Katiba ilivyotoa mwanga mabadiliko kutoka Magufuli hadi Samia

Muktasari:

  • Katiba ni msahafu wa nchi. Maudhui yake, ibara kwa ibara, kifungu hadi kifungu, ndiyo mwafaka wa nchi. Taifa limejiwekea utaratibu wa kuishi kwa kufuata maandishi hayo. Viongozi huapishwa kuitii Katiba, kwa maana kipindi chao cha utumishi, hawatakiwi kuyakiuka hayo maandishi, isipokuwa waenende kulingana na yaliyoandikwa.

Venance Mabeyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) mstaafu, ameipa uhalali minong’ono iliyochipua Machi 17, 2021, siku Rais wa awamu ya tano, Dk John Magufuli, alipofariki dunia. Ilinong’onwa kuwa baada ya Magufuli kufikwa na mauti, ziliibuka hila dhidi ya Samia Suluhu Hassan.

Ilidaiwa kuwa wapo watu, mpaka sasa hawajatajwa, eti walitaka kukiuka Katiba ili Samia asiapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mabeyo, CDF aliyekuwa kazini siku Magufuli anavuta pumzi ya mwisho, pamoja na kukiri kuwepo mjadala kabla ya uapisho wa Samia, lakini hajataja wahusika.

Rais kufikwa na mauti akiwa madarakani, lilikuwa tukio la kwanza kwa Tanzania. Katiba ya Tanzania, ibara ya 37 (5), inaeleza wazi kuwa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kikiwa wazi kutokana na kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kwa maradhi, Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliosalia. Halafu Makamu wa Rais baada ya kuwa Rais, atateua Makamu wa Rais baada ya kushauriana na chama chake, kisha uteuzi huo utathibitishwa na Bunge.

Magufuli alifariki dunia. Makamu wa Rais alikuwepo, Samia. Kikatiba hakukuwa na kizungumkuti hata kidogo. Hata hivyo, kizunguzungu kilizaliwa kwa kutazama sifa za kimaumbile alizonazo Samia. Ni mwanamke. Halafu, Tanzania haikuwa imepata kuwa na Rais mwanamke. Hata Makamu wa Rais mwanamke, Samia ndiye wa kwanza.

“Sasa inawezekana watu Katiba walikuwa wameisahau kidogo, kukatokea maongezi tofautitofauti na nini, lakini tukasema tuna taratibu, nadhani tukizifuata hazina shida. Tuzizingatie zile ili mabadiliko ya uongozi yaende vizuri,” alisema Mabeyo.

Nukuu hii ya Mabeyo, japo ameizungumza kwa wepesi, inajenga picha kuwa baada ya Magufuli kufariki dunia, walitokea watu waliotaka kufanya hujuma ya kikatiba, halafu wengine, akiwemo Mabeyo, wakataka utaratibu wa kikatiba ufuatwe. Kiulizo kinachohitaji ufumbuzi ni majina ya wahusika.

Kauli ya Mabeyo inakumbusha nyakati za mwanzo za urais wa Samia, daima mkuu huyo wa majeshi mstaafu alikuwa jirani na Amiri Jeshi Mkuu. Kutokana na minong’ono iliyokuwepo kuwa kuna watu hawakutaka Samia awe Rais, wakati ilikuwa halali yake kikatiba, ukaribu wa Mabeyo ulibeba tafsiri ya kumlinda na kuwatisha waliokuwa na nia ovu.

Naikumbuka kauli yenye msisitizo mkubwa kutoka kwa Mabeyo, aliyoitoa Machi 26, 2021, Chato, siku ya mazishi ya Magufuli. Pamoja na kutoa uthibitisho kuwa mipaka ya nchi ilikuwa salama, Mabeyo alitoa ahadi: “Vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kukulinda wewe, kama Rais, kukutii, kama Amiri Jeshi Mkuu, katika kutekeleza majukumu yako, kama yalivyoainishwa na Katiba.”

