Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Heche: Tuhuma dhidi yangu zinanipa nguvu ya kupambana

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche akizungumza na wazee wa Mkoa wa Mara Mjini Tarime leo Ijumaa Julai 17, 2026.

Muktasari:

  • Heche ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na baadhi ya wazee wilayani Tarime, ambapo amesema yeye ni mtu mwenye msimamo na si wa kugeuka nyuma pale anaposikia vishindo.

Tarime. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Heche amesema morali ya kupambania haki imeongezeka zaidi licha ya mambo kadhaa yanayoendelea dhidi yake, ikiwemo tuhuma za ubadhirifu wa fedha za chama hicho, huku akisema yeye ni dhahabu na hawezi kuchafuka.

Amesema kwa sasa uelekeo wake ni katika kufanikisha hoja na maelekezo ya Kamati Kuu ya chama hicho ambayo ni "Free Tundu Lissu" pamoja na "Katiba Mpya", na kwamba kamwe hakuna wa kumtoa katika kutekeleza mambo hayo.

Akizungumza na baadhi ya wazee wilayani Tarime leo, Ijumaa Julai 17, 2026, Heche amesema yeye ni mtu mwenye msimamo na si wa kugeuka nyuma pale anaposikia vishindo.

Heche amesema anapata nguvu za kupambania haki kupitia hoja mbili za chama hicho kutokana na idadi kubwa ya Watanzania wanaokiunga mkono chama hicho, huku akisema idadi hiyo iko wazi, ikiwa ni pamoja na namna watu wanavyounga mkono maazimio na maombi ya chama hicho.

Baadhi ya wazee wilayani Tarime wakiwa kwenye kikao na Makamu Mwenyekiti wa Chadema bara John Heche (hayupo pichani) mjini Tarime. Picha na Beldina Nyakeke

Ametolea mfano mwitikio wa Watanzania kuchangia gharama za mkutano wa Baraza Kuu la Chadema, ambapo hadi kufikia saa 10 jioni leo, Julai 17, 2026, zaidi ya Sh120 milioni zimechangwa na Watanzania kwa ajili ya kufanikisha mkutano huo.

"Kuna watu wamechangia Sh100, 200, 85, hebu fikiria watu wanaotoa kiwango hicho cha fedha hadi kupata Sh120 milioni kwa siku tano, unadhani ni watu wengi kiasi gani?" ameeleza.

Amesema nia yake bado iko pale pale na hatapoteza muda kujibu yanayosemwa dhidi yake kwani yamelenga kumtoa kwenye uelekeo.

"Mwendo unapokuwa mgumu sana, wale wagumu sana ndio wanasonga mbele. Sasa huyo mgumu ndiye mimi. Sehemu zile ngumu ndio nataka kupita na hakuna wa kunizuia kupita," amesema.

Wazee wakimkabidhi zawadi ya mbuzi, Makamu Mwenyekiti wa ChademaBara, John Heche baada ya kumaliza kuzungumza nao mkoani Tarime leo.

Amesema kwake suala la kukata tamaa halina nafasi na ujasiri huo anaupata kupitia Watanzania wengi ambao mara kwa mara wamekuwa wakimtia moyo, hivyo hawezi kuwaangusha, huku akisema harakati za chama hicho za kupambania haki zitaendelea tena kuanzia wiki ijayo.

Amesema mkutano wa Baraza Kuu unaotarajiwa kufanyika Septemba utatoa mwelekeo mzuri kwa ajili ya ustawi wa Watanzania na nchi kwa ujumla.

Heche amesema uamuzi wa chama hicho kutoshiriki Uchaguzi Mkuu mwaka jana haukuwa wa bahati mbaya, badala yake ulifanyika kwa makusudi ili kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata kile wanachostahili.

Amesema kabla ya uamuzi huo, chama hicho kilipata fundisho kupitia kushindwa kufanyika kwa uamuzi kuhusu masuala kadhaa waliyokubaliana kupitia maridhiano baina ya viongozi wa chama hicho na Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni pamoja na namna uchaguzi wa serikali za mitaa ulivyofanyika.

