Bajeti Kuu ya Zanzibar ya Sh8 trilioni yapita
Muktasari:
- Katika michango ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walionesha wasiwasi wa deni hilo kwamba limekuwa kubwa hivyo mzigo huo utakwenda kulipwa na wananchi.
Unguja. Bajeti Kuu ya Serikali Zanzibar imepitishwa, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Juma Malik akisisitiza Serikali kuendelea kukopa lakini deni hilo italilipa yenyewe na sio mwananchi kama inavyoelezwa.
Bajeti ya Serikali iliyopitishwa leo Juni 18, 2026 na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni Sh8 trilioni huku deni la Taifa likifikia Sh3 trilioni.
Hata hivyo, Bajeti hiyo imepita bila kuwemo wawakilishi wa Chama cha ACT Wazalendo ambapo baada ya kumalizika michango ya wajumbe wa baraza na kuanza kutolewa ufafanuzi wa baadhi ya hoja na mawaziri wa kisekta, walitoka nje kila mtu kwa wakati wake.
Mwananchi lilipomtafuta mnadhimu wa chama hicho ndani ya baraza, Profesa Omar Fakih Hamad, baada ya kuahirishwa Baraza, simu yake imeita bila kupokewa na alipotumiwa ujumbe mfupi hakujibu.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakiwa wamenyoosha mikono wakato wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali baada ya kuulizwa na Spika wa Baraza, Zuberi Maulid wanaounga mkono hoja kupitisha bajeti hiyo
Waziri Malik wakati akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa siku tatu wakichangia bajeti hiyo, amesema Serikali ya awamu ya nane ikiondoka madarakani mwaka 2030 hakuna deni lolote litakalobaki.
Licha ya kujibu hoja hizo kwa ujasiri, Waziri huyo ameweka wazi kwamba zilikuwa zikimkosesha usingizi akiwapongeza baadhi ya mawaziri ambao wamemsaidia kujibu baadhi ya hoja hizo akisema wamerahisishia kazi.
“Hoja zilizitolewa hapa Barazani zilikuwa zinanikosesha usingizi, lakini leo nashukuru mawaziri na naibu mawaziri kujibu hoja nyingi na mimi kazi yangu itakuwa nyepesi, imekuwa kama timu ya mpira,” amesema.
Akifafanua kuhusu hoja hizo Waziri Malik amesema; “Zimetolewa hoja hapa kwamba deni la Taifa ni mzigo kwa wananchi, hakuna mwananchi atakayelipa deni la Serikali. Serikali imeweka utaratibu mzuri kulipa deni hilo na Serikali ya awamu ya tisa ikiingia madarakani haitakuta deni, lolote.”
Dk Malik amesema, hata ikitokea ukafika mwaka 2030 bado kukawa na deni, kutokana na mikopo mingine kuwa ya muda mrefu, lakini kutakuwa na utaratibu mzuri wa kulipa maana tayari fedha hizo zinatengwa ambapo kwa mwezi zinatengwa Dola za Marekani 20 milioni kwa ajili ya deni hilo.
Kuhusu kuzikopesha taasisi za ndani, Waziri huyo amesema ni utaratibu wa kuendelea kukuza taasisi hizo kwani inapolipa inaongeza na riba.
Akizungumza kuhusu deni la ndani, amesema kwa asilimia 50 ya deni hilo linatokana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo inashea za Serikali.
Waziri Malik amesema bila kujali wanakopa, lakini uchumi wa Zanzibar unakua na ndio kinachotakiwa kwani duniani kote Serikali inalenga kukuza uchumi wake.
Amesema wataendelea kukopa na kuondokana na bajeti zenye utegemezi na kwa sasa Zanzibar ipo katika mwelekeo huo ambao bajeti yake kwa miaka mitatu ya kifedha bajeti yake inazidi kupunguza utegemezi kutoka asilimia sita mwaka 2024 hadi asilimia 2.8 mwaka 2026/27.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma akizungumza wakati akichangia mjadala wa bajeti Kuu ya Serikali
Kuhusu misamaha ya kodi ambayo imechangiwa kwa hisia na baadhi ya wajumbe, Dk Malik amesema kabla ya kuitoa wanafanya tathimini na inayotolewa inakidhi vigezo.
“Ukiona umetolea msamaha wa kodi basi umekidhi vigezo vilivyowekwa, kwa hiyo tathimini inafanyika na hakuna kinachofanyika bila kuzingatia tija na matakwa,” amesema.
Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Hamad Omar Bakar amesema bajeti hiyo imezingatia vigezo vyote na imewahusisha wananchi tofauti na inavyozungumzwa.
“Hii ni bajeti nzuri na imezingatia vigezo vyote, wanaosema haimjali mwananchi sijui wanazungumzia kitu gani, jambo la msingi hapa ni kusimamia haya yaliyomo,” amesema.
Naye Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff akizungumza kuhusu misamaha ya kodi kwa wawekezaji, amesema imeleta tija kubwa kwani wasipofanya hivyo wawekezaji watakimbia kwenda nchi zingine.
Waziri huyo amesema hatua hiyo ni nyenzo muhimu katika kukuza uwekezaji na uchumi kwa ujumla kwani kinachotolewa msamaha ni kidogo ikilinganishwa na faida inayopatikana.
“Vipi utavutia wawekezaji bila kuweka mipango mizuri, tukumbuke kuna ushindani usipoweka mazingira mazuri hakuna atakayekuja kwako. Leo mtu anasamehewa kodi ya forodha Dola milioni tano anakuja na mtaji dola milioni 25 sasa unaangalia hapa kipi bora,” amesema.
Amefafanua kuwa wamechukua maeneo sita ambapo kuna mtaji wa Dola za Marekani 735 milioni na kuzalisha ajira 5,000.