Kunaweza kutokea ubishani. Wengine wakasema, kauli ya Mabeyo kumhakikishia ulinzi Rais Samia ilikuwa utamaduni wa kawaida kwamba Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama lazima alindwe, wapo wenye kusimama upande wa pili na kujenga hoja kuwa ahadi ya Mabeyo ililenga kuwakimbiza waliokuwa hawajakata tamaa dhidi ya urais wa Samia.

Kwa mujibu wa Katiba, baada ya madaktari kutamka kuwa Magufuli amekata roho, palepale cheo cha Samia kilihama kutoka Makamu wa Rais hadi Rais Mteule. Samia alikuwa Rais wa Tanzania aliyengoja kuapishwa, sawasawa na mshindi wa kiti cha urais aliyetangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Kama ambavyo jaribio lolote la kumzuia mshindi wa kiti cha urais kuapishwa na kushika madaraka kikatiba ilivyo mapinduzi, ndivyo uamuzi wowote wa kumzuia Makamu wa Rais kuongoza dola, baada ya Rais kufariki dunia au kukosa sifa za kuendelea kukalia kiti, kunaweza kuhesabiwa mapinduzi.

Mabeyo anaposema “yalitokea maongezi” yenye maudhui ya kumzuia Samia asiapishwe kuwa Rais, anamaanisha kulikuwa na jaribio ovu. Tena, jaribio baya kwa sababu lilitaka kuipindua Katiba. Ukipitia Sheria Namba 2 ya mwaka 1970, pamoja na Sura ya Saba, kifungu cha 39 na 40 cha Kanuni ya Adhabu, matukio kama hayo yanaangukia kwenye makosa ya uhaini.

Waliotajwa kusahau Katiba na kutaka kuipuuza, bila shaka si watu wa barabarani. Ni viongozi ambao vyeo vyao huhalalishwa na viapo vya utii wa Katiba. Kwa mantiki hiyo, aliyekula kiapo kulinda Katiba, ndiye alitaka kukiuka katiba.

Katiba ni msahafu wa nchi. Maudhui yake, ibara kwa ibara, kifungu hadi kifungu, ndiyo mwafaka wa nchi. Taifa limejiwekea utaratibu wa kuishi kwa kufuata maandishi hayo. Viongozi huapishwa kuitii Katiba, kwa maana kipindi chao cha utumishi, hawatakiwi kuyakiuka hayo maandishi, isipokuwa waenende kulingana na yaliyoandikwa.

Kama ambavyo hawi Mwislamu  yule ambaye anakiuka Quran, au Injili kwa Mkristo, ndivyo Mtanzania na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mithili ya shehe asiyeamini Msahafu asivyofaa msikitini, au kasisi anayepinga Biblia asivyokubalika kanisani, ndivyo kwa kiongozi anayepishana na Katiba ya nchi.

Ukimsikiliza Mabeyo kwa kina na kutafakari, unaweza kubaini kuwa Tanzania ina viongozi kwenye nafasi nyeti kabisa, wanaochukulia Katiba kitu cha kuchezea.

Imepita miaka mitatu tangu kifo cha Magufuli, vilevile imeshatimu miezi 36 Rais Samia akiwa madarakani, kwa maana hiyo, yameshakatika majuma 156, tangu sakata hili litokee, hakuna hatua mahsusi ambazo zimeshachukuliwa dhidi ya hao waliotaka kujaribu kuvunja Katiba kwa makusudi.

Maelezo ya Mabeyo yanaweza kukaribisha maswali mengi. Mathalan, alisema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Bashiru Ally, waliitwa haraka Dar es Salaam wakitokea Dodoma. Halafu Samia, Makamu wa Rais, aliyekuwa Tanga, aliachwa.

Makamu wa Rais, mbali na kuwa msaidizi na mshauri wa Rais, ukisoma vizuri Katiba, ibara ya 37, ibara zake ndogo hasa 2, 4 na 5, pamoja na vipengele vyake, kwa usahihi kabisa Makamu wa Rais yupo kama Rais wa akiba.

