Heche: Tutasema ukweli hadi mwisho licha ya vitisho
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Heche wakati akizungumza katika mwendelezo wa mikutano ya hadhara ya Operesheni Katiba Mpya na “Free Tundu Lissu” iliyofanyika leo Jumatatu Mei 18, 2026 Kahama, mkoani Shinyanga.
Muktasari:
- Heche amesema hayo leo Jumatatu Mei 18, 2026 katika mwendelezo wa mikutano ya hadhara ya Operesheni Katiba Mpya na “Free Tundu Lissu” iliyofanyika Kahama, mkoani Shinyanga
Kahama/ Dar. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Heche amesema chama hicho kitaendelea kusimamia ukweli licha ya vitisho vinavyoendelea kuelekezwa kwa viongozi wake.
Heche amesema hayo leo Jumatatu Mei 18, 2026 katika mwendelezo wa mikutano ya hadhara ya Operesheni Katiba Mpya na “Free Tundu Lissu” iliyofanyika Kahama, mkoani Shinyanga.
Heche amesema chama hicho hakiwezi kufumbia macho changamoto zinazowakabili wananchi, ikiwamo ubovu wa miundombinu na ukosefu wa huduma muhimu.
Amesema haiwezekani viongozi wapite kwenye barabara mbovu kisha waseme ni nzuri, au kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama halafu wakadai huduma hiyo inapatikana.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Heche wakati akizungumza katika mwendelezo wa mikutano ya hadhara ya Operesheni Katiba Mpya na “Free Tundu Lissu” iliyofanyika leo Jumatatu Mei 18, 2026 Kahama, mkoani Shinyanga.
“Tusitishane hapa duniani. Tulizaliwa mara moja na tutakufa mara moja, hakuna mtu anayetakufa mara mbili. Chadema ni waumini wa amani lakini hatuwezi kukubali kuonewa,” amesema Heche
Amesema kusema ukweli kuhusu ugumu wa maisha ya Watanzania si kosa wala uvunjifu wa amani kuna baadhi ya watu wanaendelea kupora rasilimali za nchi, ikiwamo madini, huku wananchi wakibaki na mashimo na umaskini.
“Hatutakubali kukaa kimya na kushindwa kusema ukweli. Tutanyamaza tukiwa makaburini, lakini tukiwa hai tutaendelea kusema ukweli. Hatutaki Taifa letu ligeuke kuwa Taifa la uongo,” amesema.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Mzee, amewataka wananchi wa Kahama na Watanzania kwa jumla kuwaenzi waliofariki dunia katika maandamano ya Oktoba 29, 2025 kwa kuendelea kukijenga chama hicho katika harakati za kupigania haki.
Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi wa matukio hayo iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman inaonesha waliofariki dunia ni 518.
Mzee amesema wananchi wanapaswa kujitolea kwa vitendo katika kukijenga chama hicho ambacho kimekuwa mstari wa mbele kutetea haki za wananchi.
Ameongeza kuwa matukio kama hayo yaliwahi kujitokeza Zanzibar na kusababisha kuwepo kwa wakimbizi wengi.
“Mjitoe kwa vitendo katika kujenga chama chetu kilicho mstari wa mbele kupigania haki za wananchi wetu. Mambo kama haya yaliwahi kujitokeza Zanzibar na kuzalisha wakimbizi wengi,” amesema.
Amesema waliopo madarakani wanapaswa kutambua kiburi hakina nafasi, kwani hali ya nchi imeharibika na Taifa limegawanyika, hivyo ni wajibu wao kutafakari na kurekebisha hali hiyo.
“Heshima ya nchi imepungua kimataifa, hatuwezi kuendelea kuishi hivyo. Chadema ni tumaini la Watanzania, hivyo ni lazima tuchukue jukumu la kuwaunganisha wananchi,” amesema.
Mzee amesema chama hicho kinaamini katika mazungumzo na upande wa pili, lakini msimamo wao ni kwamba jumuiya za kimataifa lazima zishiriki kwa sababu hawaamini upande huo kutokana na kubadilika kwa misimamo yao mara kwa mara.
“Ikiwa mechi za Simba na Yanga zinachezeshwa na waamuzi kutoka nje ya nchi, inakuwaje Chadema izungumze na hawa watu wakati tunajua hawaaminiki? Kikubwa wananchi waendelee kuchangia chama chetu,” amesema.
Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema operesheni inayoendelea ya chama hicho si ya Chadema pekee, bali ni mjadala wa kitaifa unaolenga kuwakomboa wananchi dhidi ya umasikini uliokithiri.
