikirudia kufanya mambo yale yale pamoja na kuonekana wanaodai hilo wako wachache.