Prime
Kauli ya Dk Saada Mkuya na madai ya ACT – Wazalendo
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu ambaye ni Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar, Dk Saada Mkuya
Muktasari:
- Katika nyakati mbalimbali wakati wa uandikishaji wa wapigakura, viongozi wa chama hicho walidai hadharani kwamba, baadhi ya wanaoandikishwa kupiga kura si Wazanzibari, bali wapo wengine wanaopata fursa hiyo kutoka nje ya Zanzibar ambao hupewa vitambulisho hivyo kwa madai ya kusaidia kuongeza idadi ya kura.
Kwa muda mrefu kumekuwapo na malalamiko pamoja na hoja kubwa iliyokuwa ikijadiliwa Zanzibar kabla na baada ya uchaguzi wa Oktoba 2025. Hoja hiyo ilitolewa na baadhi ya wananchi hususan wa chama kikuu cha upinzani Zanzibar, ACT - Wazalendo.
Katika nyakati mbalimbali wakati wa uandikishaji wa wapigakura, viongozi wa chama hicho walidai hadharani kwamba, baadhi ya wanaoandikishwa kupiga kura si Wazanzibari, bali wapo wengine wanaopata fursa hiyo kutoka nje ya Zanzibar ambao hupewa vitambulisho hivyo kwa madai ya kusaidia kuongeza idadi ya kura.
Walidai kuwa hali hiyo ni mojawapo ya njia zinazoweza kuchochea au kuleta machafuko.
Tuhuma hizo mara nyingi zilielekezwa katika Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), ilidaiwa kuwa inafanya hivyo kwa kushirikiana au kutekeleza matakwa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ili kukiwezesha kushinda katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 2018, katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa kumchagua Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani, iwapo mwananchi ambaye si Mzanzibari hana kitambulisho cha Mzanzibari Mkazi (ZAN ID), lakini anacho kitambulisho cha Taifa na kadi ya mpiga kura, anaruhusiwa kupiga kura ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pekee.
Hata hivyo, haruhusiwi kupiga kura katika nafasi nyingine za Rais wa Zanzibar, Wawakilishi, Ubunge na Udiwani. Madai hayo yalielekezwa pia kwa masheha, pamoja na Tume ya Uchaguzi na Chama cha Mapinduzi.
Licha ya kuwapo kwa madai na tuhuma hizo, mara kadhaa ZEC na CCM wamekuwa wakizikanusha wakisema ni taarifa za upotoshaji zinazolenga kuibua taharuki.
Hata katika uchaguzi uliomalizika Oktoba 29, 2025, kuanzia mchakato wa kuboresha daftari la wapigakura katika awamu ya kwanza na ya pili, malalamiko hayo yaliendelea kuwapo, lakini yamekanushwa na kuelezwa kuwa hayana uhalisia bali ni propaganda.
ZEC ilieleza kuwa mchakato mzima ulifanyika kwa mujibu wa sheria na kwamba, wote walioandikishwa walikidhi vigezo vinavyotakiwa kisheria. Ilithibitisha kuwa jumla ya wapigakura waliosajiliwa ni 717,557, huku 8,325 wakiondolewa kwenye daftari la wapigakura. Hata hivyo, hivi karibuni imeonekana kana kwamba baadhi ya madai hayo yamethibitishwa kwa namna fulani na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu ambaye ni Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar, Dk Saada Mkuya, alipokuwa akijibu maswali katika Baraza la Wawakilishi wakati wa mjadala wa bajeti.
Katika mjadala huo uliosababisha hisia tofauti miongoni mwa wananchi, hasa kuhusu suala la ubaguzi, Dk Saada alizungumzia uwepo wa watu wanaopata vitambulisho vya Mzanzibari Mkazi kimakosa na kuelekeza lawama kwa masheha akisema wao ndio wanaohusika na utoaji usio sahihi wa vitambulisho hivyo.
Alifafanua kuwa kadi za matibabu zinapaswa kutolewa kwa Wazanzibari pekee, lakini katika hali halisi, hutolewa pia kwa watu wasiokuwa Wazanzibari.
Kwa mujibu wa utaratibu, mwananchi huwasilisha taarifa zake kwa sheha wa shehia husika, kisha hupatiwa kitambulisho cha Mzanzibari Mkazi na baadae hupewa huduma zinazohusiana na kadi hizo.
Mchakato wa kupata kitambulisho cha Mzanzibari Mkazi huanzia kwa sheha, kisha taarifa hupelekwa katika ofisi za usajili kwa ajili ya uchapishaji wa vitambulisho.
Hivyo, Dk Saada alieleza kuna watu wasiokuwa Wazanzibari hupata vitambulisho hivyo kimakosa na akashangazwa na namna hali hiyo inavyotokea, akisisitiza kuwa masheha wanapaswa kuwajibika kwa uaminifu katika mchakato huo.
Kutokana na kauli hiyo, licha ya kuwa Waziri Saada hana mamlaka ya moja kwa moja ya kusimamia suala hilo, mara nyingi kauli za mawaziri huchukuliwa kama msimamo wa Serikali, hususan wanapojibu maswali bungeni au katika Baraza la Wawakilishi.
Katika Baraza la 11, Dk Saada amekuwa akijitokeza mara kadhaa kutoa ufafanuzi katika wizara mbalimbali, jambo linalofanya majibu yake kuchukuliwa kama msimamo rasmi wa Serikali katika mijadala ya kisera.
Hapa ndipo hoja inapoibuka kuwa kauli ya Waziri inaonekana kama imethibitisha kuwapo kwa changamoto katika utoaji wa vitambulisho vya ZAN ID bila kufuata kikamilifu misingi na taratibu, kama ilivyokuwa ikidaiwa na ACT -Wazalendo.
Bila kujali ukweli wake, kauli hiyo ikitolewa na Waziri mwenye uzoefu mkubwa serikalini, inaiweka Serikali katika nafasi nyeti na kuipa nguvu zaidi ACT - Wazalendo katika hoja zake za hadharani, hivyo kufanya madai yao kuhusu watu wasio na sifa kusikika kwa nguvu zaidi. Ingawa kitaalamu ZEC ndiyo yenye mamlaka ya mwisho ya kuthibitisha sifa za mpiga kura, kauli ya Waziri inapaswa kuchunguzwa kwa kulinganisha na takwimu rasmi na sheria za uchaguzi zilizopo.
Kwa ujumla, kauli ya Waziri inaweza kuonekana kuunga mkono hoja za ACT - Wazalendo kisiasa, lakini si lazima iwe uthibitisho wa moja kwa moja wa kisheria wa madai hayo.