Prime
HOJA YA MALOTO: Ni wakati mwafaka tarehe ya uchaguzi mkuu iwepo kikatiba

Katiba ya Marekani, Sehemu ya kwanza, kifungu cha nne, Bunge la Marekani, limepewa mamlaka ya kuamua siku ya uchaguzi kikatiba.
Yaani siku ya kuchagua wajumbe wa kura za majimbo na ile ambayo wajumbe hao watapiga kura kuchagua rais mpya.
Congress walishapitisha siku ya taifa ya uchaguzi. Ni Jumanne ya kwanza baada ya Jumatatu ya kwanza ya Novemba.
Yaani, Jumatatu ya kwanza ya Novemba, siku inayofuata (Jumanne) ni siku ya taifa ya uchaguzi, kila baada ya miaka minne.
Ufafanuzi, endapo Novemba Mosi inakuwa Jumanne, hiyo haipaswi kuwa siku ya uchaguzi. Ni sharti Jumanne ya uchaguzi ifuate baada ya Jumatatu ya kwanza ya Novemba.
Ikitokea Novemba Mosi ni Jumatatu, basi uchaguzi unakuwa siku inayofuata, yaani Jumanne ya Novemba 2.
Sasa, kikatiba kama ilivyopitishwa na Congress, kila Jumanne ya baada ya Jumatatu ya kwanza ya Novemba, kila baada ya miaka minne, wananchi hupiga kura kuchagua wajumbe wa kura za majimbo.
Halafu, kila Jumatatu inayofuata baada ya Jumatano ya pili ya Desemba, wajumbe wa kura za majimbo hupiga kura kuchagua rais na makamu wa rais.
Wajumbe wa kura za majimbo wakishapiga kura kwenye majimbo yao, huzifunga kwenye bahasha maalumu kisha kuelekezwa kwa rais wa
seneti, ambaye ni makamu wa rais wa Marekani. Naye Makamu wa rais haruhusiwi kufungua bahasha hizo za kura za majimbo, mpaka maseneta wawepo kushuhudia.
Makamu wa rais (rais wa seneti), mbele ya maseneta, hufungua bahasha za kura za majimbo na kuhesabu. Baada ya hapo, rais
aliyeshinda hutangazwa rasmi.
Na Januari 20, ndiyo siku ambayo rais huapishwa tayari kuanza majukumu mapya ya uongozi.
Uwepo wa tafsiri ya siku ya uchaguzi kisheria, hufanya mifumo yote kuenenda kulingana na kalenda. Vyama huanza kujiandaa kwa wakati,
na mamlaka za uchaguzi huwajibika ndani ya muda. Haiwezekani kusogeza mbele au kurudisha nyuma.
Tanzania, kiutamaduni kabla ya Uchaguzi Mkuu 2020, ilikuwa imezoeleka kwamba, Jumapili ya mwisho wa Oktoba, kila baada ya miaka mitano, Watanzania watakusanyika vituoni kupiga kura, kuchagua viongozi wa muhula mpya.
Jumapili ya mwisho wa Oktoba, kila baada ya miaka mitano, haikuwa imeandikwa kikatiba, wala haikuwepo kisheria. Angalau ni utamaduni ulioheshimiwa kwa muda mrefu. Watanzania wafuatiliaji walijua bila shaka kwamba kila baada ya miaka mitano, Jumapili ya mwisho wa Oktoba, ungefanyika uchaguzi mkuu.
Uchaguzi Mkuu 2020 ulikuja na mabadiliko. Kwanza, ilikuwa mara ya pili Tanzania kufanyika katikati ya wiki. Ilikuwa Jumatano, Oktoba 28, 2020.
Ziliongezeka siku tatu, kutoka Jumapili ya mwisho wa Oktoba 2020, ambayo ilikuwa Oktoba 25.
Kuweka kumbukumbu sawa, Uchaguzi Mkuu 2005, ulifanyika pia Jumatano, katikati ya wiki. Hii ilikuwa kwa sababu ya dharura. Uchaguzi ulipaswa kufanyika Jumapili ya mwisho wa Oktoba, ambayo ilikuwa Oktoba 30, 2005. Hata hivyo, siku chache kabla ya uchaguzi, aliyekuwa mgombea mwenza wa Chadema, Jumbe Mohamed Jumbe, alifariki dunia.
Iliyokuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), iliahirisha uchaguzi hadi Desemba 14, 2005 (Jumatano). Hii ilikuwa dharura, na ilibidi Rais aliyekuwa anamaliza muda wake, Benjamin Mkapa, atangaze siku hiyo kuwa ya mapumziko ili kuruhusu Watanzania kujitokeza kwa wingi kuchagua viongozi wao.
Uchaguzi Mkuu 2015, ulifanyika Oktoba 25, 2015 ambayo ndiyo ilikuwa Jumapili ya mwisho wa Oktoba. Inawezekana, NEC, wakati huo waliona hesabu zao hazipo sawa, hivyo kusogeza mbele mpaka Oktoba 28, 2020. Urahisi huu unasababishwa na tarehe kutokuwepo kikatiba wala kisheria.
Mambo mengi yanatokea Tanzania. Chadema kuonekana wamejinyima fursa ya kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025, kwa kugomea kusaini fomu za maadili ya uchaguzi, vilevile vyama vya upinzani kuonekana havijawa na maandalizi ya kutosha. Yote hayo yanahusiana moja kwa moja na tarehe ya uchaguzi.
Laiti tarehe ya Uchaguzi Mkuu 2025, ingekuwa inafahamika kisheria, bila shaka kalenda ya matukio yote ingekuwa inajulikana.
Ni kwa msingi huo, vyama vingetambua wakati gani wa kufanya nini. Hivi sasa, inaonekana kwa asilimia kubwa vyama vya upinzani havijajiandaa kwa uchaguzi.
Januari 19, 2025, wajumbe wa Mkutano Mkuu CCM, wakifanya uamuzi nje ya utaratibu uliowekwa na Katiba yao. Walimpitisha Dk Samia Suluhu Hassan, kuwa mgombea urais, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Hussein Mwinyi, kuwa mgombea urais Zanzibar. Dk Samia alimteua Dk Emmanuel Nchimbi, kuwa mgombea mwenza wake.
Ulikuwa uamuzi nje ya utaratibu wa Katiba ya CCM, lakini Katiba hiyohiyo imetoa mamlaka kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu CCM kufanya uamuzi wowote na utahesabika kuwa halali na ndiyo wa mwisho kwenye chama hicho. Hivyo, wajumbe walitumia mamlaka yao kikatiba.
CCM wamekuwa na kasi kubwa kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, ingawa tarehe rasmi haijatangazwa. CCM ina wagombea wote wa kitaifa, mchakato wa majimbo na kata, umeshakamilika hatua ya uchukuaji, ujazaji na urejeshaji fomu. Wanasubiri vikao vya kitaifa kupitisha wagombea wa majimbo.
Hadi sasa, hakuna chama chochote cha upinzani ambacho kimeshatangaza mgombea wake wa urais. Angalau ACT-Wazalendo, walishamwonesha kiongozi wao, Dorothy Semu, akichukua fomu ya kuomba uteuzi wa kuwa mgombea urais. Vingine vipo kimya kabisa.
Ukimya uliotanda kwenye vyama vingi kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, unaweza kuleta ubashiri kwamba ama kuna ukata wa kifedha au hawajui namna ya kwenda mbele, maana hata tarehe rasmi ya uchaguzi hawaijui. Angalau Chadema, wao wapo kwenye mgomo wa kushiriki uchaguzi.
Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015, baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani, walilalamika kuwa kulikuwa na uwezekano wa Rais aliyekuwa
madarakani, Dk Jakaya Kikwete, kujiongezea muda wa kubaki ofisini, kwa kuwa tarehe ya uchaguzi ilichelewa kutangazwa.
Kikwete, alijibu kwa kushangaa, lakini muda mfupi baadaye tarehe ilitangazwa kuwa ni Oktoba 25, 2015.
Maneno kama hayo yalitokea kwa sababu tarehe ya uchaguzi imeachwa kwa tume kuamua, wakati ilitakiwa itungiwe sheria, ili kusiwe na mivutano wala konakona.
Tarehe ya uchaguzi ikiwepo kikatiba na kutungiwa sheria, itatoa uhakika kwa vyama mapema kuhusu uchaguzi.
Itakuwa rahisi kwao kujipanga kifedha, kimichakato na kimikakati kuelekea uchaguzi. Chama ambacho kitakuwa na unyonge, hakitakuwa na wa kumlaumu. Maana ni chenyewe kitakuwa kimeshindwa kujipanga.