Wawakilishi waibana Serikali kwa ongezeko la misamaha ya kodi
Mwakilishi nafasi za Wanawake, Moza Mohamed Khamis akichangia mjadala wa Bajeti ya Serikali Barazani Chukwani Unguja Zanzibar.
Muktasari:
- Jumla ya maombi 475 ya misamaha ya kodi yaliwasilishwa, kati ya hayo maombi 365 yalikidhi vigezo.
Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameeleza masikitiko yao kuhusu mwenendo wa Serikali wa kuendelea kutoa misamaha mingi ya kodi, wakati ikipanga bajeti kwa kutegemea mapato ya ndani.
Wamesema hatua hiyo inachangia kupotea kwa kiasi kikubwa cha fedha za umma kupitia taasisi na makundi ambayo, kwa maoni yao, hayastahili kunufaika na misamaha hiyo.
Hayo yamebainishwa leo, Juni 2026, ikiwa ni siku ya pili ya kujadili Bajeti Kuu ya Serikali barazani Chukwani, Unguja, Zanzibar. Bajeti hiyo ilisomwa Juni 11, 2026, na Serikali iliomba kuidhinishiwa Sh8.5 trilioni.
Alipowasilisha bajeti hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Juma Malik Akil, alisema jumla ya maombi 475 ya misamaha ya kodi yalipokewa na kati ya hayo maombi 365 yalikidhi vigezo.
Akichangia hoja hiyo, mwakilishi wa nafasi za wanawake (ACT Wazalendo), Moza Mohamed Khamis, amesema Serikali inategemea kodi kujiendesha, lakini inatoa misamaha ya kodi hata kwa taasisi zinazofanya biashara kubwa na zenye uwezo wa kulipa kodi na kuchangia mapato ya Serikali.
“Hii misamaha ni mikubwa na imekuwa mingi. Hatuwezi kufikia kile tunachotaka katika mfumo huu wa misamaha ya kodi. Kuna wakati mwingine hata baadhi ya hoteli zinapewa msamaha ilhali zinaingiza mapato makubwa.
“Kutoa misamaha si vibaya, lakini ni vyema ikaangaliwa tunatoa misamaha hiyo kwa utaratibu upi. Taasisi kama za elimu na nyingine ambazo zinaleta vifaa kwa ajili ya kuwagawa wananchi au kusaidia huduma ndizo ziangaliwe, na si kutoa misamaha ya kodi kwa taasisi zinazojiweza wakati tunataka kuongeza mapato,” amesema.
Pia, mwakilishi huyo amesema Serikali inatumia fedha kukopesha taasisi za umma ilhali taasisi hizo zinatakiwa kutengeneza faida na kuisaidia Serikali.
Amesema iwapo kutakuwa na mipango na mikakati mizuri, fedha nyingi zinazopotea zinaweza kuokolewa, na Serikali haitalazimika kuendelea kukopa na kuongeza gharama za madeni yatakayolipwa na wananchi.
Katika bajeti hii, Serikali imetenga zaidi ya Sh200 bilioni kwa ajili ya kuzikopesha taasisi za Serikali.
“Katika maeneo mengi duniani na mataifa yaliyoendelea, mashirika ndiyo yanaisaidia Serikali kwa kutoa gawio, lakini hapa kwetu imekuwa kinyume chake, Serikali ndiyo inazikopesha taasisi hizo,” amesema.
Kwa mujibu wa mwakilishi huyo, fedha hizo zingeweza kuelekezwa katika maeneo mengine.
Kuhusu miradi ya kimkakati inayokopeshwa fedha lakini isiyotarajiwa kurejesha faida yoyote, amesema huenda ikaacha mapengo makubwa ya madeni kwa wananchi na kuitaka Serikali kuwashirikisha wananchi wakati wa kuandaa miradi hiyo.
Naye Mwakilishi wa Kiembesamaki, Abdulla Kambotwe Abdulla (CCM), amesema ni jambo jema kutoa misamaha ya kodi, lakini kiwango cha Sh280 bilioni za misamaha ya kodi zilizotolewa katika mwaka wa fedha unaomalizika ni kikubwa.
Amehoji iwapo Serikali imefanya tathmini ya kutosha kwa kuangalia misamaha hiyo imezalisha tija kiasi gani katika muktadha wa uwekezaji na uzalishaji wa ajira, na kwa kipindi cha miaka mitano imechangia kwa kiwango gani katika kukuza uchumi.
“Kwa hiyo ningeomba kujua na kuona namna gani tumepiga hatua kutokana na misamaha ya kodi. Isije ikawa pengine inatolewa, lakini hakuna tathmini yoyote inayofanyika,” amesema.
Amesema licha ya kuwapo taarifa za kuwa na miradi mingi ya uwekezaji, inashangaza kuona bado kuna malalamiko kuhusu ajira.
Naye Mwakilishi wa Ziwani, Mohamed Ali Salim (ACT Wazalendo), amesema inatia shaka kuona misamaha inatolewa kwa watu wakubwa, ilhali wenye kipato cha chini hawanufaiki nayo.
“Hizi fedha zingetosha kuendesha miradi ya Serikali. Hatuoni sababu ya kuendelea kutoa misamaha ya kodi inayopunguza mapato ya Serikali. Kinachotokea ni kupoteza fedha nyingi, kisha tunawabana wananchi wa mwisho,” amesema.
Amesema Serikali inapoongeza kodi kwenye magari, anayeumia si mfanyabiashara bali ni mtumiaji wa mwisho.
“Inasikitisha sana kuwa bajeti haikueleza vyanzo vipya vya mapato. Tumeendelea kutumia vyanzo vilevile na kuongeza kodi. Tunatakiwa kubuni vyanzo vipya na kuwasaidia wanyonge,” amesema.