Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pengo kukosekana sheria ya bajeti Zanzibar latajwa

Kaimu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Shariff Ali Shariff akijibu maswali barazania

Muktasari:

  • Pamoja na mambo mengine, sheria hiyo ingetambua na kutaja majukumu na mipaka ya wahusika mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kamati ya bajeti ya Baraza la Wawakilishi na wadau wengine.


Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekiri kuwapo pengo la kutokuwepo kwa sheria mahususi ya bajeti kwa muda mrefu inayoongoza usimamizi wa mzunguko mzima wa bajeti.

Pamoja na mambo mengine, sheria hiyo ingetambua na kutaja majukumu na mipaka ya wahusika mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kamati ya bajeti ya Baraza la Wawakilishi na wadau wengine.

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi, Juni 18, 2026 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Juma Malik Akil wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Paje, Jaku Hashim Ayoub (CCM) aliyeuliza sababu za kutotungwa kwa sheria ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria.

Jaku amesema kukosekana kwa sheria hiyo kunawafanya wahusika katika mzunguko wa bajeti, kutoonekana majukumu, mipaka na utendaji wao   bayana, akitolea mfano kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi na wahusika wengine katika mzunguko.

“Kwa kuwa mabunge mengi yamekuwa na sheria ya bajeti inayoonesha ufanisi wa namna ya mzunguko wa bajeti unavyofanya kazi na kusimamiwa bayana, ni kwa sababu gani za msingi sheria hiyo haitungwi kwenye Baraza letu la Wawakilishi,” amehoji.

Akijibu swali hilo,  Waziri Malik amesema wizara kwa sasa inafanya mapitio kikamilifu katika uundaji wa mfumo kwa kuangalia kasoro za kisheria zilizopo katika sheria ya usimamizi wa fedha za umma Nambari 12 ya 2016.

“Mchakato huu umehusisha mapitio ya ndani katika wizara, ushauriano ya wadau, na kuangalia sheria zilizopo za usimamizi wa fedha za umma na za kibajeti katika ukanda wa Afrika Mashariki ili kuhakikisha sheria mahususi ya bajeti itakayopendekezwa mwisho inashughulikia vyema mapengo,” amesema Dk Malik.

Hata hivyo, amesema licha ya kutokuwepo kwa sheria inayosimamia mzunguko mzima wa bajeti, Serikali imekuwa ikiutekeleza kwa kutumia Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma Nambari 12 ya mwaka 2016.

Amesema sheria hiyo kwa kiasi kikubwa ina sehemu mbili zenye vifungu zaidi ya 16 vilivyoweka mfumo wa kisheria unaoshughulikia usimamizi na mzunguko wa bajeti pamoja na kanuni ya fedha ya mwaka 2021.

Hoja hiyo pia imezungumzwa na Mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad (ACT -Wazalendo) ambaye amesema lazima Zanzibar iwe na sheria ya bajeti kwa kuwa ni muda mrefu wanaelezwa itatungwa na haitungwi.