Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hapi: Viongozi CCM tatueni kero za wananchi acheni kushughulikiana

Katibu Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Ally Hapi akihutubia wananchi na makada wa Chama hicho Manispaa ya Geita. Picha na Geofrey Chubwa.

Muktasari:

  • Hapi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Juni 15, 2026, alipokuwa akizungumza na makada wa chama hicho katika Ofisi za CCM Wilaya zilizopo Kata ya Kalangalala, Manispaa ya Geita alikoanza ziara ya kikazi ya kukiimarisha chama.

Geita. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ally Hapi, amewataka viongozi wa chama hicho kuacha kujikita katika vikao vya kushughulikiana ndani ya chama na badala yake kuelekeza nguvu katika kutatua kero za wananchi.

Amesema CCM haiwezi kuwa chama cha vikao visivyo na tija, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kutoka ofisini na kwenda kwa wananchi kusikiliza na kutatua changamoto zao.

“Hatuwezi kuwa chama cha vikao, tuache vikao vya kushughulikiana, vikao visivyo na tija, twende kwa wananchi tuzungumze nao tutatue shida zao,” amesema Hapi.

Hapi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Juni 15, 2026, alipokuwa akizungumza na makada wa chama hicho katika Ofisi za CCM Wilaya zilizopo Kata ya Kalangalala, Manispaa ya Geita alikoanza ziara ya kikazi ya kukiimarisha chama.

Katika hatua nyingine, amedai kuwepo kwa taarifa kwamba baadhi ya wenyeviti wa vijiji na watendaji wa serikali za mitaa wanashirikiana na maofisa ardhi kuchochea migogoro ya ardhi badala ya kuitatua, amesema CCM haitasita kuchukua hatua kwa wote watakaobainika kuihujumu Serikali.

Aidha, Hapi amewataka wananchi wa Mkoa wa Geita kuwa makini na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani, akidai kuwa baadhi yao ‘wamevaa koti la ukoloni nyuma yao.’

Amesema baada ya Tanzania kupata uhuru mwaka 1961, wakoloni walibadilisha mbinu na kuanza kutumia baadhi ya vyama vya upinzani  kuvuruga amani ya Tanzania na Bara la Afrika.

Katika hoja zake, ametolea mfano baadhi ya miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo ya Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere na Daraja la Kigongo–Busisi mkoani Mwanza, kuwa ilipingwa na baadhi ya viongozi wa upinzani wakati wa Serikali ya awamu ya tano, lakini kwa sasa inaungwa mkono na kusifiwa.

Hapi amewataja baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliowaita Heche, Lema na Lissu, waliotembelea mkoani Geita hivi karibuni, akisema hawazungumzi hoja mbadala za maendeleo.

“Hutawasikia wakizungumza hoja zao mbadala kwenye maji, kwa sababu wakiongelea maji mfadhili wao hatoi fedha kwenye maji; wakiongelea afya hatoi fedha kwenye afya,” amesema Hapi.

Ameongeza kuwa, “Ili wapewe fedha lazima waseme katiba mpya, maandamano, tutakinukisha, tume huru, haya ndiyo mambo ambayo yule anayewapa fedha anataka kuyasikia.”

Pia amewataka wananchi kutodanganywa na michango ya fedha inayotolewa na Chadema kupitia mfumo wa “Tone tone”, akidai kuwa ni sehemu ya utakatishaji fedha wa wafadhili wao.

“Msihadaike na hiyo Tone tone, ni utakatishaji wa fedha ili mjue kwamba wanafanya mikutano kwa fedha za tone tone lakini wanatakatisha fedha za wafadhili wao,” amesema.

Hata hivyo, kauli ya Hapi inakuja katika kipindi cha mjadala wa kisiasa kati ya CCM na Chadema, ukiendelea kushika kasi kupitia majukwaa mbalimbali ya kisiasa.

Mei 17, 2026, viongozi wa Chadema kitaifa walipokuwa katika mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Shule ya Msingi Uwanja, Manispaa ya Geita, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche alisema wakazi wa Geita licha ya kuzungukwa na utajiri wa dhahabu, bado wanaishi katika mazingira magumu.

Heche alieleza kuwa hali hiyo inatokana na Serikali kutoweka mazingira rafiki ya kusaidia wananchi, ikiwemo kushughulikia changamoto ya ajira kwa vijana, akisisitiza kuwa wananchi wanahitaji kuona matokeo ya maendeleo hapa duniani na si kuahidiwa maisha bora ya baadaye pekee.

Chadema katika mikutano yake imeendelea kusukuma ajenda ya Katiba Mpya pamoja na kile kinachotajwa kama ‘Free Tundu Lissu’, wakishinikiza kuachiliwa kwa mwenyekiti wao anayeshikiliwa kwa zaidi ya mwaka mmoja mahabusu akishitakiwa kwa kesi ya uhaini.