Gavu: Msijaribishe watu kwenye ubunge, Bahati anatosha

Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda akimnadi mgombea ubunge wa Mbarali mkoani Mbeya kwa tiketi ya CCM, Bahati Ndingo. Picha na Mpiga picha wetu

Muktasari:

  • CCM yazindua rasmi kampeni za ubunge Mbarali yawataka wananchi wa jimbo hilo kumchagua mgombea wao, wakisema ana sifa zote    na anajua changamoto cha wananchi wa jimbo hilo.

Mbarali. Katibu wa Oganaizesheni wa CCM, Issa Ussi Gavu amewataka wananchi wa Mbarali wasijaribishe kumchagua mbunge asiye sahihi kwani wakifanya hivyo watapoteza fursa muhimu.

Kauli hiyo ameitoa jana Jumapili Septemba 10, 2023 wakati wa uzinduzi wa kampeni za ubunge wa Mbarali zilizofanyika Uwanja wa Stendi ya Mabasi Rujewa wilayani humo mkoani Mbeya.

Kampeni hizo zilihudhuriwa na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi, mbunge wa Makete, Festo Sanga.

Uchaguzi wa mdogo wa Mbarali utafanyika Agosti 19 sambamba na kata sita za Tanzania Bara, jimbo hilo limekuwa wazi kutokana aliyekuwa mbunge wa Mbarali Francis Mtega kufariki Julai Mosi kwa ajali ya kugongwa na trekta (Power Tiller).

Katika uzinduzi wa jana, Gavu aliwataka wamchague Bahati Ndigo ili aendeleze kazi nzuri iliyofanywa na mtangulizi wake.

"Msipelekea mtu mwingine bungeni kwa kuwa Ndigo anatosha, ameonyesha utu na upendo kwa wananchi wa Mbarali.

"Ndingo ataendeleza upendo na ushirikiano, huyu ni Bahati ni jina na bahati pia kwa Mbarali, kwake hataki ubunge wa kujinufaisha kwake bali kuwasemea kero zenu. Bahati ameonyesha dhamira yake mpeni kura zenu," amesema Gavu.

"Yapo mambo ya kujaribisha lakini sio ubunge mkikosea mtajuta kwa muda mrefu, tafuteni mtu mwenye nia thabiti na huyu si mwingine ni Bahati. Endeleni kukumbushana bahati imeanguka kwenu wananchi wa Mbarali," amesema.

Naye, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, amesema "Kamati kuu tulipokaa kulikuwa na mapendekezo kadhaa walikuwa wagombea 25 lakini mama huyu (Ndingo), ndiye aliongoza kwa kura kuanzia ngazi ya awali, kwa hiyo anakubalika ndio maana chama kimerudisha."

Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia amesema Ndingo ana ushirikiano mzuri na wabunge wenzake akiwa bungeni ndiyo maana wamekuja kumpa sapoti.

"Dada yenu, binti yenu ni mtu mwenye ushirikiano mzuri na wabunge wenzake, ndiyo maana wabunge wenzake tumejikusanya hapa, tunaamini Septemba 19 atakuwa mbunge. Ni binti ninayemfahamu atawapa wananchi uwakilishi mzuri.

Dk Tulia amesema kwa kauli moja akiwa na wabunge wenzake walioambatana katika uzinduzi huo wanamuunga mkono Ndingo, akisisitiza ni mtu sahihi kwa wananchi wa Mbarali na atawapa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa majukumu yake.

Amesema Ndingo alipokuwa mbunge wa viti maalumu amefanya kazi kubwa ya kuuliza kuhusu hoja za wananchi wa Mbarali sambamba na kuchangia michango mbalimbali.

 "Sasa kama alikuwa anafanya kwa ushirikiano na Mtega (marehemu) sasa mkimpa kura atafanya vizuri zaidi kuliko zamani. Kitendo Ndingo kujishusha kwa  Wanambarali ni busara asitokee mtu akisema oooh…huyu alikuwa mbunge mbona anagombea tena haya ni mapenzi kwa wananchi wa Mbarali.

"Ule ubunge wa mwanzo ulikuwa unampeleka nchi nzima, sasa anataka kuwatumikia wazazi na wananchi wenzake wa Mbarali. Mnaye mtu sahihi atawakilisha vema mpeni kura awe mwakilishi wenu, msiwe na wasiwasi CCM ndio kina wajabu wa kushughulikia hoja zenu," amesema Dk Tulia.

Kwa upande wake, Ndingo amewaomba wajumbe wa kamati kuu akiwemo Pinda kufikisha suala la changamoto ya mgogoro wa ardhi kwa Rais Samia Suluhu Hassan akimuomba aruhusu wakulima kulima maeneo yaliyozuiliwa wakati taratibu zingine za kiserikali zikiendelea.

"Hapa unapotuona shughuli yetu kuu ni kilimo, leo unaona tunapendeza hivi hawa wazazi wetu wamelima na kutukuza kwa kilimo, sasa tunaomba turuhusiwe yale maeneo ambayo yalikuwa yakilimwa zamani ambayo hivi sasa yamezuiwa.

"Natambua hili jambo halifikia mwafaka bado kuna mvutano lakini mwaka 2022 tulizuiliwa kulima, kilimo chetu ni cha mkopo ingawa uamuzi wa Serikali ulikuwa sahihi. Lakini  naomba ulibebe jambo hili ulibebe mpeleke Rais Samia," amesema Ndingo.