Kama ilivyo kwenye mpira, wachezaji wa akiba wanakuwepo na wanatumika pale waliopo uwanjani wanapoumia, wanapochoka au yanapohitajika mabadiliko ya kimfumo.

Makamu wa Rais ni Rais wa akiba, na hushika madaraka ya urais pale Rais anapokuwa nje ya mipaka ya nchi na anapougua.

Makamu wa Rais hurejesha mamlaka kwa muhusika anaporejea ndani ya mipaka ya nchi au anapopona maradhi yaliyokuwa yanamsumbua.

Makamu wa Rais hula kiapo na kuwa Rais kamili, ikiwa kiti cha Rais kitabaki wazi, kwa kifo, kujiuzulu, kuondolewa na Baraza la Mawaziri kwa kushindwa kutimiza majukumu yake au kushtakiwa na Bunge.

Kwa mujibu wa Mabeyo, Magufuli aliumwa. Samia, Makamu wa Rais, alikuwepo ndani ya mipaka ya nchi. Kwa maana hiyo, kipindi chote cha maradhi ya Magufuli, nchi ilipaswa kuwa inaongozwa na Samia. Katiba, ibara ya 37, inakataza mtu mwingine yeyote kukaimu urais, ikiwa Makamu wa Rais yupo ndani ya mipaka ya nchi na ni mzima kiafya.

Mantiki kuwa Makamu wa Rais ni Rais wa akiba, inaanza kwenye uchaguzi. Mgombea urais anakuwa na mgombea mwenza.

Sasa, ukiukwaji mkubwa Katiba ulianza tangu Magufuli akiwa anaumwa. Je, nchi ilikuwa inaongozwa na nani? Halafu swali kubwa, iweje Majaliwa na Bashiru waliitwa Dar es Salaam haraka, halafu Samia akaachwa Tanga?

Makamu wa Rais ndiye anakuwa na mamlaka ya kutangaza kifo cha Rais. Na wakati akitoa tangazo, anakuwa Kaimu Rais. Ilikuwaje Makamu wa Rais hakuwa karibu na mgonjwa, kujua maendeleo yake hatua kwa hatua hadi kifo? Kifo cha Magufuli hakikuwa cha ghafla. Aliumwa. Aliyepaswa kuhutubia Taifa na kuwaeleza wananchi kuwa Rais wao ni mgonjwa, aliwekwa mbali.

Mabeyo, Mkuu wa Majeshi, alifanya vizuri kuhakikisha Katiba inaheshimiwa. Hata hivyo, aliyoyaeleza yanaleta maswali mengi.

Kwamba Magufuli akiwa mgonjwa kabisa, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, ndiyo waliokuwa jirani. Makamu wa Rais na Waziri Mkuu walikuwa mbali.

Haishangazi kuona kuwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu walitoa kauli zenye kusigana kuhusu afya ya Magufuli, nyakati za mwisho za uhai wa Rais huyo wa tano.

Kumbe waliwekwa mbali. Hili nalo ni ukiukwaji mkubwa wa Katiba. Ni kweli Mkuu wa Majeshi, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa na Inspekta Jenerali wa Polisi ni wasaidizi wa Amiri Jeshi Mkuu.

Hata hivyo, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, ndiyo wasaidizi wa karibu zaidi wa Rais.

Ilinong’onwa mapema kuwa Jeshi la Wananchi (JWTZ), chini Mabeyo ndilo lililoulinda urais wa Samia, wengine walitaka kusaliti Katiba.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, katika hotuba yake ya mwaka 1969, alisema kuwa JWTZ ni mali ya wananchi na hakuna ambaye atakuwa kulichezea kwa masilahi yake. Mwalimu Nyerere alisema, uasi wa jeshi mwaka 1964 ilikuwa aibu ya mara moja na haitajirudia tena.

Mabadiliko ya uongozi kutoka Magufuli hadi Samia, ni dhahiri Mwalimu Nyerere alisema kweli. Utii wa Katiba jeshini ni mkubwa.