Amewataka wananchi kuipokea operesheni hiyo yenye kaulimbiu ya “Katiba Mpya, Free Tundu Lisu” kwa kudai haki, ukweli na uwajibikaji ambao amesema umepotea nchini.
Amesema mambo hayo yatawezekana endapo kutapatikana Katiba mpya yenye uwezo wa kuwawajibisha viongozi waliopo madarakani.
“Katiba ndiyo chanzo na mzizi wa matatizo yetu. Baada ya mwaka 1992 kuanzishwa mfumo wa vyama vingi, bado changamoto nyingi zimeendelea kuwepo,” amesema.
Amesema mkutano huo si wa kisiasa pekee, bali ni sehemu ya mazungumzo ya kitaifa kuhusu ubovu wa Katiba na athari zake kwa haki za wananchi.
“Huu si mkutano wa hadhara tu, ni mazungumzo ya kitaifa. Ubovu wa Katiba yetu unasababisha Watanzania kukosa haki zao. Ukweli, haki na uwajibikaji vinahitajika,” amesema.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless Lema, amesema chama hicho ni chanzo cha amani nchini, hivyo juhudi zozote za kutaka kukifuta ni sawa na kuhatarisha utulivu wa Taifa kwa kuwa, wananchi watakosa sehemu ya kusikiliza sera mbadala.
“Hakuna kitu kinacholeta amani kama mikutano ya siasa. Mfumo huo ukiondolewa, watu wanaweza kuanza kufanya mambo yasiyotabirika kwa sababu majukwaa ya kutoa maoni yatakuwa yamefungwa,” amesema Lema.
Katibu wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha), Pamela Maassasy.
Amesema chama hicho hutumia majukwaa hayo kuwakutanisha wananchi wenye changamoto mbalimbali ili kueleza matatizo yao na kudai haki zinazodaiwa kukandamizwa na baadhi ya watu waliopo katika mifumo ya utawala.
Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Boniface Jacob maarufu Boniyai amesema propaganda za kutaka Chadema ifungiwe hazipaswi kuungwa mkono kwa kuwa, chama hicho kimekuwa mstari wa mbele kupigania haki za wananchi.
“Kumekuwa na chokochoko za kutaka Chadema ifungiwe. Nawauliza wananchi, kuna chama kingine kinachopigania haki za Watanzania kwa kiwango hiki zaidi ya Chadema? Kamwe msikubali mpango huo,” amesema Boniyai.
Amesema Chadema imekuwa ikitetea hata haki za wafanyakazi, wakiwamo askari polisi, kwa kutaka wawe na maisha bora kutokana na ugumu wa kazi wanazofanya.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila amewataka wanachama wa chama hicho kujiandaa kisaikolojia iwapo chama hicho kitafungiwa au kusimamishwa shughuli zake.
“Nyie vijana wa Kahama jiandaeni. Siku mkisikia chama chetu kimefungiwa au kusimamishwa, hawa watu tuwachezeshe kindumbwendumbwe. Wao wenyewe wachague watacheza wakiwa wamechuchumaa, wamesimama au wamelala,” amesema.
Mahinyila amesema migogoro huanza kidogo kama chombo kinachotobolewa taratibu, hivyo akashauri viongozi na wananchi kuepuka ugomvi.
Amesema vijana wa chama hicho wameamua kutokuwa wabinafsi kwa kujadili masuala ya ajira na mikopo pekee, bali wanahitaji Katiba mpya itakayokuwa mwanga kwa vizazi vijavyo.
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha), Pamela Masasy amesema mwitikio mkubwa wa wananchi katika mikutano ya Chadema unaonesha wanahitaji haki na wanataka kuona rasilimali za Taifa zinawanufaisha.
“Wananchi wengi wanaishi maisha duni, wanakosa elimu bora pamoja na majisafi na salama. Haya yote yanatokea kwa sababu hakuna viongozi bora wanaosimamia rasilimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi,” amesema.
Amesema wananchi wengi wana matumaini makubwa na Chadema kutokana na msimamo wake wa kudai Katiba mpya.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema (Bazecha), Suzan Lyimo amesema haki haiwezi kupatikana nchini bila kuwepo kwa uwajibikaji wa kweli kutoka kwa viongozi.
“Tunaposema tunahitaji Katiba mpya, tunamaanisha kwamba kuna mambo mengi yanayofanyika kwa kupora haki za wengine huku kukiwa hakuna uwajibikaji wa viongozi,” amesema.