Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Nchimbi aahidi miradi itakayoibadili Kibaha

Muktasari:

  • Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameeleza yatakayofanyika Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Kibaha. Ujenzi wa vituo vya kupoza umeme, soko la kisasa, stendi ya mabasi, barabara za lami na changarawe, kupanua mtandao wa maji na kuboresha sekta ya kilimo, ni miongoni mwa ahadi za Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Kibaha.

Mgombea mwenza wa urais wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amesema ahadi hizo na zingine zitatekelezwa wilayani humo, Mkoa wa Pwani katika kipindi cha miaka mitano iwapo watachaguliwa tena.

Uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais utafanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025 ambapo Watanzania milioni 37.6 waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Mpigakura wataamua hatma ya viongozi hao.

Dk Nchimbi ametoa ahadi hizo leo Ijumaa, Oktoba 10, 2025 katika mkutano wa kampeni, uliofanyika uwanja wa mpira wa Mama Salmini, Mlandizi, ukihusisha majimbo Kibaha Mjini na Kibaha Vijijini.

Katika mkutano huo, Dk Nchimbi amewaeleza wananchi kwa nini Samia Suluhu Hassan anafaa kuchaguliwa kuwa Rais, wagombea ubunge, Mahoud Jumaa (Kibaha Vijijini) na Sylvester Koka (Kibaha Mjini) na madiwani wachaguliwe.

Dk Nchimbi aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil na Misri amesema miaka minne na nusu ya Samia madarakani, hakuna eneo wala sekta iliyoachwa nyuma ikiwemo za afya, elimu, kilimo, mifugo, utalii, ujenzi wa barabara na kuifungua nchi kiuchumi.

Miongoni mwa ahadi ambazo Dk Nchimbi amezitoa kwa wananchi wa Wilaya ya Kibaha zitakazotekelezwa endapo Samia atashinda ni kwenda kuviunganishia umeme Vitongoji 48 vya Kibaha Vijijini. Vijiji vyote vishaunganishwa.

"Tunakwenda kujenga vituo viwili vya kupoza umeme Kibaha ili umeme upatikane wa uhakika usiwe unakatika katika," amesema Dk Nchimbi.

Amesema CCM endapo itashinda inakwenda kujenga stendi ya kisasa ya mabasi na soko jipya eneo la Mlandizi.

Miundombinu ya barabara ni ahadi inayojibu maombi ya Jumaa ambayo aliyawasilisha awali kwamba zinahitaji maboresho na ujenzi ili kurahisisha upitaji.

Dk Nchimbi amebainisha baadhi ya barabara ambazo zinakwenda kujengwa ni ya Mlandizi- Ruvu kilomita 23 kwa lami, Mlandizi- Maneromango kilomita 65, Mji wa Mlandizi na za Viwanda Kwala.

Mgombea mwenza huyo aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM amesema wanakwenda kuongeza mtandao wa maji yatakayonufainisha maeneo mbalimbali ya Kibaha yakiwemo ya Misugusugu, Kongowe, Visiga, Mtongani, Mlandizi na Ruvu.

Dk Nchimbi amesema wananchi wa Kibaha zaidi ya asilimia 70 ni wakulima na Serikali itaendelea kuboresha sekta hiyo kwa kutoa mbolea na mbegu za ruzuku.

Amesema wanakwenda kujenga na kuendeleza skimu za umwagiliaji, kuimarisha huduma za kilimo.

Dk Nchimbi ambaye atakuwa mshauri namba moja wa Rais Samia kama CCM itashinda amesema miaka mitano ijayo wataboresha huduma za afya kwa kuiboresha Hospitali ya Wilaya, ujenzi wa vituo vipya vya afya viwili na zahanati mpya tisa.

"Ufugaji haukuachwa nyuma, tunakwenda kukarabati mabwawa sita ya kizamani yawe ya kisasa, majosho mapya, mnada uwe wa kisasa, hakuna ambaye tunamuacha," amesema Dk Nchimbi.

Katika eneo la elimu, Dk Nchimbi amesema wanakwenda kujenga shule za msingi mpya tano za sekondari mpya nne. Madarasa mapya 60 kwa shule za zamani za msingi na 46 kwa sekondari.

"Yote haya yakikamilika yanakwenda kuifanya Kibaha kuwa ya kisasa na hilo ndilo lengo la Rais Samia na CCM. Kikubwa jitokezeni kwa wingi Oktoba 29, tukamchague Mama Samia, wabunge na madiwani wetu," amesema.

Alichokisema Jumaa, Ally

Mgombea ubunge wa Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa amesema:"Sisi wana Pwani hatuna mashaka hata kidogo wala wasiwasi kwamba Rais Samia atashinda kwa kishindo. Tuna uhakika na chama chetu, hatuna mashaka na wabunge wetu, wagombea wetu wamepimwa kwa vigezo vingi. Wakiletwa mbele yenu wana vigezo vyote."

Jumaa amesema wilaya ya Kibaha kati ya mwaka 2020 hadi 2025 wamepokea zaidi ya Sh21 bilioni za maendeleo na Rais Samia anasema maneno machache kazi nyingi. Fedha zimeingia Sh9.1 bilioni 2025/2026,

"Ameleta fedha Sh6 bilioni za utawala bora ambazo zimejenga majengo ya halmashauri, nyumba za watumishi.

Sh5.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri na uboresha unaendelea na kuna changamoto ya ukuta. Vituo vitatu vya afya vinajengwa," amesema.

Mgombea huyo amesema, wamepokea Sh3.5 bilioni ambazo zinajenga shule za sekondari nane na kati ya hizo wameipa jina la Samia Suluhu Hassan. Shule tatu za msingi zimejengwa.

"Tuna upungufu wa shule mbili za sekondari. Lengo ni kusogeza huduma kwa wananchi na kuondoa usumbufu kwa wananchi," amesema.

Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Wilaya ya Songea Mjini, Mkoa wa Ruvuma, Hamis Ally amesema Rais Samia amefanya mambo mengi katika sekta mbalimbali ikiwemo kudumisha amani.

"Twendeni tukaombe kura, mama zetu nenda mwambie Mzee nimekuja, nakuomba kura, akikuuliza kwa nini niipe kura CCM, mweleze tulipokuwa tunapata ujauzito kulikuwa na changamoto lakini sasa Samia ameleta vifaa bora kabisa kuonesha mwenendo wa mtoto tumboni hadi anajifungua," amesema.

Ally amesema, Serikali ya CCM imeboresha mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na kupunguza adha kwa wazazi na walezi na sasa hakuna usumbufu.

"Mama amelifungua taifa letu, tumepita Kilimanjaro watalii wanamiminika, alicheza filamu watu wakambeza, lakini leo mambo yanakwenda vizuri kabisaa," amesema Ally.