"Kulikuwa na kigugumizi kuruhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa licha ya kukubaliana katika maridhiano. Mikutano hii iliruhusiwa kwa shida sana baada ya mwaka mmoja tangu kufanyika maridhiano, lakini kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa asilimia 90 ya wagombea wa Chadema waliondolewa. Sasa hapo tungeamini vipi kuwa Uchaguzi Mkuu utakuwa huru na wa haki?" amesema.

Baadhi ya wazee wilayani Tarime wakiwa kwenye kikao na Makamu Mwenyekiti wa Chadema bara John Heche (hayupo pichani) mjini Tarime. Picha na Beldina Nyakeke

Amesema Chadema wanahitaji utawala na uongozi utakaopatikana kwa njia za haki na uhuru, na kwamba hilo litawezekana kupitia Katiba Mpya ambayo itawapa haki na uhuru wananchi kuwachagua viongozi wanaowataka.

Heche amesema hali hiyo itachochea kupatikana kwa maendeleo endelevu kwa maslahi ya Watanzania wote, hivyo ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuunga mkono jitihada za chama hicho ili kufikia matokeo yanayotarajiwa.

Akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chadema Wilaya ya Tarime, Nyangoko Thomas, amewataka wazee nchini kuungana pamoja kukemea maovu yanayotokea ili kuwa na jamii yenye ustawi na inayoheshimu haki za binadamu.

Amesema hivi karibuni kumeibuka makundi ya watu, wakiwemo wazee, ambao wamekuwa wakitoa kauli ambazo wanadai ni za kumuonya Heche, jambo ambalo amesema si busara kwa maelezo kuwa Heche anapaswa kuungwa mkono na kila mpenda haki nchini.

"Uzee ni pamoja na kuwa na busara. Kama huna busara, basi huna sifa ya kuitwa mzee. Hawa wanaomkemea Makamu Mwenyekiti nilitarajia wawe mstari wa mbele kukemea maovu yanayotokea katika jamii yetu, ikiwemo katika Wilaya yetu ya Tarime," amesema.

Wazee wakimkabidhi zawadi ya mbuzi, Makamu Mwenyekiti wa ChademaBara, John Heche baada ya kumaliza kuzungumza leo Ijumaa Julai 17, 2026 wilayani Tarime.

Amesema wamebaini uwepo wa baadhi ya watu katika jamii ambao kwa makusudi wameanzisha harakati za kumchafua kiongozi huyo, jambo ambalo wao hawatakubaliana nalo, na kwamba wapo tayari kumlinda kiongozi wao kwa namna yoyote ile.

Thomas amesema miongoni mwa majukumu ya Serikali ni pamoja na kulinda raia na mali zao. Hivyo, kama jukumu hilo halitekelezwi ipasavyo, ni lazima ikumbushwe wajibu huo kama ambavyo amekuwa akifanya Heche.

Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Tarime Mjini, Bashiri Selemani, amemtaka Heche kutokata tamaa kwa maelezo kuwa mashambulizi anayoyapata ni kutokana na namna ambavyo amekuwa akiwatetea wananchi na rasilimali za nchi.

Amesema ni wakati wa Heche kuwa na subira na kamwe asipoteze uelekeo, huku akisema kuwa Chadema inalenga kushika dola, hivyo mashambulizi kutoka chama tawala ni jambo la kawaida.

"Mashambulizi kama haya lazima yatokee kwani hata sisi hatuwezi kuwaambia maneno laini. Tunataka kushika dola na wao hawataki kuachia dola. Nakuomba usikate tamaa, haya mashambulizi ni halali yako na sisi tunakuahidi tutakuwa pamoja nawe," amesema.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Mara, Donald Mwembe, amesema chama hicho hakitasita kumvua uanachama mwanachama yeyote ambaye atashiriki katika mikutano ya waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa madai ambayo amesema hayana ukweli wowote.

"Sasa hivi tunapiga doria kwenye mitandao. Endapo kuna mwanachama au kiongozi yeyote wa Chadema kutoka Mkoa wa Mara atashiriki kwenye hivyo vikao uchwara, sisi tutaruka naye. Hatuna muda wa kupoteza na watu wasiokitakia chama chetu mema," amesema.